Matumizi ya intaneti yanavyofichua fursa zilizojificha kwenye 'smartphones'

Daniel Mwingira 0742Hrs   Januari 28, 2019 Teknolojia
  • Matumizi ya intaneti yameongezeka kidogo hadi milioni 23.14 mwaka 2018 ikiwa ni mara tatu zaidi ya kiwango kilichowahi kufikiwa miaka sita iliyopita. 
  • Matumizi hayo yanachagiza ukuaji wa huduma na biashara mtandaoni kwa wajasiriamali nchini hasa katika kutangaza au kutoa huduma zao ili kuweza kuwafikia wateja wengi.
  • Intaneti isiyohamishika imeendelea kupata watumiaji wengi huku intaneti isiyohamishika matumizi yake yanapungua kila mwaka.

Dar es Salaam. Sekta ya mawasiliano nchini imendelea kushika hatamu baada ya watumiaji kuongezeka kidogo hadi milioni 23.14 mwaka 2018 ikiwa ni mara tatu zaidi ya kiwango kilichowahi kufikiwa miaka sita iliyopita. 

Takwimu mpya za robo ya mwisho wa mwaka 2018 za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuwa idadi ya watumiaji wa intaneti walifikia millioni 23.14 Desemba 2018 ikilinganishwa na milioni 22.99 waliokuwepo kipindi kama hicho mwaka 2017.

Ukuaji huo wa watumiaji wa intaneti kati ya mwaka 2017 na 2018 ni mdogo ukilinganisha na ule uliorekodiwa kati ya mwaka 2017 na 2016. Katika kipindi cha mwaka jana na juzi watumiaji wa intaneti waliongezeka kwa asilimia 0.65 ikilinganishwa na asilimia 15 iliyoripotiwa kati ya mwaka 2016 na 2017.

Ahueni imendelea kuonekana zaidi kwa watumiaji wa  intaneti inayohamishika (mobile wireless) ambayo hutumika zaidi na simu za mkononi, tableti (tablet) na kompyuta mpakato (laptop) imendelea kukuwa takribani mara tatu ndani ya mwaka mmoja kutoka watumiaji milioni 19 mwaka 2017 hadi milioni 22.2 mwaka 2018.

Idadi ya watumiaji wa aina hiyo ya intaneti ni sawa na asilimia 96.2 ya watumiaji wote wa intaneti nchini. Hiyo ni sawa na kusema kwa kila watumiaji wa intaneti 96 kati ya 100 wanatumia intaneti inayohamishika.

Hali hiyo inatokea wakati tovuti za habari na luninga za mtandaoni sasa zikihitajika kusajiliwa na Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2018 (Online Content Regulations 2018) zinazosimamiwa na TCRA ili kutambulika rasmi. Hadi Novemba 12, 2018 televesheni za mtandaoni zipatazo 91 na blogu 63 zilikuwa zimesajiliwa.  

Intaneti inayohamishika inayotmika zaidi na simu na 'laptop' imekuwa ikisaidia kufungua fursa za ajira na biashara zilizopo mtandaoni. Picha| Daniel Samson.

Katika takwimu hizo zilizochapishwa hivi karibuni watumiaji wa intaneti isiyokuwa waya na isiyohamishika (Fixed Wireless) nao wamezidi kuporomoka hadi 697,216 Desemba 2018 ikiwa ni pungufu zaidi ya mara nne ya ilivyokuwa mwaka 2017 ambapo kulikuwa na watumiaji milioni 3.46.

Kiwango cha chini zaidi kuwahi kurekodiwa katika kipengele hicho cha intaneti ilikuwa mwaka 2015 baada ya TCRA kuripoti kuwa kulikuwa na watumiaji 662,882 wa intaneti isiyo na waya na isiyohamishika.


Zinazohusiana:


Hali kadhalika watumiaji wa intaneti ya waya isiyohamishika (Fixed wired) nao wamezidi kushuka kwa zaidi ya mara tatu kutoka watumiaji 520,698 mwaka 2017 hadi watumiaji 164,017 ikiwa ni kiwango cha chini zaidi kuwahi kurekodiwa ndani ya miaka sita iliyopita. 

Mtaalamu wa programu za kompyuta kutoka kampuni ya Code for Africa (CFA), Clemence Kyara amesema kushuka kwa watumiaji wa intaneti isiyokuwa waya na isiyohamishika (Fixed Wireless) na ile  ya waya isiyohamishika (Fixed wired) kunaweza kuchangiwa na uboreshaji wa simu janja za mkononi.

Amesema pia kushuka kwa matumizi hayo kunachangiwa na gharama za matumizi katika aina hizo za intaneti.

"Mtu mmoja ua hata kampuni changa siku hizi wanatumia intaneti za simu janja kwa sababu zimeboreshwa hata gharama zake ni nafuu ndiyo maana naona hata watumiaji wa intaneti kwenye simu wanazidi kuongezeka kila kukicha,''amesema Kyara.


Ukuaji huu wa watumiaji wa intaneti inayohamishika inachagiza ukuaji wa huduma na biashara mtandaoni kwa wajasiriamali nchini hasa katika kutangaza au kutoa huduma zao ili kuweza kuwafikia wateja wengi.

Mathalani watu wengi hutangaza kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp au Instagram ambapo ili kuweza kutumia vizuri mitandao hiyo ni lazima kupakua programu za simu na kumpyuta zilizopo mtandaoni.

Ikumbukwe upatikanaji wa intaneti nchini umekua mara tatu hadi kufikia asilimia 43 mwaka 2018 kutoka asilimia 17 mwaka 2012.

Upatikanaji huo wa intaneti hapa nchini kwa sasa unazidi wastani wa Afrika ambao ni asilimia 31.2 hadi kufikia Juni 2017 kwa mujibu wa mtandao wa internetworldstats.com ambao hufuatilia matumizi ya intaneti duniani.

Matumizi hayo yanachagiza ukuaji wa huduma na biashara mtandaoni kwa wajasiriamali nchini hasa katika kutangaza au kutoa huduma zao ili kuweza kuwafikia wateja wengi.

Related Post