Twitter kuwawekea watumiaji wake muonekano mpya

Mwandishi Wetu 0659Hrs   Julai 16, 2019 Teknolojia
  • Muonekano huo utarahisisha matumizi ya mtandao huo hasa katika kipengele cha ujumbe, orodha ya vitu na vitambulisho (Bookmarks).
  • Wanaotumia mtandao huo kwa nji ya kompyuta, sasa wanaweza kutumia akaunti zaidi ya moja. 
  • Hatua hiyo ni kuwapa kilicho bora watumiaji wa mtandao huo.

Baada ya kipindi cha majaribio cha miezi kadhaa ya muonekano mpya wa Twitter, mtandao huo umesema mwonekano huo uko tayari kutumika kwa wafuasi wake wote duniani. 

Twitter imekuwa ikifanya mabadiliko mbalimbali ili kuhakikisha inakidhi matakwa ya wafuasi wake na soko ili kuvutia matangazo yanayochangia kukuza mfuko wa mtandao huo kijamii. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa Twitter jana (Julai 15, 2019) imesema hiyo ni hatua kubwa ya kuendelea kuuboresha mtandao huo ili kuwahudumia watu kila siku.

“Maboresho haya pia yanatupa sisi msingi mzuri wa kuendelea kujenga ili kuleta mabadiliko ya haraka kuliko ilivyokuwa mwanzoni,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.


Zinazohusiana:Wafanyabiashara wanavyoweza kunufaika na kalenda ya Twitter


Mwonekano huo mpya kwa watumiaji wa kompyuta umekuja na faida kadhaa ikiwemo kuendelea kupata taarifa nyingi zaidi za kihabari na kwa urahisi zaidi ikiwemo picha za vedio na taarifa zaidi kutoka katika jamii ya mtumiaji.

Mabadiliko hayo yatasaidia mtuamiaji wa Twitter kutumia mtandao huo kwa urahisi hasa katika vipengele vya vitambulisho (Bookmarks),  orodha (Lists) pamoja na ‘Profile’ ya mtumiaji ambapo vipengele hivyo sasa vitaonekana kwa urahisi ukilinganisha na mwonekano wa mwanzo.

Pia muonekano huo mpya unamuwezesha mtumiaji kuona mazungumzo yote aliyoyafanya kupitia kipengele cha ujumbe mfupi wa maneno.

Sambamba na mabadiliko hayo mengine ni mtumiaji wa Twitter kwa kwa njia ya simu ataweza kuingia na kutoka kwa urahisi huku mtumiaji wa kompyuta atakuwa na uwezo wa kubadilisha akaunti za Twitter hata kama unazo zaidi ya moja pamoja na kupata mwonekano wa usiku maarufu kama ‘themes Dim and Lights’.

Mwonekano wa usiku maarufu kama ‘themes Dim and Lights’.Picha|Twitter

Related Post