Ndugai ahitimisha safari ya miaka tisa ya ubunge wa Lissu

June 28, 2019 4:06 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema ubunge wa mbunge huyo machachari umekoma baada ya kuvunja masharti ya katiba ya kutooneka bungeni bila taarifa na kutojaza fomu ya maadili ya mali na madeni.

Dar es Salaam. Mbunge wa Jimbo la Shingida Mashariki (Chadema) Tundu Lissu amefutiwa ubunge baada ya Spika wa Bunge Job Ndugai kutangaza kuwa kiongozi huyo wa upinzani  amekiuka katiba kwa kushindwa kueleza mahali alipo na kuwasilisha fomu ya maadili ya tamko la mali na madeni.

Ndugai ameliambia Bunge leo (28 Juni 2019) kuwa amemwandikia Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji  Semistocles Kaijage kuwa jimbo hilo kwa sasa lipo wazi.

Taarifa hiyo ya Spika inakamilisha safari ya ubunge wa Lissu ya miaka takriban tisa bungeni. Lissu alianza kushika nafasi hiyo mwaka 2010 na alichaguliwa tena katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2015.

Lissu, ambaye ni mnadhimu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, yupo nchini Ubeligiji kwa ajili ya matibabu baada ya kushambuliwa vibaya kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 2017.

“Mtakumbuka kuwa Tundu Lissu kwa zaidi ya mwaka mmoja amekuwa akionekana katika vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa akitembelea nchini mbalimbali za Marekani, Ulaya na kushiriki mihadhara ya masuala mbalimbali,” amesema Ndugai na kuongeza;

“Kwa muda wote huo hajafika hapa bungeni na kwa muda wote huo hajawahi kutoa taarifa yeyote ile kwa Spika kuhusu alipo na anaendeleaje wala hajawahi kuleta taarifa yeyote kwa kupitia hata kiongozi wake wa kambi ama wa chama chake bungeni. Sasa kama mnavyojua katiba yetu ipo wazi katika mambo ya aina hii na baadhi ya wabunge wameshapata matatizo nyinyi mnajua.


Soma zaidi: Serikali kulenga shabaha tano za uchumi mwaka 2019-2020


“Kutokana na utoro wa namna hii wa kushindwa hata kumwambia Spika nipo mahali fulani na jambo fulani, hakuna chochote…ni kumdisregard (Kutomjali) kama hayupo vile,” amesema Ndugai.

Spika huyo ameeleza kuwa Lissu pia ameshindwa kujaza fomu ya maadili ya mali na madeni inayotakiwa kikatiba kujazwa na mbunge ambapo nakala moja huenda Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma na nyingine hubaki bungeni kwa ajili ya kumbukumbu.

“Baada ya kuona kwenye kumbukumbu zangu hakuna nakala yeyote ya fomu za maadili za Lissu nilichukua jukumu la kupata uhakika wa jambo hili kutoka kwa Kamishna wa Maadili lakini naye hakuwa nazo,” amesema Ndugai.

“Kwa sababu hizo mbili, moja Spika kutokuwa na taarifa ya kimaandishi au vingenevyo ya alipo mheshimiwa Tundu Lissu na kwa maana hiyo kutoonekana bungeni. 

Lakini pia kwa kutotoa tamko la mali na madeni kinyume na ibara ya 71 (1) (g) napenda kuwafahamisha ndugu wabunge kuwa nimemwandikia Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa kiti cha ubunge jimbo la Singida Mashariki kilichokuwa kinashikiliwa na mheshimiwa Tundu Antiphas Lissu kipo wazi. Hivyo, Mwenyekiti wa Tume aendelee na hatua ya kukijaza kwa mujibu wa sheria,” ameongeza.

Enable Notifications OK No thanks