Yatakayokupata usipodhibiti minyoo inayoshambulia mwili wako

September 5, 2020 6:38 am · Joshua
Share
Tweet
Copy Link
  • Minyoo iliyokomaa huishi katika utumbo na huzalisha mayai zaidi ya elfu 1,000 kila siku. 
  • Hudhoofisha afya ya binadamu na kumfanya ashambuliwe kirahisi na magonjwa. 
  • Unashauriwa kunywa dawa ya kuzuia minyoo kila baada ya miezi mitatu au mara tatu kwa mwaka.

Niko mtaani katika shughuli zangu za kila siku. Nakutana na baadhi ya watu ninaowafahamu ambao ni rafiki zangu. Wako katika mazungumzo kuhusu masuala ya afya. 

Katika mazungumzo hayo, mtu mmoja anasema yeye hajawahi kuhisi minyoo kama ni tatizo la kutisha na wala hakumbuki mara ya mwisho alikunywa dawa ya minyoo lini. 

Anaenda mbali kwa kusema afya yake itakua ni imara sana kuliko kawaida. Akili yangu kama mtaalamu wa afya na nafsi yangu ikakinzana kabisa na mwili wangu ambao wakati huu kutokana na uchovu ulikua unatamani kufika nyumbani na kupumzika tu. 

Lakini hatia yangu ya kitaaluma ikanisukuma nikae kidogo na kuwapatia elimu hii mujarabu ndugu zangu hawa. Basi ikawa hivi:

Maambukizi ya minyoo kupitia udongo ni moja kati ya maambukizi yaliozoeleka ulimwenguni na huathiri zaidi nchi zenye uchumi wa chini na zile zisizopewa kipaumbele. 

Minyoo huu huambukiza kupitia mayai ambayo mara nyingi huwa katika kinyesi cha binadamu ambacho huingiliana na kuchafua udongo katika maeneo ambayo viwango vya usafi na mazingira ni duni. 

Minyoo inayotambulika na iliyozoeleka ni pamoja na “Ascaris lumbricoides”, “Trichiura na Necator americanus”.

Kwa  mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watu bilioni 1.5 hupatwa na maambukizi ya minyoo ya matumbo huku zaidi ya watoto 267 milioni walio chini ya umri wa miaka mitano na watoto milioni 568 walio katika umri wa kwenda shule ya msingi huishi katika mazingira  ambayo maambukizi yake ni ya viwango vya juu. 

Inakadiriwa kuwa watu 600 milioni duniani wana maambukizi ya minyoo ya minyoo ya matumbo.

Hudhoofisha afya ya binadamu na kumfanya ashambuliwe kirahisi na magonjwa. Picha|Mtandao

Mtu anapataje minyoo

Minyoo hawa huambukiza hasa kupitia mayai ambayo hupitishwa katika kinyesi cha watu wenye maambukizi. Minyoo iliyokomaa huishi katika utumbo na huzalisha mayai zaidi ya elfu 1,000 kila siku. 

Katika maeneo yenye mfumo duni wa usafi wa mazingira na mifumo ya maji mibovu, mayai haya huingia katika ardhi. 

Hii huweza tokea iwapo, mayai haya yanapokua yamejishikiza kwenye mboga mboga na kisha zikaliwa bila kuoshwa, kupikwa au kumenywa vizuri. 

Pia mayai humezwa ndani ya mwili kwa kunywa maji yaliyotoka kwenye vyanzo vilivyochafuliwa au kumezwa na watoto wanaochezea udongo na kuweka mikono midomoni bila kuiosha.


Zinazohusiana:


Athari zake kwa afya ya binadamu

Minyoo hii ina athari kubwa katika mfumo lishe. Mosi, minyoo hii iko katika mfumo wa tishu za binadamu ambapo hujipatia chakula kwa kula tishu hizi ikiwemo damu.

Hali hiyo husababisha upotevu wa madini chuma na protini ambayo matokeo yake ni kupungua kwa damu hasa kwenye utumbo.

Pili, minyoo hii husababisha kutokufyonzwa ipasavyo kwa madini na chembe za lishe, jambo linalosababisha kuzorota kwa shughuli za ujenzi wa mwili. Baadhi ya minyoo hii humfanya mtu akose hamu ya kula na hivyo kuzoofika.

Kawaida maambukizi madogo ya minyoo hayaonyeshi athari. Lakini maambukizi yanapokua makubwa husababisha kuzibwa kwa njia ya utumbo, uchovu, maumivu makali ya tumbo, kuharisha na changamoto za kukua kwa watoto.

WHO na watalaam wa afya wanapendekeza watu kutumia dawa za minyoo walau mara tatu kwa mwaka au kila baada ya miezi mitatu. Watoto wanaoishi katika mazingira yenye hatari na maambukizi makubwa ya minyoo wanapaswa kupewa kipaumbele kwa kupatiwa dawa hizi ili kuondosha minyoo katika miili yao.

Dk Joshua Lameck Sultan ambaye kitaaluma ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) na Mkurugenzi wa Indigo Afya. Hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.

Enable Notifications OK No thanks