ACT-Wazalendo wazidi kukomaa na Serikali ripoti ya CAG
- Yaibua hoja 10 baada ya kufanya uchambuziq wa ripoti hiyo.
- Yaitaka Serikali kuwawajibisha wahusika waliotia hasara.
Dar es Salaam. Chama cha upinzani cha ACT wazalendo kimeikosoa Serikali kwa kuupuza mapendekezo ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) huku kikibainisha mambo 10 yanayopaswa kufanyiwa kazi kwa haraka likiwemo udhibiti wa ukuaji wa deni la taifa.
Waziri Mkuu Kivuli wa ACT-Wazalendo Isihaka Mchinjita amewaambia wanahabari kuwa licha ya CAG kutoa ripoti kila mwaka lakini hakuna hatua za kina zinazochukuliwa dhidi ya waliohusika na ukiukwaji wa sheria na taratibu za matumizi ya fedha za umma.
“Tija ya Serikali ya CCM ni kuendeleza ufujaji na upigaji, tija ya CCM sio ustawi wa wananchi. Tija ya CCM ni kutufanya tuendelee kuwa mateja wa mikopo,’’ amesema Mchinjita jijini Dar es Salaam leo Mei 10, 2025.

Jambo la pili walioanisha ACT ni malimbikizo ya madeni kwa wafanyakazi na mafao kutokupelekwa kwenye mifuko kwa wakati.
Kwa mujibu wa Mchunjita, CAG amebainisha madeni kutoka kwa wazabuni na wakandarasi takribani Sh4.56 trilioni ambayo hayajalipwa ikiwa ni madai ya wakandarasi na wazabuni hali inayokwamisha miradi ya maendeleo.
Mambo mengine ambayo ACT wazalendo wanataka yafanyiwe kazi ni kumaliza hujuma na usimamizi mbovu wa mashirika ya umma na kutokutolewa kwa fedha za Mchango wa Kampuni kwa Jamii (CSR) Sh262.34 bilioni za mradi wa bwawa la Umeme la Julius Nyerere.
Kiongozi huyo amekosoa uwekezaji kiduchu kwenye miundombinu ya barabara kiasi cha kufanya baadhi kutopitika ikiwemo barabara ya kutoka Rufiji kwenda Mtwara.
Badala ya kuhakisha ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na makusanyo, Mchinjita ameeleza kuwa CAG ameendelea kubaini ubadhirifu kwenye mauzo, manunuzi, mikataba, makusanyo, ruzuku, matumizi na malipo.
“Ripoti ya CAG kwa mwaka wa fedha 2023/24, imebainisha hoja za ubadhirifu unaotokana na upotevu fedha, ufisadi na ukiukwaji wa sheria za manunuzi zenye thamani ya Sh2.56 trilioni,’’ amesema Mchinjita.
Ili kuboredha uwajibikaji, ACT Wazalendo wameitaka Serikali kuwachukulia hatua watumishi wote wanaohusika na ubadhirifu wa rasilimali za umma.
“Licha ya hasara zote hizi kuwa wazi na kurudiwa kila mwaka lakini watu ambao wanayafanya haya hatuoni hatua zozote zikichukuliwa,’’ amesema Waziri Kivuli wa Fedha wa ACT, Kiza Mayeye.
Latest



