Fedha za sherehe ya uhuru kukarabati miundombinu iliyoharibiwa Oktoba 29

November 24, 2025 7:06 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ili kuhakisha huduma zilizositishwa zinarejea kwa haraka.
  • Dk Nchemba asisitiza amani azionya taasisi za kidini kutotochea hoja zinazoleta mgawanyiko kwa wananchi.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameagiza fedha zilizotengwa kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Uhuru Desemba 9, 2025 zitumike kukarabati miundombinu iliyoathiriwa na vurugu zilizoibuka wakati wa maandamano ya Oktoba 29, ili huduma zilizositishwa zirejee kwa haraka.

Tanzania huadhimisha siku ya uhuru kila mwaka ifikapo Desemba 9, ambapo kwa mwaka huu 2025 Tanzania itakuwa inasheherekea kutimiza miaka 64 tangu ilipopata uhuru mwaka 1961.

Hata hivyo, sherehe za mwaka huupia  hazitahusisha magwaride kutoka vikosi mbalimbali vya kijeshi na maonesho ya halaiki ambapo wananchi hukutana katika uwanja ulioteuliwa na Serikali kushuhudia maonesho hayo.

Uamuzi huo wa Serikali umekuja mara baada ya kutokea uharibifu wa miundombinu mbalimbali ikiwemo kuchomwa moto kwa vituo vya magari yaendayo kasi, mabasi, taa za kuongozea magari pamoja na kuchoma moto barabara katika maandamano yaliyotokea siku ya Uchaguzi Mkuu Tanzania Oktoba 29.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba aliyekuwa akihutubia wananchi katika ziara yake aliyoifanya jijini Dar es Salaam leo Novemba 24, 2025 amesema Rais Samia ameagiza kuwa fedha zilizopangwa kutumika kwenye sherehe za uhuru zielekezwe katika ukarabati wa miundombinu hiyo.

“Kuanzia leo sekta zinazohusika mkae,  mratibu, fedha  zote ambazo zilikuwa ziende kwenye sherehe zitumike kurekebisha miundombinu iliyoharibika, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge  na Uratibu, liratibuni hilo…, amesema Dk Nchemba,”

Kwa mujibu wa Dk Nchemba uharibifu uliofanyika Oktoba 29 umehusisha kuharibiwa kwa zaidi ya ofisi 700 za kata nchini, vituo vya polisi, pamoja na nyumba na magari ya watu binafsi.

Hata hivyo, Dk Nchemba amesema mbali na uharibifu uliofanyika Serikali inafanya jitihada za kuhakikisha miundombinu hiyo inafanyiwa ukarabati kwa haraka ili huduma zilizosimama zirejee kama kawaida.

“Mrejeshe masuala ya mawasiliano, masuala ya intaneti, pamoja na masuala ya umeme wakiwepo na Tanesco, pamoja na maeneo mengine ya ukusanyaji wa mapato, ndani ya siku 10 tuone hii shughuli ikirejea katika hali yake ya kawaida,” ameagiza Dk Nchemba.

Aidha, Dk Nchemba amewasisitiza Watanzania kutoshawishika na mtu yeyote kufanya mambo yanayohatarisha usalama wa nchi pamoja na uharibifu wa miundombinu  akisisitiza kuwa licha ya kuwepo kwa mambo ambayo wanataka yafanyiwe mabadiliko ikiwemo katiba, ni muhimu kulinda amani na utulivu wa nchi kwa kuwa mabadiliko hayawezi kufanywa katika hali ya vurugu. 

“Tutaandika tu Katiba kama tuna amani, tunaheshimiana na tunaumoja…hivi vyote mnavyoviona si mali yetu, ni mali yenu wenyewe, sisi mmetupa tu dhamana ya kuvisimamia” amesisitiza Dk Nchemba.

Katika kuhakikisha amani inaendelea kutawala Tanzania, Dk Nchemba pia amezitaka taasisi za dini kuibua hoja zenye nia ya kujenga na si kuwagonganisha wananchi kutokana na mitazamo yao binafsi ambapo pia amemuagiza Waziri wa Mambo ya Ndani kuandika upya miiko na mipaka ya ufanyaji kazi wa taasisi  hizo.

“Ziandikie taasisi zote za kidini kuwakumbusha miiko na mipaka ya ufanyaji kazi, sawa sawa na sheria na katiba ya nchi yetu na masharti ya usajili” amesisitiza Dk Nchemba. 

Aidha, mbali na maagizo ya uangalizi kwa taasisi za kidini, Dk Nchemba ameagiza kufunguliwa na kupewa uangalizi wa miezi sita kwa Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Kawe na kada wa muda mrefu wa Chama Chama cha Mapinduzi (CCM) Askofu Josephat Gwajima ambaye mara kadhaa amekuwa akiikosoa Serikali ya chama hicho. 

“Akikosea sheikh usiadhibiwe msikiti na akikosea sskofu wasiadhibiwe waumini wake,” amesema Dk Nchemba

Kanisa la ufufuo na uzima limetimiza siku 175 tangu lilipofungiwa Juni 2, 2025 ambapo kwa mujibu wa Idara ya Usajili wa Mashirika ilisema kuwa kanisa hilo lilikiuka ‘Societies Act’ kwa kutoa mahubiri yenye siasa ambayo yanaweza kuchochea mgawanyiko kati ya wananchi na Serikali. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks