Bosi UN ataka jumuiya za kimataifa kuingilia kati kuungua kwa msitu wa Amazon

August 27, 2019 8:30 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) azungumzia kuungua kwa msitu wa Amazon kama dharula ya kuzingatiwa na jamii za kimataifa
  • Amethibitisha ongezeko la hewa ya ukaa kwenye anga la dunia
  • Guterres amezitaka nchi zote kutekeleza ahadi zake kama zilivyo kwenye mkataba wa mabadiliko ya tabianchi wa Paris.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres amesema sakata la kuungua kwa msitu wa Amazon ni jambo linalohitaji kuangaziwa na jumuiya za kimataifa ili kulinda msitu huo ambao ni muhimu kwa maisha ya binadamu.

Guterres ameyasema hayo wakati anawajibu maswali ya Waandishi wa Habari kwenye mkutano wa mataifa saba yenye uchumi mkubwa zaidi duniani (G7) ambao unafanyika jijini Biarritz, Ufaransa.

“Kuna wito thabiti wa kutaka jamii ya kimataifa iweze kusaidia nchi za Amazon; hivi sasa ili kuzima mioto inayoendelea na baadaye kusaidia upandaji miti kwenye msitu jambo ambalo ni muhimu sana ili kulinda eneo hilo muhimu kwa uhai wa binadamu,” amesema Guterres. 

Zaidi Katibu Mkuu ameongelea kuyeyuka kwa theluji kwenye ncha ya kaskazini mwa dunia na moto unaoendelea kuteketeza msitu wa mvua wa Amazon huko Amerika ya Kusini.

Aidha, Guterres amezungumzia hali ya tabianchi ya sasa kuwa ni mbaya kuliko ilivyokuwa wakati wa kupitisha mkataba wa mabadiliko ya tabianchi wa Paris.


Zinazohusiana


Guterres amesema nchi nyingi hazitimizi ahadi ambazo zimetoa kwenye mkataba wa Paris ambapo amezikumbusha nchi zote kuchukua hatua zaidi kwa ajili ya kupunguza hewa chafuzi kwa kutimiza ahadi zao kama inavyobainishwa kwenye mkataba huo. 

“Tunahitaji hatua zaidi tunaona jamii zikihamasishana, vijana nao wakihamasishana, tunataka viongozi wa Serikali wanaokuja New York, kwa ajili ya mkutano wa tabianchi mwezi ujao waweze kutoa ahadi za kina ili kupunguza hewa chafuzi ifikapo mwaka 2050,” amesema Katibu Mkuu.

Enable Notifications OK No thanks