Mpango kulifanya Jiji la Dar kuwa kitovu cha utalii waja

April 5, 2019 3:27 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Serikali imesema imejipanga kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa kitovuti cha utalii kwa kulitumia jengo la tatu la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) kuingiza watalii wengi.
  • Sambamba na hilo ni kuimarisha Chaneli ya Utalii (Tanzania Safari Channel) kwa kuipatia wataalamu, vifaa na vitendea kazi stahiki.

Dar es Salaam. Huenda idadi ya watalii wanaokuja kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii na mikutano nchini ikaongezeka katika mwaka 2019/2020, baada Serikali kusema imejipanga kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa kitovu cha utalii kwa kulitumia jengo la tatu la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) kuingiza watalii wengi. 

Jengo hilo ambalo hadi kufikia Februari 2019 ujenzi wake umefikia asilimia 95.5 litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni sita kwa mwaka pindi litakapokamilika Mei 2019 kutokana na uwezo wa kuhudumia ndege 17 hadi 19 zikiwemo kubwa kwa wakati mmoja.

Akiwasilisha Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2018/2019 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2019/2020 jana (Aprili 4, 2019) Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema jengo hilo linatarajiwa kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa kitovu cha utalii kwa kuwezesha watalii wanaoingia nchini kuelekea katika maeneo mbalimbali ya vivutio  na nchi jirani katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini. 

Amesema mpango huu wa kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa kitovu cha utalii unakwenda sambamba na maboresho ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), lengo ni kuhakikisha watalii wanaoingia nchini wanakuwa na usafiri wa uhakika kuvifikia vivutio na kuelekea katika nchi za jirani. 

“Kwa kufanya hivyo, shughuli za kiuchumi nchini zenye kufungamana na utalii hususan ajira, huduma, biashara na usafirishaji zitaimarika na kuwaongezea kipato watu wetu,” amesema Majaliwa. 


Zinazohusiana:


Sambamba na hilo ni kuimarisha Chaneli ya Utalii (Tanzania Safari Channel) kwa kuipatia wataalamu, vifaa na vitendea kazi stahiki ambapo amesema chaneli hiyo itaendeleza taswira na sifa nzuri ya Tanzania kimataifa sambamba na kuongeza thamani katika mnyororo mzima wa biashara ya utalii nchini.

Muonekano wa juu wa Jiji la Dar es Salaam ambalo linakuwa kasi na kuvutia wageni wengi kutembelea vivutio mbalimbali. Picha|Mtandao.

Sekta ya utalii imeendelea kuimarika na kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa pato la Taifa na kuongeza ajira kwa wananchi na kampuni zinahusika kutoa huduma na bidhaa za utalii nchini.

“Mathalan, idadi ya watalii walioingia nchini mwaka 2018 imeongezeka na kufikia watalii milioni 1.49 ikilinganishwa na watalii milioni 1.33 walioingia nchini mwaka 2017. Vilevile, mapato yatokanayo na utalii yameongezeka na kufikia Dola za Marekani bilioni 2.43 mwaka 2018 ikilinganishwa na Dola za Marekani bilioni 2.19 mwaka 2017, sawa na ongezeko la asilimia 7.13,” amesema Majaliwa.

Katika mwaka 2019/2020, Serikali imebainisha kuwa itaendelea kuimarisha sekta ya utalii kwa kuihamasisha na kuiwezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kuendeleza sekta hiyo na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji ikiwemo usafiri wa anga ili kuvutia watalii wengi zaidi nchini.

Enable Notifications OK No thanks