Kama unadhani mtandao unaweza kuua huduma za posta Tanzania, utasubiri sana

Daniel Samson 0529Hrs   Agosti 09, 2018 Ripoti Maalum
  • Watumiaji wa huduma hizo wanaongezeka huku vifurushi vinavyotumwa vinapungua kila mwaka.
  • Wanaotumia zaidi huduma hiyo ni wanafunzi, wazazi, wafanyakazi na mashirika.
  • Kwa wastani mtu mmoja duniani hutuma barua au vifurushi 43 kwa mwaka.
  • Idadi ya mashirika yanayotumia huduma za posta nchini imeongezeka mara 10 ndani ya mwaka mmoja. 

Dar es Salaam. Kama wewe ni mmoja wa watu wanaodhani ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) inayochochewa na matumizi ya intaneti, barua pepe na mitandao ya kijamii umeua huduma za posta nchini, basi utasubiri sana. 

Hali ni tofauti, wateja wanaotumia huduma za posta yaani kutuma vifurushi na barua  ikiwa ni njia ya kuwasiliana na ndugu, jamaa, marafiki na shughuli rasmi za ofisini inaongezeka kila mwaka nchini.

Idadi ya watumiaji hao ni sawa na asilimia 1.35 ya watu milioni 40.3 wanaomiliki laini simu za mkononi nchini ambapo huzitumia kwa mawasiliano na kama mbadala wa barua ambazo zinaandikwa kwa kalamu na karatasi.

Kimsingi huduma za Posta ni mfumo wa kusafirisha barua na vifurushi kwa wapokeaji kwa kutumia anuani maalum na stempu za malipo kutegemeana na ukubwa au uzito wa barua au kifurushi, pia kutegemeana na kasi ya kufikisha ujumbe au mzigo sehemu husika.

Uchambuzi  wa takwimu za mawasiliano za robo ya kwanza ya mwaka 2018 (Januari-Machi) zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2017 watumiaji wa huduma za posta nchini walifikia 545,160 ikiwa ni ongezeko la wateja 385,786 ukilinganisha na miaka mitano iliyopita.

Idadi hiyo ya wateja wa huduma za posta inajumuisha watu binafsi na mashirika mbalimbali ya umma na binafsi yanayofanya kazi nchini.

Mpaka kufikia Desemba 2017 kulikuwa na watu binafsi 364,853 wanaotumia huduma za posta, idadi hiyo imepungua kidogo ukilinganisha na mwaka 2016 ambapo walikuwa 364,953. Wakati watumiaji binafsi wakipungua, mashirika yanayotumia huduma za posta yameongezeka mara 10 hadi kufikia 180,307 mwaka 2017 ukilinganisha na mashrika 16,423 mwaka 2016.

Kumekuwepo na mawazo tofauti kuwa huduma za posta ni jambo lililopitwa na wakati lakini ikumbukwe kuwa bado kuna watanzania wanatumia huduma hiyo kwa sababu ni salama na inakidhi mahitaji, usiri wa barua na mizigo inayotumwa na kupokelewa. 

Huenda imani hiyo juu ya posta inatokana na changamoto za usiri zinazotokea kwenye barua pepe au mitandao ya kijamii ambapo baadhi ya mashirika kama Facebook na Google yamekuwa yakishutumiwa kwa kuvujisha taarifa na mawasiliano ya wateja wao

Hali hiyo imewafanya baadhi ya watu waanze kurudi kwenye mifumo ya zamani ya mawasiliano. 

Kwa mujibu wa Muungano wa Posta Duniani, hadi kufikia mwaka 2015 watu milioni 5.26 walikuwa wameajiriwa kwenye sekta ya posta ambapo vituo 690,700 vinavyotoa huduma za posta vilikuwa vimeanzishwa. Kwa wastani mtu mmoja duniani hutuma barua au vifurushi 43 kwa mwaka.

Licha ya takwimu kuonyesha kuwa huduma za posta zitaendelea kuwepo kwa muda mrefu ujao, idadi ya barua na vifurushi vinatumwa na kupokelewa ndani na nje ya nchi ya Tanzania inapungua kila mwaka tofauti na soko la ndani. 

Shirika la Accenture la Marekani linaeleza katika utafiti wake wa mwaka 2015 kuwa kupungua kwa vifurushi vinavyotumwa na posta duniani kunatokana na watu kutafuta njia rahisi ya mtandao inayookoa muda na gharama za kutuma kifurushi lakini bado huduma za posta zinahitajika sana kulingana na aina ya kifurushi kinachotumwa.

Baadhi ya stempi zilizowahi kutumika miaka ya nyuma kama ushahidi kuwa barua imelipiwa gharama zake. Picha| stampmail.com

Watumiaji wengi wa huduma za posta ni wanafunzi na wazazi wanaopokea ripoti za matokeo ya masomo darasani, wanafunzi wanaoomba mikopo ya elimu ya juu, watu wanaotafuta ajira, wafanyakazi na mashirika yanayoratibu shughuli za kiofisi.

Kutokana na umuhimu wa posta, Umoja wa Mataifa (UN) umeitenga Oktoba 9 kila mwaka kuwa siku ya Kimataifa ya Posta Duniani aliyoanza kuadhimishwa 1969 ambapo inaaminika kuwa sekta ya posta imesaidia kuboresha biashara na maisha ya kila siku ya watu na kuchangia katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya jamii. 

Huduma za posta hutolewa na kampuni, taasisi na mashirika mbalimbali ya umma na binafsi kutegemeana aina, uzito wa barua na mzigo unaotumwa. Tanzania ina shirika moja la umma la posta na kampuni 34 binafsi ambazo hutoa huduma hizo ndani ya miji, mji mmoja kwenda mwingine, ndani ya nchi, Afrika Mashariki na kimataifa. 

Inaelezwa kuwa huduma za posta zilianza kutolewa tangu zamani hasa katika tawala za kifalme za Uajemi ya Kale, China ya Kale na Roma ya Kale ambapo watumishi wa mtawala walikaa katika vituo vyenye umbali wa safari ya siku moja, kupokea barua na kuzipeleka sehemu husika kwa kutumia farasi. Wakati wa mapigano huduma hizo zilisimama. 

Katika karne ya 19 mawasiliano miongoni mwa nchi za Ulaya yaliongezeka ambapo matumizi ya stempu kama ushahidi  wa kuwa barua imeshalipiwa gharama zake na bahasha sanifu pamoja na maumbo ya anwani zilikubaliwa na kusambaa duniani kote.

Posta na mkakati mpya

Ili kuhakikisha huduma za posta zinakuwa endelevu nchini, Shirika la Posta linalomilikiwa na serikali, limeendelea kuboresha huduma zake kwa kuongeza wigo wa kuwafikia wateja wengi ambao wanatuma na kupokea vifurushi ndani na nje ya nchi. 

Postamasta Mkuu  wa Shirika la Posta Tanzania (TPC), Hassan Mwang’ombe anasema shirika hilo limeendelea kuimarisha huduma ya Posta Mlangoni katika sehemu ambazo miundombinu ya anwani za makazi zimekamilika ili kumfikia kila mteja. 

“Huduma ya Posta Mlangoni itawezesha kuwafikishia wateja wa Posta barua au taarifa zinazohusiana na huduma zetu maofisini au majumbani kwao, badala ya kutumia utaratibu uliozoeleka wa masunduku ya barua,” anasema. 

Mwang’ombe anasema wanabuni huduma mpya kila wakati ili kuhakikisha wanaongeza idadi ya wateja na ubora wa huduma, “Huduma mpya ambazo zimeanza kutolewa ni kupitia maduka ya kubadilisha fedha ya Bureau de Change na huduma mbalimbali zinazotolewa na kituo cha Jamii Centre,” anasema Mwang’ombe.

Jamii Centre ni vituo maalumu vya kutolea huduma ya jamii kwa pamoja kwa niaba ya serikali na taasisi mbalimbali zikiwemo huduma za kibenki, ukusanyaji wa maduhuli, malipo ya leseni, kodi za serikali na  miamala ya fedha kwa kutumia simu za mkononi. 


Related Post