Siasa, biashara ya nyama vyatawala kuungua kwa msitu wa Amazon

August 29, 2019 12:18 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Rais wa Brazili, Jair Bolsonaro alitaja msitu wa Amazon kama moja ya sababu inayozuia maendeleo ya nchi hiyo.
  • Baadhi ya wachambuzi wamesema msitu huo uliachwa uungue kwa makusudi ili watu wapate sehemu ya kufugia mifugo.  
  • Msitu huo unachangia asilimia sita ya hewa ya oskijeni duniani

Dar es Salaam. Suala la moto  kwenye nchi ya Brazil sio kitu kigeni kwani kwa mwaka 2019 pekee, nchi hiyo imepata majanga ya moto zaidi ya mara 74,000 ambapo kati ya majanga hayo, msitu wa Amazon umeripotiwa kupata majanga takribani 40,000.

Amazon ni msitu mkubwa duniani na unachangia asilimia 6 ya hewa ya oskijeni duniani kote huku ukiwa na mabilioni ya miti na mamilioni ya viumbe hai.

Asilimia 60 ambayo ni sawa na hekari milioni 670 za msitu huo zinapatikana kwenye mipaka ya Brazil na asilimia 40 iliyobaki kugawanywa kati ya Bolivia, Peru, Colombia, Ecuador, Guyana, Venezuela na Suriname na hivyo kuipa Brazil mamlaka makubwa juu ya msitu huo. 

Hivi karibuni, msitu huo umeripotiwa kuungua kwa muda mrefu na Serikali ya nchi hiyo haijafanya chochote kuhakikisha moto huo unazimwa na hivyo kuzua mjadala mbalimbali katika jumuiya za kimataifa na vyombo vya habari duniani

Mwendelezo wa kuungua kwa msitu huo ambao hadi sasa ni kilometa za mraba 3444.7 zimeteketea kwa moto kwa mwaka 2019 pekee kunachukuliwa kama tishio kwa uhai wa binadamu ikizingatiwa kuwa sehemu kubwa ya Amazon iko Brazil na kuungua kwake siyo ishara nzuri kwa wakazi wa nchi hiyo.

Msitu wa Amazon ni makazi ya mamilioni ya viumbe hai. Picha|Mtandao

Kati ya mambo ambayo yameripotiwa kutokea ni pamoja na giza linalosababishwa na moshi kutanda kwenye mji wa São Paulo saa kadhaa kabla hata ya jua kuzama kitu ambacho ni kigeni kwa wakazi wa mji huo na nchi ya Brazil.

Rais wa nchi hiyo, Jair Bolsonaro amekataa msaada wa kuzima moto huo uliotolewa na nchi 7 zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani (G7) wa Dola za Marekani milioni 22 (Sh50.5 milioni).  

Bolsonaro amedai kuwa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kupitia ukurasa wa Twitter alimdhalilisha na amemtaka aombe msamaha kwanza kabla nchi yake haijapokea msaada huo. 

Huenda chanzo cha moto huo kikawa ni siasa kwani katika kampeni zake wakati anapigania kiti cha urais, Bolsonaro alitaja msitu wa Amazon kama moja ya sababu inayozuia maendeleo ya nchi ya Brazil.

Brazil ni nchi inayafanya vizuri kwa biashara ya nyama hasa ya ng’ombe duniani ambapo mwaka 2018, iliongoza kusafirisha kiasi kikubwa cha nyama ya ng’ombe karibu asilimia 20 ya usafirishaji wote wa bidhaa hiyo. 

Baadhi ya wataalamu wa masuala ya moto wameviambia vyombo vya habari kuwa moto huo sio wakusababishwa na radi bali ni moto uliowashwa makusudi.

Catherine Stoof ambaye ni mratibu wa kituo cha masuala ya moto kwenye chuo cha Wageningen huko Netherlands amesema “huu moto umeanzishwa makusudi ili kusafisha huu msitu. Watu wanataka kuondoa msitu kuweka nafasi ya shughuli za ufugaji.”


Zinazohusiana

Bosi UN ataka jumuiya za kimataifa kuingilia kati kuungua kwa msitu wa Amazon


Nimuhimu kujua kuwa, msitu wa Amazon unanufaisha kila mtu anayeishi duniani kwani miti yake inanyonya hewa ukaa “green house” ambayo zipo kutokana na uchafuzi wa mazingira. 

Kutoweka kwa msitu huo ni jambo litakalobadilisha taswira ya maisha ya binadamu na kuongeza zaidi athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mmoja kati ya wanasayansi nchini Brazili, Carlos Quesada amesema msitu wa Amazon ulikuwa unachelewesha athari za tabianchi, jambo ambalo lilikuwa linawanufaisha wakazi wa dunia. 

Hata hivyo, Brazil inaendelea na jitihada za kuuzima moto huo ili kuhakikisha auharibu ikolojia ya viumbe wanaotegemea mazingira Amazon.

Enable Notifications OK No thanks