Rais Magufuli, dunia wamlilia Robert Mugabe
- Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe amefariki akiwa na miaka 95.
- Rais Magufuli awaongoza Watanzania kutuma salamu za rambirambi nchini Zimbabwe.
- Mugabe atakumbukwa kwa mengi ikiwemo uzalendo na ujasiri.
Dar es Salaam. Kufuatia kifo cha Rais wa kwanza wa Zimbabwe, Robert Mugabe, Rais John Magufuli ameungana na viongozi wengine duniani kuomboleza kifo hicho, huku wakimkumbuka kwa mchango wake katika ukombozi wa bara la Afrika.
Kiongozi huyo ambaye alitawala nchi ya Zimbabwe tangu mwaka 1987 hadi 2017 amefariki dunia akiwa nchini Singapore leo ambako alikuwa anapatiwa matibabu kwa muda mrefu sasa.
Taarifa ya kifo chake zimethibitishwa na familia na Rais wa sasa wa nchi hiyo, Emmerson Mnangagwa kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Mnangagwa amesema Mugabe alikuwa alama ya ukombozi, mtu wa Afrika aliyejitolea maisha yake kwa ukombozi na uwezeshaji wa watu wake.
“Kwa masikitiko makubwa natangaza kifo cha Baba wa Taifa la Zimbabwe na Rais wa kwanza, Robert Mugabe.
“Mugabe alikuwa ni alama ya ukombozi, mpigania uhuru wa Afrika aliyejitoa kwa ajili ya watu, mchango wake kwa Taifa letu na ulimwengu mzima hautosahaulika,” ameandika Rais Mnangagwa kwenye akaunti yake ya Twitter.
Ameacha mjane, Grace Mugabe, na watoto watatu; Bona Mugabe, Chatunga Bellarmine Mugabe, Robert Peter Mugabe Jr.
Rais Magufuli ametoa rambirambi zake kwa wananchi wa Zimbabwe kwa kumpoteza kiongozi shupavu ambaye alikataa ukoloni kwa vitendo.
“Afrika imepoteza mmoja wa viongozi Jasiri, shupavu, mwanajumuia wa Afrika na aliyekataa ukoloni kwa vitendo,” ameandika Rais Magufuli kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Rais Mstaafu na Baba wa Taifa la Zimbabwe Mzee Robert Mugabe. Afrika imepoteza mmoja wa viongozi Jasiri, Shupavu, Mwanamajumui wa Afrika na aliyekataa ukoloni kwa vitendo. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina.
— Dr John Magufuli (@MagufuliJP) September 6, 2019
Naye Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye amesema Mugabe alikuwa mtoto wa Afrika, licha ya mapungufu aliyokuwa nayo enzi za uhai wake.
“Pamoja na mapungufu yake kadhaa kama binadamu, Cde Robert Gabriel Mugabe ni mtoto wa Afrika!,” ameandika Nape katika ukurasa wake wa Twitter.
Viongozi wa Afrika wapaza sauti zao
Nje ya Tanzania, viongozi mbalimbali wameendelea kutuma salamu zao za rambirambi wakikumbushia mema na mchango wa marehemu Robert Mugabe enzi za uhai wake.
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema maneno yake hayatoshi kuelezea uzito wa kuachwa na kiongozi shupavu, shujaa na mzalendo wa Afrika ambaye jukumu muhimu la kutetea maslahi ya bara la Afrika lilikua kati ya utekelezaji wake.
“Tutamkumbuka Rais Mugabe kama mwanaume mwenye ujasiri ambaye hajawahi kuogopa kupigania alichokiamini hata kama hakikuwa maarufu,” amesema Kenyatta.
Zinazohusiana:
Naye Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema Mugabe ni kati ya viongozi wa kipekee na vinara wa Afrika katika kupigania uhuru wa bara hilo.
Amesema nchi ya Zimbabwe chini ya uongozi wa Mugabe iliwahifadhi wapigani uhuru wa Afrika Kusini wakati wakitekeleza mikakati ya kuwaondoa wakoloni katika nchi yao.
“Afrika imepoteza mmoja wa viongozi Jasiri, shupavu, mwanajumuia wa Afrika na aliyekataa ukoloni kwa vitendo,” ameandika Rais Magufuli. Picha| Mtandao
Nelson Chamisa ambaye ni kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe ametoa pole kwa familia ya kiongozi huyo na kusema kuwa wakati huu ni wakati wa giza zito nchini humo.
Amesema licha ya chama chake cha MDC (Movement for Democratic Change) kutofautiana kimtazamo na Mugabe bado anatambua mchango wa maendeleo enzi za uhai wake.
Chamisa amesema kuna mengi ya kuongelea juu ya miaka 95 ya kuishi na miaka zaidi ya 37 ya uongozi wa Mugabe lakini ndani ya nafsi thabiti ya “Ubuntu” anaheshimu maombolezo ya kiongozi huyo na kutakuwa na muda wa tafakari zaidi juu ya maisha yake.
Ubalozi wa Marekani nchini Zimbabwe kupitia ukarasa wake wa Twitter umeungana na ulimwengu kutoa masikitiko yao juu ya kifo cha rais huyo wa zamani wa Zimbabwe.
“Tunaunganana dunia kutafakari mchango wake katika kupigania uhuru wa Zimbabwe”, unasomeka ujumbe wa ubalozi huo kwenye ukurasa wa Twitter.