Ujenzi meli kubwa kuliko zote Ziwa Victoria wafikia pazuri

March 28, 2023 6:13 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Meli mpya ya Mv Mwanza hapa kazi tu inayojengwa ndani ya Ziwa Victoria kwa gharama ya zaidi ya Sh109 bilioni. Picha | Mariam John.


  • Tayari iko majini Ziwa Victoria.
  • Marekebisho ya ndani yanafanyika kwa sasa. 
  • Itainua uchumi wa Mkoa wa Mwanza ikikamilika. 

Mwanza. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeridhishwa na ujenzi meli mpya ya Mv Mwanza inayojengwa ndani ya Ziwa Victoria na kueleza kuwa kukamilika kwake kutachochea ukuaji wa uchumi wa nchi. 

Meli hiyo yenye urefu wa mita 92.6, kimo cha mita 20 na upana wa mita 17 ilianza kujengwa mwaka 2020 kwa gharama zaidi ya Sh109 bilioni na inatarajia kukamilika mwaka huu wa 2023.

Ndani ya meli hiyo kutakuwa na huduma mbalimbali ikiwemo zahanati, huduma za kifedha na sehemu za starehe. Itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo na magari madogo 20.

Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa meli hiyo pamoja na ile ya mizigo ya Mv Umoja, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jerry Silaa amesema wameona kwa vitendo kazi ya ujenzi wa meli hiyo haijasimama na kwamba mara tu itakapokamilika uchumi wa Mkoa wa Mwanza utaenda kuboreka na kuimarika.

“Tumeridhishwa na kazi inayofanyika hapa, na hii imeonyesha dhahiri fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili uwekezaji zinafanya kazi sawa na malengo, zaidi ya Sh60 trilioni zimetolewa kwa makampuni ya umma kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” amesema Silaa.

Amesema kamati yake imeshuhudia kila sehemu waliyopitishwa ndani ya meli hiyo kuna vijana wa kitanzania wakiendelea na majukumu yao sehemu mbalimbali ikiwemo sehemu ya injini, mitambo ya uongozaji na uchomeleaji.

“Hii ni dhahiri kuwa kuna teknolojia kubwa imehamishwa kutoka kwa wageni kwenda kwa vijana wa kitanzania, na kwamba baada ya kazi hiyo kukamilika kuna baadhi ya vijana watapata ajira ya kudumu kwenye kampuni hiyo ili waweze kusimamia miradi ya maendeleo,” amesema Silaa.

Msimamizi wa miradi kutoka Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Abel Gwanafyo amesema tangu Februari 12 mwaka huu, meli iliposhushwa majini.

Kazi kubwa inayofanyika hivi sasa ni za ndani za kufunga vitanda, viti,  mifumo ya umeme na kuunganisha mitambo ili ije ijaribiwe kabla ya kukabidhi meli.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bodi ya MSCL, John Mbungo amewaahidi wananchi kuwa kamati hiyo itafanya kazi kwa ufanisi na kwa wakati  na kwamba kamati iko macho kuhakikisha mambo yote yanafanyika kwa wakati.

“Niwaahidi wananchi kuwa kamati inayofanyika hapa itakamilika kwa wakati ili waweze kuona matunza ya kazi hiyo ambayo yataenda kuibadilisha mkoa wa Mwanza na taifa kwa ujumla,” amesema Mbungo.

Enable Notifications OK No thanks