Temesa kuiteka Dar kwa taa za barabarani

February 23, 2021 11:03 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wakala wa Ufundi na Umeme umeanza kusimika taa za barabarani jijini humo.
  • Taa hizo zitasaidia kuongoza magari na umakini wa madereva wanapofika kwenye makutano ya barabara.
  • Barabara mbalimbali zitafaidika na mradi huo zikiwemo za Shekilango, Sam-Nujoma na Ubungo Interchange.

Dar es Salaam. Huenda ajali za barabarani zinazotokea kwenye makutano ya barabara zikapungua jijini Dar es Salaam, baada ya Serikali kuanza kazi ya kufunga taa za kuongozea vyombo vya moto katika maeneo muhimu jijini humo. 

Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) umeanza kazi ya kusimika taa za kuongozea vyombo vya moto (traffic lights) katika barabara mbalimbali za jiji hilo zikiwemo za Shekilango, Sam-Nujoma na Ubungo Interchange.

Meneja wa Kikosi cha Umeme kutoka Temesa anayesimamia mradi huo, Mhandisi Pongeza Semakuwa amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika haraka iwezekanavyo ili uanze kutumika. 

‘‘Katika barabara ya Shekilango, taa hizo zinasimikwa katika makutano yapatayo matano kwa gharama ya shilingi 700 milioni. Katika barabara ya Sam-Nujoma taa hizo zina simikwa katika makutano matatu yaliyopo Mawasiliano tower na Simu 2000 kwa gharama ya Sh350 milioni

“Wakati katika makutano ya Ubungo ‘flyover interchange’ kazi hii imefanyika kwa kushirikiana na mkandarasi wa mradi wa daraja hilo kwa gharama ya Sh70 milioni,’’ amesema Mhandisi Semakuwa leo Februari 23, 2021 jijini Dar es Salaam. 


Soma zaidi: 


Amesisitiza kuwa gharama za mradi huo zimekuwa nafuu tofauti na hapo awali kwa sababu nguzo zote zinazotumika kama malighafi za kutengenezea taa hizo zinatengenezwa katika karakana ya kikosi hicho iliyopo Keko Darajani.

“Hapo awali nguzo hizo pamoja na malighafi zake zilikuwa zikinunuliwa kwa gharama kubwa kutoka nje ya nchi na hivyo kusababisha miradi hiyo kuwa ya gharama kubwa na wakati mwingine kuchelewa kumalizika kwa wakati,” anaeleza Mhandisi Semakuwa katika taarifa iliyotolewa na Temesa. 

Mradi huo unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi mitatu, jambo litakalosaidia kuongeza umakini wa madereva kwenye makutano ya barabara na hivyo kupunguza ajali.

Enable Notifications OK No thanks