Fursa, EU ikiiondoa Tanzania katika orodha ya nchi hatarishi kifedha
- Uamuzi huo unatarajia kufungua fursa za uwekezaji na kukuza uchumi.
Dar es Salaam. Umoja wa Ulaya (EU) umeiondoa rasmi Tanzania kwenye orodha ya nchi hatarishi kifedha jambo litakalorahisisha biashara na kufungua fursa za uwekezaji baina ya Tanzania na nchi zinazounda umoja huo.
Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula, aliyekuwa akizungumza leo Januari 21, 2025 jijini Tanga, amesema mafanikio haya yanatokana na juhudi kubwa za Tanzania kuimarisha na kudhibiti mifumo yake ya kifedha.
“Mafanikio haya yanatokana na jiitihada kubwa za Tanzania kuimarisha utakatshaji fedha na ufadhili wa ujangili, amesema Luswetula katika uzinduzi wa maadhimisho ya tano ya wiki ya huduma za fedha kitaifa mwaka 2026.
EU na taasisi nyingine za kifedha hutoa orodha ya nchi zenye hatari ya kifedha (high risk countries) ili kulinda mfumo wa kifedha wa kimataifa.
Nchi huwekwa kwenye orodha hii ikiwa zina udhibiti dhaifu wa kifedha, uwazi mdogo wa taarifa za kifedha, kiwango kikubwa cha ufisadi au utapeli, utoaji wa mikopo isiyo endelevu, au kushindwa kufuata viwango vya kimataifa kama AML/CFT.
Desemba 5, 2025 EU ilitangaza rasmi kuiondoa Tanzania na nchi nyingine za Afrika ikiwemo Mali, Nigeria, Msumbiji, Afrika Kusini na Burkina Faso baada ya utekelezaji wa marekebisho makubwa ya mifumo yao ya kifedha.
Ni fursa kwa Tanzania
Naibu Waziri Luswetula aliyekuwa akimuwakilisha Waziri wa Fedha, amesema kuwa uamuzi huo wa EU ni fursa kwa Tanzania kuimarisha uchumi wake na biashara katika nchi zinazounda umoja huo.
“Kutokana na hatua hiyo biasara na miamala ya kifedha kati ya Tanzania na nchi za ulaya itakuwa rahisi, haraka na yenye gharama nafuu ifikapo Januari 29, 2026,” amesema Luswetula.
Aidha, Luswetula amebainisha kuwa hatua hiyo itafungua hatua mpya za uwekezaji na kufungua milango ya uwekezaji ikitazamia kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara Afrika.
Huenda umuamuzi huo wa EU ukaongeza mapato yatokanayo na uuzwaji wa bidhaa katika nchi za umoja huo kutoka Sh3.5 bilioni ( Euro 1,195) zilizorekodiwa kwa mwaka 2024 kwa mujibu wa tovuti rasmi ya EU.
Ukuaji wa sekta ya fedha unaongezeka
Kwa mujibu wa Luswetula, ukuaji wa shughuli za kiuchumi na sekta ya fedha nchini Tanzania umeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka ambapo hadi kufikia Septemba 2025, Tanzania ilikuwa na jumla ya benki za kibiashara 35, benki za kijamii mbili, benki za maendeleo mbili pamoja na benki tatu za huduma ndogo za fedha.
Aidha, amesema kuwa taasisi 2,811 za huduma ndogo za fedha pamoja na vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha 70,913 zilisajiliwa, huku taasisi mbili za ubadilishanaji wa fedha zikiongeza idadi ya watoa huduma rasmi nchini.
Kwa mujibu wa Luswetula, upanuzi huo umeenda sambamba na ongezeko kubwa la mawakala wa benki nchini. Ambapo Idadi ya mawakala wa benki imeongezeka kutoka 106,176 hadi kufikia 145,430, jambo linalorahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha hadi ngazi ya jamii.
Mbali na ongezeko la taasisi, rasilimali za kibenki nazo zimeendelea kuimarika na kufikia Sh71.8 trilioni Septemba 2025, ikilinganishwa na Sh62.2 trilioni zilizorekodiwa Septemba 2024.
Aidha, katika kipindi kama hicho, amana za benki zimeongezeka hadi Sh50.2 trilioni kutoka Sh42.7 trilioni mwaka uliotangulia, hatua inayotafsiriwa kama ishara ya kuongezeka kwa imani ya wananchi katika sekta ya fedha.
Katika maelezo yake, Luswetula pia amebainisha kuwa mikopo kwa sekta binafsi imekua kwa kasi kubwa. Ikiongezeka na kufikia Sh42 trilioni mwaka 2025 kutoka Sh35 trilioni mwaka 2024, sawa na ukuaji wa asilimia 24.
Hata hivyo, pamoja na ongezeko la mikopo, amebainisha kiwango cha mikopo chechefu bado kiko katika hali inayodhibitiwa.
“Mikopo chechefu imeongezeka kwa asilimia 2.78, kiwango ambacho bado kipo ndani ya ukomo wa kisheria wa asilimia tano,” ameeleza Luswetula.
Soko la hisa laongezeka
Kwa upande wa sekta ndogo ya mitaji na dhamana, Luswetula amesema Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) limeendelea kukua ambapo kuonesha ukuaji idadi ya kampuni zilizosajiliwa katika soko hilo imefikia 28 huku mifuko ya uwezeshaji ikifikia 21.
Aidha, ameainisha kuwa thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji ilifikia Sh63.7 trilioni katika kipindi kilichoishia Desemba 2025.
“Jumla ya mauzo ya hisa na hati fungani katika soko la hisa la Dae es Salaam yamefikia Sh6.87 trilioni vilevile thamani ya mifuko ya uwekezaji wa pamoja ilifikia Sh4.35 trilioni katika kipindi hicho,” ameongeza Luswetula.

Elimu ya fedha kwa wananchi bado kikwazo
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika uboreshaji wa sekta ya fedha, Luswetula amesema bado kuna changamoto kwa Watanzania wengi, ikiwemo uelewa mdogo wa masuala ya kifedha, uandishi wa maandiko ya miradi pamoja na kuendelea kutumia huduma zisizo rasmi za kifedha.
Kutokana na hali hiyo, amewahimiza wananchi kushiriki kwa wingi katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa ili kupata elimu sahihi kuhusu matumizi ya huduma rasmi, ikiwemo kufungua akaunti, kuweka akiba, kukata bima, kuwekeza na kutoa maoni au malalamiko yanayohusu sekta ya fedha.
“Kwa waelimishaji kwa ngazi zote, mjikite kutoa elimu ya fedha na ujasiriamali kwa weledi na lugha raisi ambapo wananchi watawaelewa kirahisi zaidi,” ameelekeza Luswetula.
Wakati huohuo, Luswetula amewahimiza watoa huduma za fedha wasio rasmi, wakiwemo wakopeshaji binafsi, kujisajili na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na mamlaka nyingine husika.
Pia ameagiza BoT kuongeza udhibiti wa sekta ya fedha ili kuwalinda wananchi dhidi ya madhara ya mikopo umiza maarufu kama kausha damu, ambayo mara nyingi husababisha wananchi kupoteza mali zao.
Latest