Soko la chai mbioni kufunguliwa Dar

Daniel Samson 0246Hrs   Aprili 30, 2019 Biashara


  • Soko hilo litasaidia kupunguza gharama za usafirishaji wa chai inayouzwa katika mnada uliopo katika mji wa Mombasa nchini Kenya. 
  • Mnada wa chai utakuwa unafanyika katika soko linalotarajiwa kufunguliwa jijini Dar es Salaam Mei mwaka huu. 

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa amesema Serikali inaendelea kutekeleza mikakati ya kufufua kilimo cha chai nchini ikiwemo kuanzisha mnada wa pamoja wa kuuza zao hilo hapa nchini ili kuwapatia wakulima bei nzuri. 

Chai inayozalishwa Tanzania husafirishwa nje ya nchi ambapo mnada wa zao hilo hufanyika katika soko lililopo mji wa Mombasa nchini Kenya. 

Bashungwa ametoa kauli hiyo bungeni leo (Aprili 30, 2019) wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalum mkoa wa Mbeya (Chadema), Sophia Mwakagenda ambaye alitaka kufahamu mkakati wa Serikali wa kuongeza bei ya zao la chai katika wilaya ya Rungwe na kokoa katika wilaya Kyela.

“Moja ya mkakati wa Serikali kwenye zao la chai ni kuanzisha mnada hapa hapa nchini badala ya kutegemea mnada wa Mombasa (Kenya). Pamoja na kokoa tunaendelea kuwasiliana na wanunuzi duniani ili kuona kama wanaweza kununua kokoa ya Tanzania,” amesema Bashungwa.


Soma zaidi: TADB yakusudia kujenga kiwanda cha kuchakata chai Iringa


Hata hivyo, Basungwa amesema kuongezeka kwa bei ya chai kunategemea hali ya soko ya mwaka husika.

Kwa wastani Tanzania inazalisha tani 34,000 za chai ukilinganisha na Kenya inayozalisha wastani wa tani 40,000 kwa mwaka.

Kama ilivyo kwa zao la tumbaku na pamba, Je ni lini Serikali itaongeza bei katika zao la chai katika wilaya ya Rungwe na kakao katika wilaya Kyela?

Chai ni miongoni mwa mazao ya biashara ambayo yanaliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni, ambapo kwa mujibu wa takwimu zilizopo kwenye Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa cha mwaka 2017 cha Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ambapo mwaka 2017 iliingiza Sh108. bilioni ikiwa mbele ya pamba ambayo iliingiza Sh80.2 bilioni.

Januari 15, 2019 wakati akizungumza na wananchi na wanachama wa chama cha ushirika cha wakulima wa chai katika kijiji cha Mkonge wilayani Mufindi mkoani Iringa alisema mkakati wa kuanzisha mnada wa chai utakamilika Mei mwaka huu na utakuwa unafanyika katika jiji la Dar es Salaam ambapo linajengwa soko la zao hilo. 

Kukamilika kwa soko hilo hapa nchini kutasaidia kupunguza gharama za usafirishaji wa chai kwenda Mombasa na kuwanufaisha zaidi wakulima hasa wa mikoa ya Mbeya, Arusha, Tanga, Iringa na Njombe wanaotegemea zao hilo kwa ajili ya kuendesha maisha yao. 


Related Post