Nini kimetokea kuporomoka kwa huduma za posta 2018?

February 14, 2019 5:48 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ndani ya mwaka mmoja watumiaji wa huduma hizo wamepungua kwa asimia 4.8 huku watoa huduma hizo wakipungua kutoka 35 mwaka 2017 hadi 28 Disemba mwaka jana.
  • Utumaji wa vifurushi ndani na nje ya nchi umeongezeka kidogo kwa mwaka 2018.
  • Wachambuzi wamesema huduma za posta zitaendelea kuwepo muda mrefu ujao kutokana na kupata uungwaji mkono wa biashara ya mtandaoni (E-Commerce).

Dar es Salaam. Licha ya kuonyesha mwenendo mzuri wa ukuaji katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, idadi ya watumiaji na watoa huduma za posta imeporomoka kidogo mwaka 2018, jambo linaloibua maswali juu mstakabali wa aina hiyo ya mawasiliano nchini. 

Huduma za Posta ni mfumo wa kusafirisha na kupokea barua na vifurushi kwa kutumia anuani maalum na stempu za malipo kutegemeana na ukubwa au uzito wa barua au kifurushi, pia kutegemeana na kasi ya kufikisha ujumbe au mzigo sehemu husika.

Uchambuzi  wa takwimu za robo ya mwisho ya mwaka 2018 zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2018 watumiaji wa huduma za posta nchini walipungua hadi 353,742 Desemba 2018 kutoka 445,160 waliokuwepo katika kipindi kama hicho mwaka 2017. 

Katika kipindi cha mwaka mmoja tu watu 91,418 au sawa na kusema asilimia 4.8 ya watumiaji wa waliokuwepo mwaka 2017 hawakutumia huduma hizo za posta. 

Idadi hiyo ya wateja wa posta inajumuisha watu na mashirika mbalimbali ya umma na binafsi yanayofanya kazi nchini.

Hali hiyo inaondoa matumaini yaliyoanza kuonekana baada ya watumiaji kuanza kuongezeka miaka minne iliyopita hadi kufikia kiwango cha juu kwa hivi karibuni cha watumiaji 522,945 mwaka 2015 ukilinganisha na 188,297 waliokuwepo mwaka 2014 .

Hata hivyo, mwenendo wa idadi ya watumiaji wa huduma za posta umekuwa ni wa kupanda na kushuka lakini haujawahi kuporomoka kufikia kiwango kilichorekodiwa mwaka 2014.

Sekta hiyo haijakumbwa na kushuka tu kwa watumiaji. Takwimu za TCRA zinabainisha kuwa idadi ya watoa huduma nayo imeporomoka kutoka 35 mwaka 2017 hadi kufikia 28 Disemba mwaka uliopita. Hiyo ina maana kuwa ndani ya mwaka mmoja tu watoa huduma saba wameachana na biashara ya vifurushi na barua. 

Anguko hilo linaweza kuwa la ghafla au kuacha maswali mengi ikizingatiwa kuwa idadi ya watoa huduma iliongezeka kutoka 33 mwaka 2016 hadi 35 mwaka 2017 kabla ya kushuka mwaka jana. 

Wakati watoa huduma na watumiaji wa huduma za posta wakipungua, idadi ya barua na vifurushi vinavyotumwa ndani na nje ya nchi imeongezeka kidogo hadi kufikia milioni 10.8 Disemba mwaka jana ukilinganisha na milioni 10.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2017. 

Pamoja na takwimu kuonyesha kushuka kwa watumiaji wa huduma za posta na watoa huduma kupungua, baadhi ya wachambuzi wameiambia Nukta kuwa zitaendelea kuwepo kwa muda mrefu ujao hasa katika usafirishaji wa vifurushi kimataifa kunakochagizwa na manunuzi ya mtandaoni (E-Commerce) yanayoratibiwa na kampuni kama Amazon, Alibaba, Jumia, Kupatana. 


Soma zaidi: Kama unafikiri mtandao unaweza kuua huduma za posta Tanzania, utasubiri sana


Biashara hiyo ya mtandaoni ambayo imeanza kuchukua nafasi ya biashara ya maduka makubwa inawapa fursa watoa huduma za posta kuendelea kuwepo katika soko la ushindani kwa kutumia ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) ambayo imepunguza idadi ya watu wanaotumia barua za kawaida kupashana habari. 

Mtaalam wa Usalama Mtandaoni kutoka kampuni ya Kabolik, Robert Matefu anasema matumizi ya huduma za posta hasa utumaji na upokeaji vifurushi yataendelea kuwepo kwa sababu ni njia rahisi ya watu kupokea mizigo wanayonunua kwenye maduka ya mtandaoni. 

“Huduma za posta zitaendelea kuwepo, kutakuwa na mabadiliko ya jinsi zinavyofanya kazi ili kuendana na ongezeko la biashara ya kimataifa ya mtandaoni,” amesema Matefu.

Hata hivyo, Shirika la Posta (TPC) linalomilikiwa na Serikali, limeeleza kuwa linaendelea kuboresha huduma zake ili ziendane na mabadiliko ya teknolojia ikiwemo kuongeza wigo wa kuwafikia wateja wengi ambao wanatuma na kupokea vifurushi ndani na nje ya nchi.

Enable Notifications OK No thanks