TMA yatoa ushauri, tahadhari ujio mvua za vuli Oktoba

Daniel Samson 0738Hrs   Septemba 03, 2019 Ripoti Maalum
  • Mvua hizo za vuli ambazo huanza Oktoba hadi Desemba ni mahususi kwa maeneo ya nchi yanayopata vipindi viwili vya mvua kwa mwaka. 
  • Imesema baadhi ya maeneo hasa kanda ya Ziwa Victoria yatapa mvua nyingi, wananchi wanapaswa kujiandaa kwa kilimo.
  • Wananchi wa mikoa Pwani, Dar es Salaam na Tanga watakiwa kujiandaa kukabiliana na vipindi vya upungufu wa mvua.

Dar es Salaam. Wakati msimu mvua za vuli ukitarajiwa kuanza Oktoba mwaka huu, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeeleza mambo mbalimbali ambayo wananchi wanatakiwa kufanya ili kufaidika na mvua hizo ikiwemo kujiandaa vyema kwa shughuli kilimo na ufugaji.

Mvua hizo za vuli ambazo huanza Oktoba hadi Desemba ni mahususi kwa maeneo ya nchi yanayopata vipindi viwili vya mvua kwa mwaka ambapo hujumuisha mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria, Ukanda wa Pwani ya Kaskazini na Nyanda za juu Kaskazini Mashariki. 

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi aliyekuwa anatoa mwelekeo wa msimu za vuli za Oktoba hadi Desemba leo (Septemba 3, 2019) jijini Dar es Salaam, amesema mwenendo wa mvua katika kanda hizo tatu utatofautiana na hivyo tahadhari na mambo ya kufanya yanaweza kutofautiana. 

Dk Kijazi amesema maeneo yanayozunguka ukanda wa Ziwa Viktoria ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi ya ukanda huo. 

“Msimu wa mvua za vuli katika maeneo haya unatarajiwa kuisha kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Januari, 2020,” amesema na kuongeza kuwa maeneo machache ya mkoa wa Kagera mvua za nje ya msimu zinaendelea toka Agosti na zinatarajiwa kusambaa katika maeneo mengine ya ziwa Viktoria hadi kufikia wiki ya pili ya Oktoba.

Akizungumzia ukanda wa pwani ya askazini wenye mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Dk Kijazi amesema mvua katika maeneo hayo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani.

“Mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuanza katika wiki ya pili ya mwezi Oktoba ingawa mtawanyiko wake unatarajiwa kuwa hafifu. Vipindi virefu vya ukavu na mvua chache pia vinatarajiwa katika maeneo mengi ya ukanda wa pwani ya kaskazini,” amesema.

Hali kama hiyo ya mvua za wastani hadi chini ya wastani inatarajiwa kujitokeza katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara.

MWELEKEO WA MVUA ZA VULI (OKTOBA – DISEMBA), 2019


 Mambo ya kuzingatia wakati wa mvua za vuli

Katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani, upungufu wa unyevunyevu ardhini unatarajiwa kujitokeza na kusababisha upungufu wa malisho na maji kwa ajili ya mifugo jambo linaloweza kuibua migogoro kati ya wakulima na wafugaji. 

“Wafugaji wanahamasishwa na kushauriwa kuvuna mifugo yao ikiwa bado katika hali nzuri. Wafugaji pia wanashauriwa kutunza mifugo yao kwa kuzingatia ushauri kutoka kwa maafisa ugani katika maeneo yao,” amesema Dk Kijazi ambaye pia ni Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO)

Sekta ya uvuvi, katika maeneo hayo, inaweza kuathiriwa kutokana na upungufu wa maji katika mabwawa ya samaki na hivyo wafugaji wanashauriwa kuimarisha miundombinu ya ufugaji wa samaki na kuzingatia matumizi sahihi ya maji.

Amebainisha kuwa katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, shughuli za kawaida za kilimo zitaenda vizuri kwa sababu mvua zitakuwepo za kutosha. 

Hata hivyo, athari katika miundombinu na rasilimali maji inaweza kujitokeza katika maeneo yatakoyopata mvua nyingi hasa migodini ambapo wachimbaji wanashauriwa kuchukua tahadhari ya maporomoko ya ardhi. 


Soma zaidi: 


Sekta ya Afya na maafa zatakiwa kujipanga

Katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua nyingi matukio ya magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza, hali kadhalika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani magonjwa ya mlipuko pia yanaweza kujitokeza kutokana na uhaba wa maji safi na salama.  

“Ushauri unatolewa kwa mamlaka husika na jamii kuchukua hatua stahiki kupunguza athari za kiafya zinazoweza kujitokeza,” amesema Mkurugenzi Mkuu huyo wa TMA. 

Menejimenti za maafa zinashauriwa kuandaa mikakati ya kupunguza athari zinazoweza kujitokeza katika msimu wa mvua za Vuli 2019 ikiwemo uandaa mbinu za kukabiliana na mafuriko na vipindi vya ukavu, kama vile kuimarisha na kutenga rasilimali tayari kwa ajili ya kukabiliana na athari zinazoweza kijitokeza. 

Mabadiliko ya mifumo ya hali ya hewa

Dk Kijazi amesema kuwepo kwa tofauti ya mvua kunasababishwa na mifumo ya hali hewa hasa joto la bahari na mvumo wa upepo kuelekea nchi kavu. 

Maeneo ya pwani ya kaskazini pamoja na nyanda za juu kaskazini mashariki yanatarajia kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani kwa sababu hali ya joto la bahari la juu ya wastani katika maeneo ya kati mwa bahari ya Hindi, kusini-magharibi pamoja na kaskazini magharibi (pwani ya Somalia) mwa Bahari ya Hindi inatarajiwa kuendelea katika kipindi chote cha Oktoba hadi Disemba 2019. 

Hali hiyo inatarajiwa kusababisha mtawanyiko wa upepo kutoka katika pwani ya Tanzania kuelekea katikati ya Bahari ya Hindi, hivyo, kusababisha vipindi vya upungufu wa mvua katika maeneo ya pwani ya kaskazini pamoja na nyanda za juu kaskazini mashariki. 

Menejimenti za maafa zinashauriwa kuandaa mikakati ya kupunguza athari zinazoweza kujitokeza katika msimu wa mvua za Vuli 2019. Picha|Mtandao.

Kwa upande mwingine, joto la chini ya wastani linatarajiwa kuendelea kusini-mashariki mwa Bahari ya Atlantiki (karibu na pwani ya Angola) na hivyo inatarajiwa kuwepo kwa msukumo wa upepo wenye unyevunyevu kutoka katika misitu ya Kongo, na kusababisha mvua katika mikoa ya kanda ya Ziwa Victoria na maeneo jirani. 

Usahihi wa utabiri wa hali ya hewa

TMA imeeleza kuwa inatarajia kuona viwango vya utabiri wa msimu wa vuli unaoanza Oktoba vitakuwa sahihi kama vilivyotabiriwa ili kuwawezesha wananchi na mamlaka husika kupanga mipango na kufanya maamuzi sahihi katika maeneo yao. 

Mchambuzi wa Utabiri wa hali ya hewa kutoka TMA, Abubakar Lungo amesema kiwango cha usahihi wa utabiri wa msimu wa mvua za masika za Machi hadi Mei katika maeneo yanayopata vipindi viwili vya mvua ulikuwa asilimia 82.6 ukiwa umeshuka kidogo ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2018. 

Usahihi wa viwango vya utabiri vinategemea zaidi mabadiliko ya joto la bahari na upepo. Lakini pia changamoto za usafirishaji, upakiaji na usambazaji wa taarifa za hali ya hewa kutoka sehemu moja kwenda nyingine. 

Related Post