Sarufi AI teknolojia ya akili bandia inayorahisisha mawasiliano

Lucy Samson 0644Hrs   Juni 22, 2023 Teknolojia
  • Ni teknolojia inayowezesha kuwasiliana na kuwahudumia wateja kwa urahisi.
  • Ni rahisi kutengeneza teknolojia hiyo bila msaada wa wataalamu wa kompyuta

Dar es Salaam. Kwa wamiliki wa kampuni zinazohudumia wateja wengi, suala la mawasiliano na wateja linaweza kuwa moja kati ya mambo muhimu wanayozingatia muda wote wawapo kazini.

Suala hilo huwalazimu kuajiri wafanyakazi wanapokea simu za wateja, kujibu maswali mbalimbali na kuwasaidia kupata baadhi ya huduma zinazotolewa na kampuni zao.

Lakini je, unafahamu kuwa sayansi na teknolojia inaweza kurahisisha mawasiliano na wateja wako bila kuhitaji kuajiri watu wengi wa kukusaidia?.

Nukta Habari leo inakukutanisha na teknolojia ya akili bandia (Sarufi AI) yenye uwezo wa kuwasiliana na kuwahudumia wateja kwa urahisi.

Sarufi AI ni nini?

Sarufi Ai ni teknolojia iliyobuniwa na kampuni ya kitanzania Neuro Tech Afrika inayobuni na kutengeneza bidhaa aina mbalimbali kwa kutumia akili bandia.

Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Kalebu Gwalugano, anasema alisukumwa kuanzisha kampuni hiyo mwaka 2022  kutokana na uhitaji uliopo wa kurahisisha mawasiliano na kutokuwepo kwa teknolojia hiyo nchini.

“Tukaona kwamba Tanzania kuna fursa ya kuanzisha  kampuni ambayo itawezesha mabadiliko kutoka kutumia programu tumizi za kawaida(app), nakuhamia kutumia hii mifumo ya kuwasiliana kwa soga(chatting) na wateja.

Ili kutumia programu hiyo ni lazima utengeneze roboti yako inayopatikana katika tovuti ya Sarufi, kisha unapakia taarifa zako ambazo zitasaidia roboti kujibu maswali kwa urahisi baada ya hapo unaweza kuweka roboti hilo kwenye tovuti yako au mahali ambapo wateja wanaweza kufikia kwa urahisi.


Soma zaidi


Kuhusu lugha, teknolojia hiyo imetengenezwa kuelewa lugha mbalimbali za kiafrika ikiwemo kiswahili ambazo mara nyingi hazitambuliwi na baadhi ya mifumo na teknolojia zinazobuniwa na nchi zilizoendelea.

Hata wakati lugha hizo zikitumika kuwasiliana na wateja mtengenezaji wa roboti hiyo ni lazima afahamu lugha ya kompyuta.

Kwa kutambua hilo Sarufi AI wamelazimika kurahisisha lugha ya kompyuta (coding language) ili kumuwezesha mtu yoyote kutumia teknolojia hiyo

“Kutumia Sarufi AI kutengeneza roboti itakayowezesha soga (chatting) na mteja ni rahisi tu, hata kama hujui lugha ya kompyuta (coding language) kuna namna rahisi unayoweza kuitumia kutengeneza roboti.

Ni mkombozi wa mawasiliano

Dakika kadhaa baada ya kutengeneza roboti hilo mtumiaji anaweza kuwasiliana na wateja moja kwa moja bila ulazima wa yeye kuwepo ofisini.

Mtumiaji anaweza kuuliza maswali, kuuliza kufahamu zaidi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na kampuni husika,kupewa namba ya malipo na kufikishiwa huduma moja kwa moja katika maeneo yao.

“Mfano tuna kampuni inayouza madawa kwa jumla wao wametumia Sarufi kutengeneza mfumo unaowasaidia wateja kuagiza madawa, kutuma risiti za malipo na kuwasaidia kupata taarifa mbalimbali za bidhaa,”ameongeza Kaleb.

Mbunifu  huyo anasema anasema kwa miaka ya baadae wanatazamia kuboresha zaidi mfumo huo ili kuwawezesha watumiaji kuunganisha mfumo huo na mitandao ya kijamii kama Whatsapp.

“Ni ngumu kidogo kwa mtumiaji wa kawaida kwa sasa ni lazima uwe na tovuti,  au uwe unajua lugha ya codding kwa miaka ya baadaye wanafikiria kuwezesha watumiaji kutumia kwenye Whatsapp kwa urahisi,”amesema.

Ikiwa unamiliki kampuni zaidi ya moja teknolojia hii itakuwezesha kutengeneza roboti atakayewezesha mawasiliano kulingana na mahitaji ya kampuni zote ulizonazo. Picha|Sarufi AI.

Vijana kunufaika zaidi

Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia yanayoendelea kupiga hatua duniani kote Kaleb anasema kampuni yake haifanyi mauzo pekee lakini pia inawekeza zaidi kwa vijana kuhakikisha wanakuwa sehemu ya gunduzi za akili bandia zinazoendelea.

"Mimi muda wangu nautoa kwa vijana, natembelea vyuo na kuongea nao, ikiwa kuna msaada wowote nawapatia ili kuendelea kuhamasisha uvumbuzi wa teknolojia mbalimbali za akili bandia,” amesema mtaalamu huyo wa teknolojia.

Kwa sasa wanafunzi  kutoka vyuo mbalimbali hutumia mfumo huo kutenegeneza gunduzi tofauti zinazowasaidia kufanya kazi za mazoezi zinazohitajika wakiwa mwaka wa mwisho chuoni.

Sambamba na hilo Kampuni hiyo inatarajia kuanzisha kablu za teknolojia katika kila chuo kilichopo nchini ili kuwafundisha wanafunzi namna ya kutumia akili bandia kutengeneza mifuminayorahisisha maisha na kujiongezea kipato.

Ajira zipo hatarini

Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti uliongazia athari za akili bandia kwenye ukuaji wa uchumi uliofanywa na taasisi ya Goldman Sanch iliyopo nchini Marekani, inakadiriwa kuwa watu 300 milioni wanatarajiwa kukosa ajira kutokana na matumizi ya akili bandia duniani.

Hata hivyo, ripoti hiyo imesema kwa watu watakaoamua kuwekeza katika matumizi ya teknolojia wanakadiriwa kuongeza uzalishaji maradufu na mapato kwa ujumla.

“Tunakadiria kuwa akili bandia (AI) inaweza kuongeza pato la taifa la kila mwaka kwa asilimia saba duniani kote,” imesema ripoti hiyo iliyotolewa Machi 26, 2023. 

Ikiwa unataka kujifunza zaidi kuhusu teknolojia hii ya akili bandia unaweza kuwasiliana nasi www.nukta.co.tz , tupigie 0677 088 088 au wasiliana na Kaleb Gwalugano kwa namba 0757 294,146.

Related Post