Nyuma ya pazia ulaji chipsi wanafunzi vyuoni Dar

March 13, 2019 2:12 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Wataalam wa afya wameeleza kuwa tabia hiyo ikizidi inaweza kuathiri afya na mwenendo wa ujifunzaji darasani.
  • Kama mwanafunzi hawezi kuacha kula chipsi, ni vema aongeze matunda, mbogamboga, juisi katika mlo wake ili kupata virutubisho muhimu.

Dar es Salaam. Kutokana na mtindo wa maisha wa baadhi vijana hasa wanaosoma elimu ya juu kupendelea kula chipsi kama chakula kikuu, wataalamu wa afya wameeleza kuwa tabia hiyo inaweza kuathiri afya ya mwili na mwenendo wa kujifunza darasani. 

Chipsi maarufu kama “viepe” hutokana na viazi vilivyokatwa na kukaangwa kwenye mafuta ya kula ambapo vijana wa kike na kiume huvutiwa nazo kutokana urahisi wa upatikanaji wake ukilinganisha vyakula vingine kama wali na ugali ambao unahitaji muda mrefu kidogo kuandaa.   

Mtaalamu wa afya, Dk Sandra Sillas kutoka hospitali ya Care Plus ya Msasani jijini Dar es Salaam ameiambia www.nukta.co.tz kuwa chips kavu humpatia mlaji wanga tu na kumkosesha virutubisho muhimu vinavyohitajika katika utendaji wa mwili. 

“Afya ya akili huenda sambamba na afya ya mwili hivyo mtindo wa ulaji huweza kuathiri afya ya akili ya mtu ambaye hali chakula sahihi,” amesema Dk Sillas.

Amesema hata kama chipsi zitaongezewa kachumbari ya kabichi bado hakitakuwa na mchanganyiko wa kutosha kwa sababu huongeza asidi mwilini ambayo ikizidishwa inaweza kuwa na madhara. 

Hata hivyo, wapo vijana ambao hawawezi kula chipsi bila kuweka mayai, nyama (mishkaki) au kuku wa kukaangwa ambapo mlaji akitumia kwa wingi anapata mafuta mengi mwili ambayo yanamfanya anenepe na kupata maradhi ya moyo na hata kiharusi. 

Dk Sillas anasema ulaji huo pia unaathiri mwenendo wa ujifunzaji darasani kwasababu wanafunzi wanakuwa hawapati virutubisho muhimu kuboresha utendaji wa ubongo. 

“Kwa wasichana mtindo mbaya wa kula huwapelekea kunenepa pasipo na mpangilio na hivyo mtu hupoteza kujiamini kutokana na mwili wake na inaweza kumpelekea kuwa na msongo wa mawazo,” amesema.

Ulaji wa chipsi kavu ambazo hazina mchanganyiko wa virutubisho vingine kama matunda, mboga mboga unaweza kuathiri afya ya mwili na akili. Picha|Mtandao.

Sababu za vijana kupenda chipsi

Salim Mansoor (22), mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini kampasi ya Dar es Salaam (TUDARCO) ameiambia www.nukta.co.tz kuwa yeye hutumia  chips mara mbili kila siku na sababu kuu ikiwa ni uharaka na wepesi wa upatikanaji wake.

“Kuna muda mwingine nachelewa kutoka chuo lakini sijawahi kulala njaa kwa sababu chips zipo muda wote,” anasema Mansoor.


Soma zaidi: biashara ya juisi inavyowatoa kimaisha vijana waliokataa kuajiriwa


Sababu nyingine ni kuwa hosteli za vyuo mbalimbali haziruhu wanafunzi kupika katika vyumba vyao na hivyo hulazimika kununua chakula kwenye migahawa.

Naye mfabiashara wa Kariakoo, Simon Mbutu (24) anasema muda ni changamoto ya vijana wengi kupika chakula kutokana foleni ya magari hasa nyakati za jioni na kuchelewa kurudi nyumba akiwa amechoka. 

Anafikiri chipsi ni chakula sahihi kuliko vyakula vingine vya mama lishe ambavyo huandaliwa katika mazingira mabovu vinavyoweza kusababisha magonjwa ya tumbo.  

“Chips walau haziwezi kunipa shida tumboni kwani nyingi hukaangwa huku unaziona lakini msosi wa nje hauna uhakika jinsi unavyopikwa hivyo mtu anaweza kupata maradhi kama kuhara na mengineyo,” anasema Mbutu.

Kama unapendelea chipsi basi kula na matunda au juisi ili kupata mlo kamili. Picha|Mtandao.

Hata hivyo, vijana wengine wamekuwa na maoni tofauti kuhusu tabia ya ulaji chipsi ambapo wanasema vijana wanapaswa kuwekeza katika afya zao kwa kula chakula bora bila kujali mazingira yanayowazunguka kwa sababu afya ni mtaji namba moja.

“Maisha ni mipango tu. Nilikua natoka darasani saa 8:00 nikifika nyumbani nalala kisha jioni naenda mazoezini au mpirani. nikirudi napika msosi wa mtu mmoja na wala hauchukui muda. Mashine za kupikia wali zipo nyingi sana,” anasema Peter Mashauri, mkazi wa jijini hapa.

Dk Sillas anasema kama mazingira ya chuo ni changamoto kwa wanafunzi na hawawezi kuacha kula chipsi, basi wanapaswa kuongeza mlo huo na matunda, juisi na mayai ili kupata virutubisho muhimu mwilini kuliko kula chipsi kavu.

Enable Notifications OK No thanks