Nani kumrithi Ineke Bussemaker NMB?

November 17, 2018 11:18 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ineke Bussemaker  anayemaliza muda wake Disemba 2018. Picha| topvrouwen.nl


  • Mama huyo anang’atuka mwishoni mwa Desemba 2018 na kurejea nchini Uholanzi kuchukua majukumu mapya katika benki ya Rabobank yenye ubia na NMB.
  • Katika kipindi chake amefanikiwa pia kuimarisha mfumo wa jumuishi wa kifedha na matumizi ya dijitali katika kusogeza huduma karibu na wateja.
  • Bodi ya NMB bado haijaweka bayana ni nani atamrithi mama huyo raia wa Uholanzi.

Dar es Salaam. Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya NMB imetangaza kuwa Mkurugenzi Mtendaji wake Ineke Bussemaker atang’atuka katika taasisi hiyo mwishoni mwa Desemba 2018 kutekeleza majukumu mapya nchini Uholanzi, jambo linaloanzisha mchakato mpya wa kumpata mrithi wa mama huyo kutoka Uholanzi. 

Taarifa bodi hiyo iliyotolewa leo (Novemba 16, 2018) imesema, Bussemaker aliyejiunga na benki hiyo Mei 2015, atarejea nchini Uholanzi kwa majukumu mapya katika benki ya Rabobank ambayo ni mbia wa NMB.

NMB imemshukuru Bussemaker kwa uongozi wake madhubuti katika kipindi cha miaka minne ambao amesaidia kuipandisha chati benki hiyo na kujipatia mafanikio makubwa ikiwemo kuimarisha mfumo jumuishi wa huduma za kibenki kwa njia ya mtandao miongoni mwa watanzania.

Katika uongozi wake amefanikisha kusukuma mabadiliko makubwa ya huduma za kifedha ndani ya benki yakiwemo kuanzishwa kwa matumizi ya Mastercard na ‘QR codes’ katika kufanikisha manunuzi mbalimbali ndani na nje ya nchi.

NMB ilikuwa miongoni mwa benki za awali Tanzania kuzindua kadi ya “MasterCard World Rewards” Juni 2015. Kadi hiyo inawapa fursa wamiliki kupata huduma za kipekee za ofa kama huduma za usafiri wa ndege, malazi, kukodisha gari, vyakula, manunuzi, michezo na burudani kupitia  programu maalum ya “Mastercard priceless Cities and Priceless Africa Programmes”.

 Agosti mwaka huu benki hiyo ilizindua huduma tatu zinazojumuisha namna mpya ya kujiunga na benki (accessebility), namna mpya inayomwezesha mteja kutumia benki yake kikamilifu kidijitali na huduma ya tatu inalenga zaidi kujenga jamii isiyotegemea pesa za mifukoni (Cashless society).


Zinazohusiana: 


Bussemaker ni kigogo wa pili kutoka Rabobank kuiongoza NMB. Kabla ya kuchukua madaraka hayo mwaka 2015, NMB iliyorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), ilikuwa ikiongozwa na Mark Weissing ambaye baada ya kumaliza muda wake alipangiwa majukumu mengine katika benki ya Rabobank ambayo sasa mwanamama huyo anarudi kuendelea na kazi zake.

Kitendo cha raia hao wa kigeni kuongoza benki hiyo kwa vipindi viwili mfululizo kinaacha maswali iwapo atakuja mgeni mwingine au mzawa kuongoza taasisi hiyo ambayo faida yake ilipungua hadi Sh93 bilioni baada ya kodi mwaka 2017 kutoka Sh154 bilioni mwaka 2016. 

Hata hivyo, bodi hiyo haijaweka wazi ni nani atakayemrithi Bussemaker ikizingatiwa kuwa chini ya uongozi wake, NMB imejipatia mafanikio mengi na kuifanya kuwa miongoni mwa benki kubwa nchini.

Katika salamu zake, Bussemaker amewashukuru watendaji wote wa benki hiyo kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chote cha uongozi wake na kuifanya NMB kutambulika ndani na nje ya Tanzania kwa huduma bora. 

Amesema anapata faraja kuona NMB imekuwa sehemu ya kuboresha maisha ya wateja wake kupitia huduma za kibenki ambapo wengi wao wameweza kukuza mitaji ya biashara, kujiendeleza kielimu, kujenga nyumba na kuanzisha miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.

“Nitaondoka nikiwa mwenye furaha sana, ndani ya miaka minne tumefanya mambo makubwa kwa pamoja ndani ya NMB kwa kuona benki inakua na kuendeleza mafanikio ya biashara mpaka tulipo hapa,” amesema Bussemaker.

(Habari hii imeongezwa viunganishi (links).

Enable Notifications OK No thanks