Rais Magufuli akosoa mapendekezo ya ripoti ya mazingira Stiegler’s Gorge
- Asema baadhi ya mapendekezo yaliyopo katika ripoti hiyo yamelenga kukwamisha mradi huo unaotarajiwa kuzalisha umeme wa 2100MW.
- Awaponda wataalamu wazawa waliotoa mapendekezo hayo kuhusu tathmini ya mazingira katika Pori la Akiba la Selous.
- Awashutumu kwa kutumiwa na mataifa makubwa kukwamisha miradi ya maendeleo.
- Rais Magufuli aeleza kuwa mradi wa Stiegler’s Gorge unalenga kumaliza tatizo la umeme na kuchagiza uchumi wa viwanda.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameagiza kufanyika kwa marekebisho ya mapendekezo ya ripoti ya tathmini ya mazingira kuhusu ujenzi wa mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge akikosoa kuwa baadhi hayatekelezeki na ni kikwazo katika ufanikishaji wa mradi huo.
Mradi wa Stiegler’s Gorge, unatarajiwa kujengwa katika Pori la Akiba la Selous, umekuwa ukipingwa na watetezi wa mazingira kwa madai kuwa siyo rafiki kwa viumbe hai ambao wako hatarini kutoweka. Baadhi walikuwa wakisubiri kuona mapendekezo ya ripoti hiyo iwapo ingeruhusu ujenzi huo ama la.
Hata hivyo, leo (September 27, 2018) wakati wa uzinduzi wa barabara ya juu ya Mfugale (Mfugale Flyover) iliyopo katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela (TAZARA), Rais Magufuli amesema mapendekezo yaliyotolewa na wataalamu wa mazingira katika ripoti hiyo ni kikwazo katika kuwaondolea watanzania adha ya ukosefu wa umeme.
“Nimeshatoa maelekezo wayabadilishe hayo yote waliyoyaandika na ole wake nimkute huyu mtaalam bado yuko salama ni lazima tujenge maslahi ya nchi yetu kwanza,” amesema Rais.
Dk Magufuli amesema moja ya mapendekezo hayo ni zuio la ujenzi wa vyoo ndani ya eneo la mradi jambo ambalo ni gumu kulitekeleza kwa kuwa wafanyakazi watapata tabu kupata sehemu ya kujisaidia.
“Baadhi ya mambo waliyoyapendekeza kwamba ili tujenge Stiegler’s Gorge wafanyakazi wote watakaokuwa wanafanya pale ambao ni watanzania wasiwe wanajisaidia au wasiwe wanatengeneza vyoo maeneo hayo lazima wawe wanajisaidia choo kiwe kinapelekwa kilomita 10 nje ya eneo hilo,” amesema Rais.
Amesema hata wakiwazuia kujenga vyoo, bado uchafu au kinyesi kitaletwa kwa njia mbalimbali ikiwemo mito inayokatiza eneo la pori hilo.
Pendekezo lingine lililotolewa, kwa mujibu wa Rais, ni kufanya ufuatiliaji wa vitu vyote (Screaning) vitakavyopelekwa eneo la mradi ikiwemo kupima udongo na mboga mboga zitakazolimwa ili isiwe sehemu ya uharibifu wa mazingira
“Wataalam hao wakapendekeza kwamba kama kuna injini au kuna gari limeharibikia pale lisitengenezewe hapo hata kama unatoa oil (mafuta). Mambo mengine ya hovyo,” amesema Dk Magufuli akionekana kuchukizwa na mapendekezo hayo.
Aidha emesema mapendekezo hayo na mengine yametolewa kwa shinikizo la watu wa nje ambao hawana nia njema na mradi huo wa megawati 2100 za umeme ambao Serikali inakusudia kujenga ili kupunguza tatizo la umeme nchini.
“Tusijifunze utaalam wa kutumiwa na watu wa nje ni kwa vyovyote watu wasioitakia mema Stiegler’s Gorge hawawezi kutaka sisi tupate umeme wanataka walete majenerata yao watuuzie kwa bei ya juu tuendelee kuwa watumwa katika maisha yote,” amebainisha.
Zinazohusiana:
- Rais Magufuli kuzuru Mwanza, Simiyu na Mara kwa siku saba
- Umemejua kimbilio kwa waliopitwa na gridi ya taifa.
- Megawati 300 za umeme wa upepo kuchagiza ukuaji wa viwanda Tanzania.
Upatikanaji wa umeme bado changamoto
Rais Magufuli ameeleza kuwa bei ya umeme bado iko juu kuliko maeneo mengine, hali inayowafanya watanzania kushindwa kuwekeza katika shughuli ndogo ndogo za uzalishaji mali.
Mathalani, uniti moja ya umeme hapa nchini, amesema, inauzwa kwa senti za Marekani 10.7 ambapo kuna utofauti mkubwa ukilinganisha na nchi zilizoendelea kama Marekani ambao huuza kwa senti 0.12 na Uingereza senti 0.15.
“Kama umeme wetu ni bei ghali maana yake hatuwezi tukashindana katika soko la viwanda bidhaa zetu siku zote zitakuwa za bei ya juu kuliko bidhaa za wenzetu wanazotengeneza kwa bei ya umeme kidogo,” amesema Rais.
Kwa sasa uwezo wa nchi kuzalisha umeme umefikia megawati 1,560 ambapo chanzo kikubwa ni umeme unaotokana na maji, gesi na makaa ya mawe lakini ujenzi wa mradi wa Stiegler’s Gorge utazalisha megawati zaidi ya 2,100 na kumaliza tatizo la umeme.
Kumekuwa na maoni tofauti ya wadau wa mazingira kuhusu mradi huo unaotarajiwa kuchukua asilimia tatu ya eneo la pori hilo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 50,000.
Hata hivyo, Serikali imesema itaendelea kujenga mradi huo ambao unatarajia kugharimu Dola za Marekani 3.5 bilioni au takriban Sh8 trilioni.