Unataka kusafiri nje ya nchi? Jiweke tayari kwa mambo haya

June 26, 2019 7:21 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Andaa nyaraka muhimu ikiwemo pasipoti, viza, cheti cha hali ya afya yako. 
  • Fanya utafiti wa kina wa nchi unayoenda ikiwemo kujua tamaduni za wenyeji wako.
  • Hakika umejiunga na mfumo wa kimataifa wa malipo (Credit Card).

Kusafiri nje ya nchi, iwe kwa ajili ya masomo, kazi au biashara ni jambo linaloleta furaha na amani ya moyo hasa kama safari husika inafungua fursa mpya ya maisha kwa msafiri. 

Lakini ili ndoto yako itimie, unahitaji maandalizi. Kila nchi ina utaratibu na sheria zake zinazosimamia safari za wageni wanaoingia kwenye nchi zao. Ni lazima ufahamu na ufuate mchakato ili kuepuka usumbufu. 

Yapo mambo ya msingi yanayofanana karibu katika nchi zote unayopaswa kuzingatia au kujiandaa kabla hujaanza safari nje ya nchi.

Tafuta au kagua pasipoti yako

Kama hauna pasipoti ni wakati mwafaka wa kuitafuta kupitia mamlaka za uhamiaji zinazohusika na utoaji wa pasi hizo za kusafiria. Pasipoti ni nyaraka muhimu ya kusafiria, unaweza kuikosa safari yako kama hauna pasipoti.

Lakini kama unamiliki pasipoti, ni  vema kuangalia muda wake wa matumizi kama umeisha ili kuihuisha. Zipo nchi zinataka uhai wa pasipoti usipungue miezi sita kabla ya muda wake kuisha. 

Kwa muktadha huo, itakupasa kutathmini ni muda gani unaenda kukaa nje na uhai wa pasipoti yako.


 Zinazohusiana:


Omba viza (Visa Application)

Ukipata pasipoti, angalia masharti mengine ya kuingia katika nchi unayokwenda. Unahitaji kupata viza au kibali cha kuingia katika nchi husika ambayo hutolewa na maafisa wa ubalozi wanaoziwakilisha nchi zao. 

Ni muhimu kusoma masharti ya viza utakayopewa kwasababu yanakupa picha ya mambo ya kuzingatia katika nchi unayokwenda.

Kwa mfano, ikiwa unaomba viza ya wanafunzi nchini Uingereza, utahitaji kutoa nakala ya barua yako kutoka Chuo unachoenda kusoma na kuthibitisha kuwa una fedha za kutosha kujiunga wakati wa masomo yako. 

Viza ni muhimu hasa kama unasafiri katika nchi zilizoendelea. Picha|Mtandao. 

Fanya utafiti wa kina

Fanya utafiti wa kina unakokwenda hata kama una taarifa za nchi husika. Jipe muda tena wa kujua mambo kadhaa ya nchi hiyo. Utafiti unaweza kuwa katika maeneo ya kujua taratibu na maisha ya wenyeji wako unakoenda kuishi na jinsi gani unaweza kuendana nao.

Lugha, utamaduni wao na aina ya chakula ni sehemu ya masuala muhimu ya kuayafanyia utafiti. Unaweza ukaenda nchi ambazo chakula chao ni mboga mboga tu wakati huku Tanzania umezoea kula ugali maharage au viazi vitamu ili ushibe vizuri. 

Kama huwezi kuendana na chakula cha nchi husika hakikisha unatafuta migahawa inayopika chakula cha asili ya Afrika au China angalau unaweza kupata wali, ndizi na kuku.

Jiunge mfumo wa mawasiliano, malipo wa kimataifa

Unaweza ukawa n akaunti ya benki pamoja na kadi ya kutolea pesa (ATM Card) hakikisha zote zimeunganishwa na mifumo ya kimataifa ya malipo ili kurahisisha upatikanaji wa pesa ukiwa nje ya nchi. 

Kama unataka kufungua akaunti mpya katika benki za kimataifa, tafiti ni mahitaji gani unatakiwa kutimiza ili kukuhakikishia upatikanaji wa pesa wakati wote wa safari yako. 

Pia ni muhimu kuwa na mawasiliano ya uhakika ya simu. Unaweza kuwasiliana na kampuni ya simu, ukaunganishwa na huduma za kimataifa ili kukuwezesha kuwasiliana mahali popote duniani na kukupunguzia gharama za mawasiliano. 

Kadi za malipo za kielektroniki zinazokubalia kimataifa ni muhimu katika kurahisisha malipo ya bidhaa na huduma. Picha|Mtandao.

Nakala za nyaraka muhimu

Ni vema ukatoa nakala ya nyaraka zako muhimu ikiwemo cheti za kuzaliwa, pasipoti, kadi za benki n.k. Nakala hizo zitakusaidia na kukuondolea usumbufu inapotokea dharura au vikipotea.

Tathmini hali ya afya yako

Afya ndiyo kila kitu katika maisha yako. Kabla ya kusafiri tafuta ushauri wa daktari ili aangalia kama afya yako inaruhusu kusafiri masafa marefu na kuendana na hali ya hewa ya nchi unayoenda. 

Ni muhimu kupata chanjo. Shirika la Afya Duniani (WHO) linawataka wasafiri wote wa kimataifa kupata chanjo ya homa ya manjano kabla hawajaenda nje ya nchi. Fuatilia masharti ya kiafya ya nchi unayoenda ambayo unatakiwa kutimiza kabla hujaingia kwenye nchi husika.

Kama hiyo haitoshi, wapaswa kuwa na bima ya afya ya safari za kimataifa ambayo unaweza kuikata katika kampuni za bima nchini na bei yake siyo juu sana. Gharama za bima hiyo hutofautina na umri wa msafiri, historia ya magonjwa na masuala mengine ambayo kampuni husika ya bima itayotoa. 

Safari yenye mafanikio nje ya nchi hutegemea maandalizi mazuri na uelewa mpana wa unakokwenda.

Enable Notifications OK No thanks