Mjadala umri sahihi binti kuolewa wachukua sura mpya Tanzania

Lucy Samson 0803Hrs   Machi 28, 2023 Habari
  • Wanaharakati wadai kuruhusu binti kuolewa chini ya miaka 18 ni kumnyima haki zake.
  • Lhrc waitaka Serikali kuharakisha mchakato wa maboresho ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971.

Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimewataka Watanzania kuwapuuzia watu wanaohamasisha watoto wa kike kuolewa katika umri mdogo huku kikiitaka Serikali kuharakisha mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971.

Hivi karibuni kumekuwa na mijadala mpana kwenye jamii juu ya umri sahihi kwa mtoto wa kike kuolewa ambapo baadhi wamekuwa wakiunga mkono Sheria ya Ndoa ambayo inayoruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na miaka 15 kama wazazi wataridhia au miaka 14 kwa amri ya mahakama.

Watu wengine wakiwemo wanaharakati wa haki za binadamu wamekuwa wakitofautiana na msimamo huo na kudai kuwa kuruhusu hilo ni kumkandamiza mtoto wa kike na kumnyima haki yake ya kupata elimu na kufurahia utoto wake kabla hajaingia katika majukumu ya ndoa. 

Majadala huo ulitokana na msimamo wa Baraza Kuu Waislamu Tanzania (BAKWATA)  ambalo linapendekeza mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 11, 12 au 13 aliyeingia kwenye kipindi cha balehe aruhusiwe kuolewa kwa uhalali wa mahakama utakaozingatia vielelezo vya kimazingira.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga(Kushoto)akisistiza jambo kwenye mkutano wa wanahabari jijini Dar es Salaam, kulia ni Getrude Dyabene kutoka LHRC. Picha|LHRC. 

Bakwata ilitoa maoni hayo Machi 22, 2023 wakati ilipokutana na wajumbe wa kamati ya kupitia mfumo wa haki jinai Tanzania iliyopewa jukumu hilo na Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni. 

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga amesema mapendekezo kama hayo yaliyotolewa na Bakwata yanarudisha nyuma juhudi za kumkomboa mtoto wa kike dhidi ya imani, mila na desturi kandamizi.

“Ndoa hizi mara nyingi husababishwa na hali duni za kimaisha, mila na desturi zilizopitwa na wakati, ukeketaji, ukosefu wa elimu juu ya madhara ya ndoa za utotoni,” amesema Wakili Henga leo Machi 28, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. 

Mkurugenzi huyo ameainisha baadhi ya nchi zilizopitisha sheria za kumlinda mtoto asiolewe chini ya umri wa miaka 18 ikiwemo Tunisia ambayo umri wa kuoa na kuolewa ni miaka 20.


Soma zaidi:


Mabadiliko ya sheria ya ndoa

LHRC  imeitaka Serikali kutii amri ya mahakama na kuharakisha mchakato wa kutunga sheria itakayoweka umri wa chiini wa kuoa na kuolewa kwa wavulana na wasichana kuwa miaka 18 kwani ndio umri wa mtu mzima kwa Tanzania.

Mwaka  2016,  Mahakama Kuu ya Tanzania ilitoa hukumu katika kesi aliyofungua Mwanaharakati na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Her Initiative, Rebeca Gyumi iliyopinga mtoto wa kike kuolewa akiwa na miaka 15 kwa ridhaa  ya wazazi na miaka 15 kwa amri ya mahakama.

Katika kesi hiyo mahakama ilikubali uwepo wa vifungu vya Sheria ya Ndoa vinavyopingana na Katiba ya nchi kwa kuweka umri tofauti wa kuoa au kuolewa kati ya mtoto wa kike na wa kiume.

Mahakama hiyo iliitaka Serikali kupitia kwa Mwanasheria Mkuu kujipanga kuvirekebisha vifungu ndani ya mwaka mmoja.

Licha ya miaka saba kupita tangu kutolewa kwa maamuzi hayo ya mahakama, hakuna mabadiliko yoyote ya sheria hiyo na vipengele vyake yaliyofanyika.

Mara kwa mara Serikali imekua ikikiri kwamba kushindwa kubadili kifungu hicho ni kutokana na unyeti wa kitamaduni na wa kidini juu ya jambo hilo.

Pia katika shauri lililofunguliwa na LHRC dhidI ya Serikali ya Tanzania katika Kamati ya Wataalamu ya Afrika ya Haki na Ustawi wa Mtoto, iliyomalizika mwaka 2022, Serikali ya Tanzania iliamriwa na kamati hiyo kuchukua hatua stahiki kuondoa kabisa ndoa za utotoni na mila nyingine kandamizi.

Sambamba na hilo Serikali iliamriwa  kuhakikisha wanatatua visababishi vya ndoa za utotoni ikiwemo ubaguzi, umasikini, mila na desturi zilizopitwa na wakati.

Related Post