Ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake bado kitendawili duniani
- Mfumo dume na fikra kandamizi vyatajwa kuchochea wimbi la ukatili.
- Mwanamke 1 kati ya 3 duniani sawa na wanawake milioni 840 wamewahi kukumbana na ukatili.
Dar es Salaam. Licha ya juhudi, kampeni na mijadala isiyokoma ya wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu, ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake unaendelea kuwa janga sugu duniani.
Kwa mujibu wa WHO, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, wanawake milioni 840 (asilimia 11) wenye umri wa miaka 15 na zaidi ambao wamewahi kuwa kwenye mahusiano wamepitia ukatili wa kimwili au kingono kutoka kwa wenzi wao wa karibu.
Kwa takwimu hizo ni sawa na kusema mwanamke 1 kati ya 3 duniani kote wamewahi kukumbana na ukatili wa kimwili au kingono katika maisha yao.
Hii ni ishara kwamba ukatili huu si tu changamoto ya kijamii, bali ni dharura ya kiafya na haki za binadamu.
Ripoti hiyo pia imeweka wazi kuwa kwa mara ya kwanza, wanawake milioni 263 wamewahi kukumbana na ukatili wa kingono kutoka kwa mtu ambaye si mwenza wa kimapenzi.
Hata hivyo, wataalamu wanasema idadi halisi huenda ni kubwa zaidi kutokana na unyanyapaa na hofu ya kuripoti.
Sababu ukatili dhidi ya wanawake kuongezeka
Wakili Halima Sonda, Mkurugenzi wa Mipango na Uendeshaji kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), ameiambia Nukta Habari kuwa ongezeko la ukatili wa kijinsia kwa wanawake linasababishwa na mfumo dume na fikra kandamizi zinazoongoza jamii nyingi.
“Mifumo hii hupelekea kuendeleza unyanyasaji na kumwona mwanamke kama mali ya jamii na huweka mazingira ya ukatili,” amefafanua Wakili Sonda.
Kwa mujibu wa Wakili Sonda, mfumo huo unafanya mtoto wa kiume hupewa thamani na fursa zaidi kuliko mtoto wa kike, huku nafasi za kiuchumi na maamuzi zikielekezwa kwa wanaume.
Mtazamo huo humdidimiza mwanamke katika familia na jamii, na kuendeleza mazingira yanayochochea ukatili katika maeneo mbalimbali ya maisha.
Sababu nyingine ambayo Sonda amefafanua ni pamoja na mila kandamizi kama kuamini kuwa mtoto wa kike anapaswa tu kuolewa au hana haki sawa ya kurithi, zimejenga mtazamo unaofanya ukatili uonekane kawaida hali inayowafanya wanawake wengi kunyamaza wanapokumbana na unyanyasaji.
Kuelekea kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia Novemba 25 hadi Disemba 10, 2025, kampeni inayolenga kuongeza uelewa na kutoa wito wa kuzuia na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana duniani kote kauli mbiu ya mwaka huu inalenga kutokomeza ukatili huo mitandaoni.
Mbinu za kumsaidia mwanamke aliyeathirika na ukatili wa kijinsia
Leyla Abubakari Mtaalamu wa Saikolojia na Malezi kutoka mkoani Tanga ameeleza kuwa mwanamke ambaye amepitia ukatili wa kijinsia, ni muhimu kupatiwa matibabu ya kitaalamu.
“Kwanza anahitaji ushauri. Lakini kama amepata majeraha labda usoni, kukatwa viungo, lazima apewe ‘mindset counsellin’ (ushauri wa kisaikolojia) kubadilisha mtazamo wake ili aweze kurudi akae sawa tofauti na alivyokuwa,”amesema Leyla.
Mtaalamu huyo ameongeza kuwa mtu aliyepitia ukatili jambo la msingi ni kumsaidia kutafuta haki na utulivu ikiwa ni sambamba na kupata haki yake kupitia mfumo wa sheria ii kuipa utulivu nafsi yake.
Vilevile, Leyla amesisitiza kuwa mhanga wa ukatili anapaswa kupewa kitu cha kufanya ambacho kitamfanya awe awe na shughuli nyingi ili iwe vigumu kurudi kufikiria yale mabaya yaliyomtokea.
“Mwisho ni kuwa karibu watu wanaowapenda, na waonyeshe kumjali na kumpenda, watu wake wa karibu, waepuke kuyazungumzia yale mapito ambayo ameyapitia,” ameongeza Leyla.
Latest