NECTA yafuta matokeo ya watahiniwa zaidi ya 1,000 darasa la saba 2020

Daniel Samson 0631Hrs   Novemba 21, 2020 Habari
  • Ni waliohusika na vitendo vya udanganyifu wakati wa mtihani.
  • Wengine 110 matokeo yao yamezuiliwa.
  • Yashauri waliohusika na udanganyifu wachukuliwe hatua za kisheria.

Dar es Salaam. Baraza la Mtihani Tanzania (NECTA) limewafutia matokeo watahiniwa 1,059 waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2020 kwa sababu mbalimbali ikiwemo kufanya udanganyifu. 

Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk Charles Msonde amewaambia wanahabari jijini Dar es Salaam leo (Novemba 21, 2020) wakati akitangaza matokeo ya darasa la saba kuwa wamebaini vitendo vya udanganyifu katika mtihani huo uliofanyika Oktoba mwaka huu na wamechukua hatua ya kufuta matokeo ya watahiniwa hao zaidi ya 1,000.

Katika matokeo hayo ya darasa asilimia 82.68 ya watahiniwa milioni 1.01 waliofanya mtihani huo wamefaulu. Hii ina maana kuwa wanafunzi nane kati ya 10 waliofanya mtihani huo mwaka huu wamefaulu. Wanafunzi wawili kati ya 10 wao wameshindwa kupata fursa ya kuendelea na masomo ya elimu ya sekondari. 

Ufaulu huo ni sawa na ongezeko la asilimia 1.18 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka jana. 

Dk Msonde amesema wameshazitaarifu mamlaka zinazohusika kuwachukulia hatua za kisheria watu wote waliohusika kwa namna moja au nyingine na udanganyifu huo. 

Kwa mujibu wa NECTA, idadi ya wanafunzi waliofutiwa matokeo imeongezeka mwaka huu ikilinganishwa na mwaka 2019 ambapo watahiniwa waliofutiwa matokeo walikuwa 909. 


Soma zaidi: 


Aidha, NECTA imezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 110 ambao waliugua au kupata matatizo na kushindwa kufanya mtihani kwa masomo yote au baadhi ya masomo.

“Watahiniwa husika wamepewa fursa nyingine  ya kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE) 2020 kwa mujibu wa kifungu 32 (1) cha Kanuni za Mitihani,” amesema Dk Msonde wakati akitangaza matokeo hayo. 

Related Post