Tanzania, Kenya Uganda wenyeji Afcon 2027

Mwandishi Wetu 1020Hrs   Septemba 27, 2023 Burudani
  • Wenyeji wa mashindo hayo unarudi tena katika ukanda wa CECAFA  baada ya miaka 47. 
  • Kwa mara ya kwanza michuano hiyo inafanyika katika nchi tatu.
  • Rais Samia atoa maagizo mazito kwa wizara.

Dar es Salaam. Shirikisho la mpira wa miguu barani Afrika (CAF) Iimezitangaza nchi za Tanzania Kenya na Uganda kuwa wenyeji wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Africa (AFCON) yanayorajiwa kufanyika mwaka 2027.

Rais wa CAF Patrice Motsepe, aliyekuwa akitangaza ushindi wa kuandaa michuano hiyo leo (Septemba 27, 2023) Cairo nchini Misri, amesema vigezo vilivyotumika kuzichagua nchi hizo ni pamoja na miundombinu bora ikiwemo malazi na hospitali.

“Mataifa haya matatu yamejiunga pamoja kwa sababu viwango na vigezo vyetu ni vya juu sana,” amesema Motsepe.

Michuano hiyo mikubwa zaidi barani Afrika katika ngazi ya timu za Taifa inarejea katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) baada ya miaka 47 ambapo mara ya mwisho iliandaliwa na Ethiopia mwaka 1976.


Tanzania, Kenya na Uganda zinaingia kwenye historia mpya ya michezo kutokana na kuwa wa kwanza kushinda kinyang’anyiro hicho cha kuwa wenyeji katika mashindano hayo yanayowaleta pamoja wadau wa michezo kutoka nchi mbalimbali.

Ni nchi mbili pekee kutoka ukanda wa CECAFA zilizowahi kuandaa michuani hiyo kabla ambazo ni Sudan iliyoandaa mara mbili pamoja na Ethiopia iliyoandaa mara tatu.


Zinazohusiana: Rais Samia aongeza dau ‘goli la mama’


Ni fursa kwa Tanzania

Hatua hiyo huenda ikachochea zaidi uchumi wa mataifa hayo ya Afrika Mashariki, hususan Tanzania inayotegemewa zaidi kutokana na kuwa na wingi wa viwanja bora vinavyofaa kwa ajili ya mashindano ya kimataifa.

Fursa hiyo inakuja wakati ambao Tanzania imezindua kampeni ya kuhamasisha watalii kutembelea vivutio vyake vya utalii kupitia filamu ya ‘Tanzania Royal Tour’ hivyo juhudi zikiwekwa itakuwa fursa nzuri ya kukuza mapato kupitia utalii.



Rais Samia aagiza maboresho ya viwanja vya michezo

Kufuatia Tanzania kutangazwa kuwa mwenyeji wa michuano ya AFCON Rais Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Sanaa, Utamaduni na  Michezo kufanya maandalizi ya michuano hiyo ikiwemo maboresho ya viwanja vya taifa.

“Nawaagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuhakikisha tunafanya maandalizi mazuri, ikiwemo kukamilika kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu, viwanja viwili vipya vya kisasa vya michezo Arusha na Dodoma,” amesema Rais Samia kupitia ukurasa wa Twitter.

Related Post