Shule za Serikali zinavyoweza kuepuka matokeo mabovu darasa la saba
- Kwa miaka mitatu mfululizo shule za Serikali hazijafanikiwa kuingia 10 bora kitaifa
- Shule binafsi zinaendelea kutikisa katika matokeo ya darasa la saba na kutoa changamoto kwa shule za Serikali.
- Wadau washauri mazingira ya kusomea yaboreshwe sambamba na kurejesha heshima ya awali.
Dar es Salaam. Wakati watahiniwa wa darasa la saba wakijiandaa kwa mitihani yao ya kumaliza elimu ya msingi katika maeneo mbalimbali nchini, wadau wa elimu washauri Serikali kuboresha ubora wa elimu inayotolewa katika shule za msingi za umma ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
Hali hiyo inajitokeza wakati ambao shule nyingi za Serikali zinashika mkia katika matokeo ya darasa la saba huku shule binafsi zikifanikiwa kukaa kileleni kwa ubora wa ufaulu.
Uchambuzi wa matokeo ya Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) unaonyesha shule za Serikali ndizo hufanya vibaya kila mwaka kwenye matokeo ya darasa la saba, jambo ambalo ni tofauti na matokeo ya kidato cha nne na sita ambapo zimekuwa zikichuana vikali na shule binafsi kuingia 10 bora na hata 100 bora kitaifa.
Uchambuzi wa takwimu wa takwimu hizo za NECTA kati ya 2015 na 2017 unaonyesha kuwa katika kipindi hicho, shule za Serikali hazijawahi kuingia 10 bora ya shule za msingi zinazofanya vizuri kitaifa.
Badala yake 10 bora imekuwa ikishikiliwa na shule binafsi katika maeneo mbalimbali nchini, jambo linaloibua maswali juu ya ubora wa elimu inayotolewa katika shule za msingi ikiwa ni daraja muhimu la kumuandaa mwanafunzi kuendelea na masomo ya sekondari.
Licha ya 10 bora kutawaliwa na shule binafsi, takwimu za NECTA zinaonyesha kuwa shule hizo zinatoka zaidi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kaskazini na Mashariki mwa Tanzania.
Mathalani mwaka 2017, Kanda ya Ziwa ilitoa shule sita ambazo zilitoka mikoa ya Kagera ikiwa na shule nne, Mwanza (1), Shinyanga (1) ikifuatiwa na Kanda ya Mashariki ambapo Dar es Salaam ilitoa shule tatu na Tanga (1).
Mgawanyiko huo wa shule hautofautiani sana na miaka iliyotangulia, ikiashiria uwekezaji mkubwa unaofanywa na watu au mashirika binafsi katika elimu ya watoto wa Kanda hizo.
Wakati shule binafsi zikitamba 10 bora kitaifa, upande wa pili shule za Serikali zimeendelea kuwa vinara katika shule 10 za mwisho zinazofanya vibaya kitaifa.
Ikumbukwe katika kipindi hicho cha miaka mitatu mfufululizo hakuna shule binafsi hata moja iliyoingia katika kundi la shule zilizofanya vibaya. Hiyo ni tofauti kabisa na mitihani ya kidato cha nne na sita ambapo baadhi ya shule binafsi zimekuwa zikingia kwenye kundi hilo.
Kama ilivyo 10 bora, bado Kanda ya Mashariki, Ziwa na kwa sehemu Kanda za Kusini, Kaskazini na Kusini Magharibi ndiyo vinara wa kutoa shule za mwisho kitaifa ambazo zote zinamilikiwa na Serikali.
Katika matokeo ya mwaka 2016, Kanda ya Mashariki ilitoa shule tano kutoka mkoa mmoja wa Morogoro ikifuatiwa na Kanda ya Kaskazini kutoa shule nne na Kanda ya Ziwa ilitoa shule moja.
Licha ya matokeo mabovu katika Kanda zilizotajwa, bado iko mikoa kama Dar es Salaam imeanza kufanya juhudi za kuboresha elimu yake ambapo katika matokeo ya miaka miwili iliyopita haikuingiza shule yoyote kwenye kundi la shule za mwisho kitaifa.
Utofauti wa ufaulu unaotokea kwenye kanda pia unaathiriwa na utofauti wa matokeo unaojitokeza kwenye wilaya na mikoa.
Moja ya madarasa yaliyopo kwenye shule ya msingi Mpanda iliyopo wilaya ya Kyela Mbeya. Picha| Daniel Samson.
Tafsiri yake nini kwa elimu ya shule ya msingi?
Tofauti ya ufaulu wa shule za Serikali na binafsi katika ufaulu inatokana pia na uwekezaji wa elimu ambapo shule binafsi zimefanikiwa kuimarisha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia.
Mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), Mutegeya Joseph aliyewahi kusoma katika shule ya msingi Karume wilaya ya Newala mkoa wa Mtwara amesema bado shule za Serikali zinakabiliwa na changamoto nyingi ambapo wanafunzi wanakosa usimamizi mzuri wa wazazi na walimu jambo linaloathiri ufaulu wao.
“Wanafunzi wengi wanakosa usimamizi katika masomo yao kuanzia kwa wazazi mpaka shuleni kwa walimu wao hii inapelekea wao kutofanya vizuri,” anabainisha Joseph.
“Upande wa kitaaluma, wanafunzi wengi hufeli kutokana na kukosa elimu bora na iliyojitosheleza kutoka kwa walimu.”
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya elimu wameiambia Nukta kuwa watoto wanaoishi Kanda ya Ziwa wanakabiliwa na changamoto ya kukatisha masomo na kwenda kuchunga ng’ombe na wengine kuolewa katika umri mdogo jambo linalowafanya washindwe kuhudhuria masomo darasani.
Zinazohusiana:
- Mbinu zitakazowasaidia watahiniwa darasa la saba kufanya vizuri.
- Mbinu zinazoweza kuisaidia Temeke kutokomeza sifuri elimu ya sekondari.
- Udanganyifu mitihani darasa la saba kujirudia tena mwaka huu?.
Mhadhili wa Shule Kuu ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE), Dk Luka Mkonongwa akizungumzia shule binafsi anasema zimefanikiwa kuwekeza katika elimu ikiwemo miundombinu na zinajitahidi kumaliza mitaala mapema na hivyo kupata muda mwingi wa kufanya marudio na masahihisho kabla ya kuingia katika mtihani wa mwisho.
Shule hizo pia huwapatia wanafunzi wake majaribio ya kutosha ili kuwanoa na mitihani yao ya Taifa. Hata hivyo, anasema baadhi ya shule za Serikali hazitoi huduma hizi kwa ukamilifu kutokana na uhaba wa waalimu na ukosefu wa miundombinu ya kuwasaidia wanafunzi kama maktaba na maabara.
“Wazazi walio peleka watoto wao kwenye mfumo wa elimu bure wafahamu kuwa wana sehemu yao ikiwamo ufuatiliaji, kununua viabu na mahitaji ya watoto wao,” anasema Dk Mkonongwa.
Hata hivyo, katika hatua za awali mdau huyo wa elimu anashauri heshima ya mwalimu izingatiwe kwasababu amebeba dhamana kubwa ya kuwaelimisha wanafunzi ambapo anaamini kuanzishwa kwa Bodi ya Walimu kutasaidia kuongeza walimu wenye sifa ya kufundisha nchini.
“Turudishe heshima ya mwalimu. Mwalimu huyo huyo anayefelisha shule za Serikali akienda shule binafsi anafaulisha,” anabainisha Dk Mkonongwa.
Ripoti ya taasisi ya Uwezo iliyo chini ya Twaweza ya mwaka 2015 inabainisha kuwa asilimia 16 ya watoto wa darasa la saba mwaka 2014 walihitimu bila kuwa na uwezo wa kusoma mafunzo ya hadithi rahisi ya Kiswahili ya darasa la pili.
Afisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Hamis Lisu amekiri shule za Serikali kutofanya vizuri katika mitihani akieleza kuwa sababu ni wingi wa wanafunzi ikilinganishwa na madarasa na idadi ya walimu waliopo shuleni.
“Wenzetu wana mikakati zaidi yetu kuhakikisha wale wanaofika darasa la saba ni wale wenye uwezo mkubwa darasani,” amesema Lisu.
Hata hivyo, amesema katika mkoa wake wana mikakati mbalimbali kuhakikisha shule za Serikali zinaboreshwa ili kupata matokeo mazuri katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi.
“Mikakati ya kuwa na usimamizi wa karibu katika ufundishaji na kuwapa motisha walimu wetu,” amesema Lisu.