Namna ya kupima ugonjwa wa rimoti kwa kamera ya simu
- Moja ya njia rahisi kupima iwapo rimoti inafanya kazi ama la ni kutumia kamera ya simu.
- Kwa mtu asiyefundi anashauri kufanya vitu vya msingi tu mengine hatarishi amwachie fundi mweledi.
Hakuna ambacho hukera zaidi kama wakati upo sebuleni unatazama televisheni na ghafla rimoti ikakugomea kufanya kazi unayoiamuru kama kuongeza sauti ama kuhamisha chaneli.
Kwa baadhi ya vifaa vya kielektroniki ambavyo vinategemea rimoti kwa sehemu kubwa kuendeshwa, kiburi hicho cha rimoti siyo tu hukatisha furaha bali hufanya hata vyombo husika kukosa maana.
Rimoti imetengenezwa rasmi kurahisisha kazi kwa kuzuia watu kuinuka mara kwa mara ili kukiendesha chombo cha kielektroniki kama televisheni, redio, na kiyoyozi. Utainuka mara ngani kwenda kukiamuru chombo cha kielektroniki kufanya kazi?
Katika kipindi cha miaka 10 niliyotumia kufanya shughuli za ufundi wa kielektroniki kabla sijaachana nao na kujikita katika uandishi wa habari nilibaini kuwa miongoni mwa vyanzo vikubwa vinavyofanya rimoti zigome kufanya kazi ni kuisha kwa betri, kuvujiwa na tindikali za betri, kubamizwa mara kwa mara na watoto na kuchoka baadhi ya vifaa vidogo vidogo ndani yake.
Hata hivyo, kwa namna rimoti ilivyotengenezwa ni mara chache sana kuona kifaa kimekufa kwa kuwa haina vifaa vingi ndani yake zaidi ya sakiti ndogo inayosaidia uendeshaji.
Mbali na rimoti, huenda kushindwa kufanya kazi kwa rimoti hiyo kunatokana na kifaa kikuu kama televisheni au redio kuharibika na kushindwa kuwa na mawasiliano.
Hivyo kwa mtu ambaye siyo fundi siyo rahisi kubaini iwapo rimoti ni nzima ama la.
Nukta (nukta.co.tz) inakuletea mbinu kuu inayosaidia kujua iwapo rimoti yako ni nzima ama la.
Njia rahisi zaidi kwa watu wasio mafundi ni matumizi ya simu yenye kamera kubaini ufanisi wa rimoti husika.
Rimoti ni kifaa muhimu kwa kuwa hutoa uhuru kwa mtu kukiendesha kifaa cha kielektroniki bila usumbufu wa kusimama mara kwa mara. Picha|Mtandao.
Tumia kamera ya simu kubaini ugonjwa wa rimoti
Kwa kawaida rimoti huwa na kitu cheupe juu kama taa ndogo katika upande wa mbele ambao huwa tunanyooshea vifaa vya elektroniki husika.
Kwa jicho la kawaida taa hiyo huwa haionekani kama inawaka ukibonyeza kitufe cha rimoti husika kutokana na mwanga wake kuwa mdogo sana.
Hata hivyo, kamera ya simu inaweza kuonyesha ule mwanga. Kuwaka kwa mwanga kunaonyesha rimoti ni nzima japo mwanga unaofifia unaweza kuonyesha kuwa betri zinakata roho.
Unafanyaje kupima rimoti hiyo?
Washa kamera ya simu yako kisha elekeza taa ya rimoti katika kamera hiyo. Hapa unatakiwa uone ile taa kwenye kioo cha simu yako. Bonyeza kitufe chochote cha rimoti na utaona kuna mwanga unaotokea baada ya kubonyeza. Hakikisha rimoti ina betri.
Iwapo hutaona mwanga wowote hata baada ya kubonyeza mara nyingi basi rimoti yako itakuwa na matatizo na unatakiwa kuyafanya yafuatayo .
Badiri betri za rimoti yako
Iwapo rimoti hiyo haijabamizwa bamizwa na watoto, jambo la kwanza ni kubadilisha betri ambazo mara nyingi huwa ni aina ya Double A (AA) au Tripple A (AAA). Weka betri mpya najaribu iwapo itafanya kazi. Mara nyingi huwa zinafanya kazi kwa kuwa kuisha betri ni tatizo kuu kwa rimoti na ni kawaida kwa vifaa vya kielektroniki kwa kuwa lazima zipate mlo.
Safisha ‘terminal’ za betri
Terminal ni vibati vidogo ambavyo huunganisha betri na sakiti ya rimoti ambacho chenye moto chanya huwa ni bapa na hasi huwa kina springi ama kibati kinachobonyea.
Mara nyingi terminal hizi huvujiwa na betri zilizokaa muda mrefu bila kubadilishwa na kusababisha kutu. Kutu hiyo huzuia betri kuunganishwa na sakiti ya rimoti ili ifanye kazi. Terminal hizo hupatikana mahali zinapowekwa betri.
Iwapo utabaini zina kutu baada ya kuzichunguza, unachotakiwa kufanya ni kuchukua msasa, tupa au kifaa kinachoweza kuondoa kutu hiyo kuzisugua kikamilifu hadi ziwe safi. Baada ya zoezi hilo kikamilifu weka betri zako mpya na ujaribu iwapo itafanya kazi. Ni zoezi la dakika tatu tu na itaanza kufanya kazi.
Baada ya kufanya hayo rimoti yako itaanza kufanya kazi kama zamani na kukuondolewa usumbufu uliokuwa nao.
Zinazohusiana:
- Mbinu tano za kudhibiti matumizi makubwa ya intaneti kwenye ‘smartphones’
- Mambo ya kuzingatia unapotumia Uber, Taxify
Mara nyingi njia hizo mbili huweza kufanyika kwa mtumiaji wa kawaida na iwapo rimoti imevunjika au ama imepata hitilafu unashauriwa kuipeleka kwa fundi mweledi karibu yako. Usijaribu kufungua kifaa cha kielektroniki bila kuwa na ujuzi ni hatari.
Baadhi ya vifaa kama televisheni, pasi, redio, vina moto mkubwa unaoweza kukudhuru ikiwemo kukua kabisa.
Uzoefu unaonyesha vifaa vingi vya kielektroniki vinakuwa na rimoti ambazo zinaweza kuwa mbadala baada ya awali kuharibika kabisa. Rimoti hizi hupatikana kirahisi na kwa bei nafuu kwenye maduka ya vifaa vya kielektroniki ikiwemo Kariakoo kwa Dar es Salaam isipokuwa kwa vifaa vile vya kielektroniki vya mitumba.
Usikubali kulipa fedha nyingi kurekebisha rimoti ambayo inaendana na thamani ya kununua rimoti mpya.
Video ya zoezi hili itapatikana hivi karibuni kwa Kiswahili. Endelea kusoma nukta.co.tz.