Mikopo ya nyumba yapaa Tanzania

March 12, 2020 9:48 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Mikopo ya nyumba iliyotolewa na benki za biashara iliongezeka hadi kufikia Sh438.5 bilioni Desemba 31, 2019 kutoka Sh421.1 bilioni iliyorekodiwa Desemba 31, 2019. 
  • Ongezeko hilo ni sawa na asilimia nne ndani ya kipindi cha mwaka mmoja. 
  •  Imechagizwa na ongezeko la benki zinazotoa mikopo hiyo na mahitaji ya nyumba za kuishi nchini. 

Dar es Salaam. Ripoti mpya ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza kuwa mikopo ya nyumba inayotolewa na benki za biashara imeongezeka kwa asilimia nne katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ukichagizwa na ongezeko la benki zinazotoa mikopo hiyo na mahitaji ya nyumba za kuishi nchini. 

Ripoti hiyo ya soko la mikopo ya nyumba (Tanzania Mortgage Market Updates) iliyotolewa na BoT kwa kushirikiana kampuni ya Tanzania Mortgage Refinance Ltd hivi karibuni inaeleza kuwa mikopo ya nyumba iliyotolewa na benki za biashara iliongezeka hadi kufikia Sh438.5 bilioni Desemba 31, 2019 kutoka Sh421.1 bilioni iliyorekodiwa Desemba 31, 2019.

Ongezeko hilo ni sawa na asilimia nne ndani ya kipindi cha mwaka mmoja. 

Katika ripoti hiyo, BoT inaeleza kuwa ongezeko la mikopo ya nyumba inayotolewa na taasisi za benki kumechangiwa na ongezeko la mahitaji ya nyumba za kuishi na watu wanatumia fursa ya mikopo hiyo kujipatia makazi bora.

“Mahitaji ya nyumba Tanzania kila mwaka yanakadiriwa kufikia nyumba 200,000 kila mwaka na kuna upungufu wa nyumba milioni 3 za makazi ya watu, kumechochea upatikanaji rahisi wa mikopo ya nyumba,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Pia hatua ya Serikali kuhamia jijini Dodoma imechochea wawekezaji kutumia fursa ya mikopo hiyo kujenga miundombinu na nyumba za makazi kwa ajili ya kupangisha na kuuza. 


Soma zaidi:


Hata wakati mikopo ya nyumba ikiongezeka, taasisi za fedha zinazotoa mikopo hiyo nazo zimeongezeka katika kipindi hicho, jambo linaloimarisha ushindani baina yao na kuwafaidisha zaidi wananchi wenye uhitaji wa nyumba. 

Idadi ya watoa mikopo ya nyumba imeongezeka hadi kufikia 34 mwaka jana kutoka 32 iliyorekodiwa mwaka 2018 baada ya benki mbili za Ecobank na Benki ya Posta Tanzania (TPB) kuingia katika soko hilo.

Kuongezeka kwa ushindani wa taasisi zinazotoa mikopo hiyo kumesaidia kushusha riba kutoka asilimia 22 iliyokuwa inatumika mwaka 2009 hadi asilimia 15 mwaka jana.  

Hata hivyo, soko la mikopo ya nyumba limetawaliwa na benki tano ambazo ni CRDB, Stanbic, Azania, NMB na KCB ambazo zote kwa pamoja zinatawala soko kwa asilimia 68.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa jitihada zinahitajika kuiimarisha sekta hiyo kwa sababu inakabiliwa na changamoto nyingi gharama kubwa za nyumba na riba ambayo siyo rahisi kwa Watanzania wa kawaida kumudu. 

“Wakopeshaji wengi wanatoa mikopo ya kununua nyumba na kupangisha wakati wachache wanatoa mikopo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba binafsi ambapo kwa sehemu kubwa imeendeelea kuwa ni gharama ambayo haiwezi kufikiwa na Watanzania wa kawaida,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Enable Notifications OK No thanks