Wafanyabiashara kuunganishwa kwenye jukwaa la vifaa vya ujenzi Dar
- Inakadiriwa kuwa nyumba 200,000 huhitajika kila mwaka kukidhi ongezeko la idadi ya watu.
- Hali hiyo inafungua milango kwa wafanyabiashara kusambaza malighafi na vifaa vingi kwa wanunuzi.
- Wadau waandaa jukwaa kuwakutanisha wauzaji na wanunuzi wa vifaa vya ujenzi.
Mfanikio ya ujenzi hutegemea zaidi upatikanaji wa malighafi na vifaa. Picha| Huktersure.
Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi huenda wakatengeneza faida kubwa mwaka huu wa 2018 kutokana na ongezeko la idadi ya watu na mahitaji ya nyumba za kuishi katika maeneo mbalimbali nchini.
Ujenzi wa majengo ya biashara au makazi ya kuishi hutegemea zaidi upatikanaji wa vifaa na malighafi za ujenzi ambazo katika maduka mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2016 kuhusu mikopo ya ujenzi wa nyumba inaeleza kuwa mahitaji ya nyumba nchini yanakadiriwa kufikia nyumba 200,000 kila mwaka ambapo mpaka sasa kuna upungufu wa nyumba 3 milioni za makazi ya watu hasa katika majiji makubwa kama Dar es Salaam.
Mahitaji ya nyumba yanachochewa zaidi na ongezeko la idadi ya watu kila mwaka. Hali hiyo ndiyo inayoyafanya mashirika mashirika mbalimbali ya umma na binafsi kujitokeza kuchangamkia fursa ya kujenga nyumba za bei nafuu ambazo hupangishwa au kuuzwa kwa watu.
Ujenzi wa nyumba inahitaji vifaa na malighafi za uhakika ambazo zinaweza kupatikana wakati wote wa ujenzi ili kuhakikisha watumishi na watu binafsi wanapata nyumba bora za kuishi.
Meneja Miradi wa Maonyesho ya Vifaa vya Ujenzi (Dar Construction Expo 2018) yanayotarajiwa kufanyika Septemba 27 hadi 29, 2018 Jijini Dar es Salaam, Stephen Sange amesema kutokana na ongezeko la mahitaji ya nyumba nchini, Tanzania itakuwa sehemu muhimu kwa wafanyabiashara kusambaza vifaa vya ujenzi na kujipatia faida kubwa.
“Kwa fursa kubwa kama hiyo, Tanzania inakuwa soko muhimu Afrika kwa usambazaji wa vifaa vya ujenzi,” amesema Sange.
Amebainisha kuwa wameendaa maonyesho makubwa ya ujenzi ambayo yatakuwa jukwaa la kuwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara na kampuni za ujenzi ili kujionea bidhaa na kutengeneza mtandao wa biashara utakaorahisisha upatikanaji wa malighafi na vifaa kwa wakati.
“Maonyesho ya Ujenzi Dar yanakupa jukwaa la kuunda mahusiano ya kibiashara na kukuza biashara yako,” amesema Sange.
Maonyesho hayo yatakuwa sehemu ya kuunufaisha Mfuko wa Nyumba za Watumishi wa Umma (PSHS) unaosimamiwa na Kampuni ya Watumishi Housing (WHC) kwa ushirikiano na kampuni ya Uendelezaji Majengo ya Real Estate Investment Trust (REIT) wanaokusudia kujenga nyumba 50,000 kwa awamu tano ili kuwapunguzia watumishi umma hadha ya makazi ya kuishi.
Awamu ya kwanza ya mradi huo ilianza mwaka 2015 ambapo ilifanikiwa kuwapunguzia watumishi 10,000 kati ya 650,000 ambao walikuwa wana mahitaji ya nyumba kupitia mifuko mbalimbali ya nyumba za bei nafuu.
Katika kuhakikisha inatekeleza mradi wa nyumba kwa wakati, WHC imesaini mkataba na benki za CRDB, Azania, NMB na Benki ya Africa ili kuwapatia wafanyakazi mikopo ya nyumba itakayolipwa kwa miaka 25 ijayo kwa riba ndogo ya asilimia 11 hadi 13 badala ya sasa ya asilimia 16 hadi 19 (16-19%)
Kulingana na mtandao wa Numbeo unaojihusisha na masuala ya ubora maisha katika majiji, bei ya nyumba kwa mita moja ya mraba ni Dola za Marekani 1,200 katika Jiji la Dar es Salaam ukilinganisha na Jiji la Nairobi (Dola 1,235) na ikiwa mtu anataka kununua nje ya Dar es Salaam basi atalipia mita ya mraba kwa Dola 608.17