Ratiba mitihani darasa la saba, kidato cha nne hadharani Tanzania

Daniel Samson 0351Hrs   Juni 17, 2020 Habari
  • Muda wa wanafunzi kusoma darasani kuongezwa kwa saa mbili kwa siku.
  • Ratiba ya mitihani ya kitaifa ya darasa la saba, kidato cha pili na nne nayo yatangazwa. 
  • Walimu, wanafunzi watakiwa kuchukua tahadhari kujikinga na Corona. 

Dar es Salaam. Ni dhahiri kuwa itakuwa ni mchakamchaka kwa wanafunzi na walimu katika shule msingi na sekondari kukamilisha masomo ya mwaka 2020, baada ya Serikali kutangaza kufunguliwa kwa shule zote mwishoni mwa Juni mwaka huu na kuweka bayana ratiba za mitihani ya Taifa. 

Jumanne hii wakati anavunja Bunge la 11 jijini Dodoma, Rais John Magufuli alitangaza kufunguliwa kwa shule zote ifikapo Juni 29 baada ya wanafunzi kukaa nyumbani kwa zaidi ya miezi miwili kutokana na janga la Corona (COVID-19).

Rais alisema wameruhusu shule na shughuli nyingine ziendelee kutokana na  maambukizi ya COVID-19 kupungua kwa kiasi kikubwa.

Baada ya agizo hilo la Rais, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako leo ametangaza ratiba za mitihani ya kitaifa na namna masomo yatakavyoendeshwa shuleni baada ya wanafunzi kurejea.

Amesema wanafunzi watamalizia muhula wa kwanza wa masomo Agosti 28, 2020 na kuanza muhula wa pili ambao utakamilika Desemba 18 kabla ya kufanyika kwa mitihani ya kufungia shule.

“Ili kukamilisha muhtasari wa masomo, shule zitalazimika kuongeza saa mbili za masomo kwa siku ili kufidia muda uliopotea. Maelekezo ya kuongeza muda hayatahusisha madarasa ya awali,” amesema Prof Ndalichako. 


Zinazohusiana:


Kwa wanafunzi wa kidato cha tano watakaoripoti shuleni Juni 29 watasoma na kukamilisha muhtasari wa kidato cha tano na mitihani ifikapo Julai 24.“Wanafunzi hawa wataanza rasmi masomo ya kidato cha sita tarehe 27 Julai, 2020,” amesema waziri huyo huku akibainisha kuwa wanafunzi wapya wanaoanza kidato cha tano, wao utaratibu wao utatangazwa majina yao yatakapotolewa.

Amewataka walimu wanaporudi shuleni wafundishe bila kukosa vipindi vyovyote ili wanafunzi waweze kufuatilia mihutahsari yao na wizara itafuatilia kwa karibu kuhakikisha wanafunzi wanasoma wakati wote. 


Kuhusu ratiba za mitihani 

Kwa wahitimu wa elimu ya msingi, Prof Ndalichako amesema darasa la saba watafanya mitihani yao kwa siku mbili kati ya Oktoba 7 na 8 mwaka huu.Kidato cha pili watafanya mitihani kuanzia Novemba 9 mpaka 20, 2020 huku wale wa darasa la nne, mitahani yao itaanza Novemba 23 na kukamilika Desemba 11, 2020.

“Wanafunzi wanaofanya mitihani ya kidato cha nne pamoja na wanafunzi wanaofanya mitihani ya kujitegemea na maarifa, mitihani itaanza Novemba 23 na kukamilika Desemba 11, 2020,” amesema waziri huyo leo jijini Dodoma. 


Tahadhari ya virusi vya Corona

Uongozi wa shule umetakiwa kuhakikisha wanafunzi, walimu na wafanyakazi wote wanazingatia maelekezo ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona kama ilivyotolewa katika mwongozo wa wizara ya afya. 

Mwongozo huo uliotolewa na Wizara ya Afya wakati wa kufunguliwa kwa vyuo na kidato cha sita Juni mosi mwaka huu. 

“Bado mwongozo huu utahusu shule ambazo zinafunguliwa, naomba niwasihi sana shule kuhakikisha zina vifaa vya kunawa mikono vya kutosha. Vilevile kunawa mikono kwa maji tiririka pia na sabuni,” amesema.

Amesema tangu wanafunzi wa kidato cha sita na vyuo warejee katika masomo Juni 1 hakuna hata mwanafunzi mmoja aliyeripotiwa kuwa na maambukizi ya Corona kutokana na hatua zilizochukuliwa kudhibiti ugonjwa huo.

Related Post