Ni uzushi mtupu: Wakenya hawajaandamana kupinga zuio la kutotoka nje
- Picha ya maandamano yaliyotokea Mei 8 jijini Nairobi haina uhusiano na watu kupinga marufuku ya kutoka nje.
- Bali ni picha inayoelezea waandamanaji kupinga kutolewa katika nyumba walizokuwa wanakaa.
- Picha hiyo ni uzushi na haina ukweli wowote kuhusu Corona.
Dar es Salaam. Kwa sasa katika mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook na WhatsApp imesambaa picha ikionyesha watu wakiandamana nchini Kenya ikidaiwa kuwa wanapinga marufuku ya kutokutoka nje wakati huu wa janga la Corona.
Picha hiyo imebeba ujumbe unaodai kuwa wananchi wa Kenya hawataki tena kukaa ndani na sasa wanashinikiza kuendelea na shughuli zao.
Lakini kimsingi ujumbe uliowekwa katika picha hiyo hauna uhusiano wowote na watu kuandamana kupinga marufuku ya kutokutoka nje (lockdown) kwa sababu ya kujikinga na ugonjwa wa virusi vya Corona.
Ukweli ni upi?
Timu ya Nukta Fakti imebaini kuwa tukio hilo ambalo liko kwenye picha hiyo limechukuliwa katika kipande cha video cha maandamano yaliyotokea nje kidogo ya jijini Nairobi siku ya ijumaa Mei 8, 2020 na kuwekwa katika ukurasa wa Facebook wa The Star Kenya.
Yalikuwa ni maandamano ya wakazi wa maeneo ya Korogocho and Kariobangi jijini humo baada ya kuondolewa katika nyumba zinazodaiwa kuwa ni za kampuni ya maji safi na taka jijini humo.
Katika maandamano hayo, unaonekana moto unawaka katikati ya barabara za maeneo hayo huku mabomu ya machozi yakirushwa kuwatawanya waandamanaji.
Zinazohusiana.
- Picha za tetemeko Croatia zilivyotumika kupotosha Corona mtandaoni
- Siyo kweli wananchi Italia wanatupa pesa mitaani kuepuka Corona
Tukio hilo halikutokea kwa sababu ya raia hao kupinga kutokuruhusiwa kutoka nje ili kujikinga na Corona.
Video hiyo inayosambaa mtandaoni ikihusishwa na Corona ni uzushi na haina ukweli wowote kwa sababu ni ya tukio lingine kabisa.
Hata hivyo, nchi hiyo imeyafunga baadhi ya maeneo ya nchi hiyo yenye maambukizi makubwa likiwemo jiji la Nairobi ili kuzuia kusambaa zaidi kwa virusi vya Corona.