Mfahamu mhandisi Patrick Mfugale ‘kichwa’ nyuma ya flyover ya Tazara

September 29, 2018 10:50 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ametumia muda wake mwingi wa kazi kama mtaalamu wa madaraja akibuni na kusimamia madaraja makubwa na madogo yapatayo 1,400 nchini Tanzania.
  • Weledi wake na utumishi wa muda mrefu katika uhandisi wafanya flyover ya kwanza Tanzania ipewe jina lake.
  • Rais Magufuli aeleza kuwa kuna siku Mfugale aliwahi kuamka nje ya nyumba aliyokuwa amelala pamoja na wakandarasi wenzie huko Songea kutokana “uhandisi” wa watu wa Songea.

Huenda umesikia hivi karibuni kuwa barabara ya kwanza ya juu Tanzania (flyover) iliyopo katika makutano ya Barabara ya Mandela na Nyerere imepewa jina “Mhandisi Patrick Mfugale”. Je, umeshajua kwanini flyover hiyo imepewa jina hilo?

Kwa wachache huenda waliwahi sikia jina hilo la Mfugale kama Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads). Lakini kuna mengi zaidi yanayomhusu mhandisi Mfugale zaidi ya cheo chake Tanroads kiasi cha kufanya flyover hiyo ipewe jina lake.

Mfugale ni moja ya waandisi wakongwe nchini waliotoa mchango mkubwa katika sekta ya ujenzi hususan katika ujenzi wa barabara baada ya kulitumikia taifa kwa miaka 41 akiongoza usanifu na usimamizi wa baadhi ya madaraja mbalimbali nchini. 


Safari yake ya Elimu

Katika uzinduzi wa flyover hiyo ya Tazara, Mfugale ndiye alikuwa habari ya mjini. Karibu kila aliyepata fursa ya kuzungumza alimtaja na kumshukuru kwa kazi yake. Lakini safari ya mtaalamu huyo ilianzia wapi?

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wahandisi Tanzania (ERB) Profesa Ninatubu Lema,  Mfugale alizaliwa huko Ifunda mkoani Iringa ambapo na kupata elimu yake ya msingi mkoani humo. Prof Lema alipata wasaa wa kumueleza mutaalamu huyo leo (Septemba 27, 2018) wakati wa uzinduzi wa flyover hiyo yenye urefu wa mita 425 na uwezo wa kubeba tani 180 kwa wakati mmoja. 

Katika safari yake hiyo ya masomo, Mfugale alifanikiwa kumaliza elimu ya sekondari mwaka 1975 katika Shule ya Sekondari Moshi akimzidi darasa moja Prof Lema. Alipata shahada ya kwanza ya uhandisi mwaka 1983 kutoka Chuo Kikuu cha Rokii India na shahada ya pili kutoka Chuo Kikuu cha Loughborough Uingereza mwaka 1995. Kama bahati, Mfugale alikutana na Prof Lema katika chuo hicho wakisaka maarifa zaidi. 


Safari ya miaka 41 ya utumishi

Hata wakati akiendelea kuwa bosi wa Tanroads, Mfugale tayari ameshalitumikia taifa kwa zaidi ya miaka 41 sasa. 

Prof Lema amesema Mfugale  aliajiriwa wizara ya ujenzi mwaka 1977 kama fundi sanifu na baadaye kupanda cheo hadi kuwa mkurugenzi wa barabara za mikoa mwaka 1992. Aliteuliwa kuwa mhandisi mkuu wa madaraja nchini mwaka 1992 na akiwa masomoni Uingereza mwaka 1995 alitafiti na kutengeneza mfumo wa usimamizi wa madaraja nchini. 

Pamoja na kuanza kazi mapema, Mfugale alisajiliwa kama mhandisi mtaalamu mwaka 1991, mhandisi mshauri mwaka 2014 na pia ni mwanachama wa chama cha wahandisi Tanzania. Pia, amekua mkuu wa bodi mbalimbali nchini.


Zinazohusiana: 


Utumishi wa kukumbukwa

Katika maisha yake ya kitaaluma, Mfugale ametumia muda wake mwingi wa kazi kama mtaalamu wa madaraja akibuni na kusimamia madaraja makubwa na madogo yapatayo 1,400 nchini Tanzania.

 Miongoni mwa kazi zake adimu ni ubunifu wake wa daraja la Malagarasi lenye urefu wa mita 178 kwa muda wa miezi mitatu kwa gharama ya Sh300 milioni kwa wakati huo.

Hata hivyo, wengi kwa sasa wanalifahamu Daraja la Nyerere linalounganisha sehemu ya kati ya jiji na Kigamboni ambalo ni kwanza kujengwa baharini nchini lenye urefu wa mita 680 na upana wa mita 32. Kwa waliobahatika kupita au kusoma habari za daraja hilo  lililogharimu kiasi cha Sh214.6 bilioni, basi miongoni mwa vichwa nyuma ya usanifu wake ni Mfugale ukiachana na nafasi yake ya kusimamia kama kigogo wa Tanroads. 

 Mfugale amehusika katika ujenzi wa madaraja mengine mengi kama daraja la Mkapa lenye urefu wa kilometa 10 likiwa ni daraja refu kuliko yote Afrika Mashariki na kati, daraja la Rufiji, daraja la Umoja ambalo lina unganisha Tanzania na Msumbiji na daraja jipya la Magufuli lililopo Kilombero mkoani Morogoro.


Mfugale yupo hadi kwenye ujenzi wa reli ya kisasa (SGR)

Ukiachana na madaraja ambayo yamemtambulisha vilivyo, Prof Lema amesema mhandisi huyo amebuni na kusimamia barabara za kitaifa zenye urefu wa kilometa 36,258 na kati ya hizo kilometa 9,951 ni za lami. 

“Amekua mwenyekiti wa kikosi cha wataalamu cha ujenzi wa reli ya kisasa SGR, ujenzi wa Dodoma Sports Complex na ni mjumbe wa timu ya majadiliano ya mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge nchini,” amesema Prof Lema.

Kutokana na kazi yake hiyo, Mfugale amepokea tuzo mbalimbali  ambapo mwaka 2003 alipokea tuzo ya mafanikio katika fani ya uandisi (Distinguished engineering accomplishment award) inayotolewa ERB na kupendekezwa kutunukiwa tuzo ya mhandisi bora mwaka 2018 (Engineering excellence award) na bodi hiyo hiyo. 

Ukiachana na tuzo hizo, heshima kubwa zaidi ni barabara ya kwanza ya juu nchini iliyogharimu zaidi ya Sh106 kupewa jina lake. 


 Changamoto alizopitia katika Utendaji wake

Kila kazi na changamoto zake. Akihutubia wananchi katika uzinduzi wa flyover hiyo,  Rais John Magufuli amesema Mfugale amepitia changamoto nyingi  katika utumishi wake ikiwamo kuamka nje ya nyumba aliyokuwa amelala pamoja na wakandarasi huko mkoani Ruvuma.

“Mfugale akiwa Songea kwa watani zangu wakiwa wamejenga kambi Matomondo na Kimesela, jioni yake walilala kwenye hako kajumba kesho yake waliamka saa nne wapo nje,” amesema Rais Magufuli huku akitania “huu ndiyo uhandisi wa watani zangu wa Songea.”

Amesema pia katika ujenzi wa barabara huko huko Matomondo fremu za greda ziliwahi kukatika wakati wa shughuli za utengenezaji wa barabara. Rais Magufuli alisema kazi hiyo iliendelea baada ya marehemu mzee Gama kuwaomba wanakijiji wa eneo hilo kuruhusu muendelezo wa utengenezwaji wa barabara hiyo kwa kuwa ilikuwa na manufaa kwao.

Rais Magufuli pia alisema Mfugale amewahi kukaa ofisini bila kulala kwa siku tatu akibuni daraja la Umoja na kusahaulika katika utambulisho wa ufunguzi ya daraja hilo.

“Nilipopata nafasi ya kusalimu nikataja tumpongeze Mfugale kwa daraja hili,” amesema Magufuli.

Rais Magufuli amemweleza Mfugale kama mchapakazi, mzalendo, mbunifu na mwaminifu katika kazi zake na kwamba hakupendelewa kwa uamuzi wa flyover hiyo kupewa jina lake.


“Kwa naamna ya pekee ni mpongeze mtendaji mkuu wa Tanroad Mhandisi Patric Mfugale kwa kusiriki kubuni nakusimamia michoro katika kutelekeza mradio huu,” amesema Rais Magufuli akizungumza kabla ya kuzindua Flyover hiyo.

Huyo ndiye Mhandisi Patrick Mfugale.

Enable Notifications OK No thanks