Matarajio ya wanafunzi elimu ya juu Uchaguzi Mkuu 2020

Daniel Samson 0247Hrs   Septemba 10, 2020 Ripoti Maalum
  • Baadhi ya wanafunzi wapendekeza elimu ya juu itolewe bure na kuboresha mazingira ya kusomea chuoni. 
  • Baadhi ya vyama vyaahidi kuwalipia wanafunzi wa vyuo vikuu ada na kuboresha miundombinu ya vyuo.
  • CCM yasema itaboresha mfumo wa utoaji mikopo na elimu ili wanafunzi wengi wanufaike.

Dar es Salaam. Kila kundi limebeba matarajio yake kwa vyama vya siasa vinavyoshiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ambao utatoa taswira ya Tanzania kwa miaka mitano ijayo. 

Uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba 28 utakuwa uchaguzi wa sita toka nchi  iliporejea kwenye siasa ya mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Kama zilivyo chaguzi zinazofanyika katika maeneo mbalimbali duniani, wanafunzi wanaosoma au wanaojiandaa kusoma elimu ya juu wana mahitaji yao ambayo wangependa Serikali mpya itakayoundwa baada ya Oktoba iwatimizie. 

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Alpha Emanuel ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa anapenda kuona Serikali mpya ikishughulikia upungufu wa hosteli kwa wanafunzi wa vyuo vya umma ili kuwawezesha kupata mazingira rafiki ya kusomea.

“Hosteli zipo lakini hazitoshelezi wanafunzi wote, mkiwa mwaka wa kwanza mnapata hosteli lakini mkifika mwaka wa pili inabidi kila mtu aangalie namna ya kupata sehemu ya kukaa, jambo ambalo linaleta usumbufu na kuongeza gharama,” amesema Emanuel.

Mwanafunzi huyo wa mwaka wa kwanza amesema mikopo inayotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) iwe kwa wanafunzi wote wanaojiunga vyuoni na iwe ya kiwango kinacholingana kukidhi mahitaji ya ada na malazi. 

Wakati Emanuel akitaka mikopo yenye usawa na hosteli, mwenzake kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Frank John matarajio yake ni kuona wanafunzi wote wa elimu ya juu wanasoma bure kwa sababu Serikali inawajibika kuwapatia elimu bila vikwazo vyovyote.

“Akitokea mwanasiasa akasema tutapata elimu bure vyuoni, tutamchagua kwa sababu mikopo haiwafikii wanafunzi wote na inakuwa ni changamoto kusoma bila ada hasa kama unatoka familia maskini,” anasema mwanafunzi huyo.

Matarajio yake mengine ni kuona elimu ya juu inaboreshwa zaidi kwa kutengeneza miundombinu inayokidhi mahitaji ya wanafunzi na wahadhiri na kuboresha mitaala ili elimu inayotolewa iwe ile inayowasaidia wahitimu kutatua changamoto za ukosefu wa ajira.

Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Global Group na Mhamasishaji, Eric Shigongo akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Novemba 2018. Picha| Global Publisher. 


Vyama vinasemaje?

Wakati wanafunzi wakiwa na matarajio yao, baadhi ya vyama vimezungumzia mambo mbalimbali ambayo vitafanya vikichaguliwa ili kuboresha elimu ya juu. 

Huenda wewe ni miongoni mwa wanaoguswa na masuala ya elimu ya juu yaani vyuo na vyuo vikuu, hizi ni baadhi ya ahadi za vyama kwa ngazi hiyo ya elimu:


ACT-Wazalendo kuwasomesha wanafunzi vyuoni bure

Chama cha ACT-Wazalendo katika ilani yake ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2020-2025 kimeeleza kuwa iwapo mgombe wake wa urais Yeremia Maganja atachaguliwa kitalipa ada ya masomo, fedha za vitabu, na gharama za mafunzo kwa vitendo kwa kila mwanafunzi anayedahiliwa kwenye chuo kikuu.

“Itatunga Sheria kuhakikisha kuwa Mikopo ya Elimu ya juu itakuwa ni kwa ajili ya gharama za kujikimu tu (Meals & Accomodations),” inaeleza sehemu ya ilani ya chama hicho. 

Sambamba na hilo itafuta mikopo yote ya miaka ya nyuma iliyotolewa kwa wanafunzi wa elimu ya juu na ya wahitimu wote watakaoingia mikataba maalum na Serikali ya kufanya kazi kwa miaka mitatu mfululizo katika maeneo ya pembezoni na yenye mazingira magumu ya kazi.

ACT-Wazalendo ambayo kauli mbiu yake ni “Uhuru, Haki na Demokrasia” imejinasibu kuwa itatoa ruzuku ya sawa na asilimia 40 ya bajeti ya chuo kwa vyuo vikuu kufanya tafiti mbalimbali zitakazotoa dira na miongozo kwenye fani mbalimbali hasa za sayansi ya jamii ili kuwa na Serikali na jamii inayofanya maamuzi ya kitaalamu. 

“Itaajiri wahadhiri wasiopungua 5,000 kwa miaka mitano ili kupunguza uwiano mkubwa uliopo kati ya wahadhiri na wanafunzi,” inaeleza ilani ya chama hicho kwa mwaka 2020-2025.



Pia imeeleza kuwa itaboresha mazingira ya vyuo hasa ujenzi wa vyoo na mifumo ya maji safi na majitaka, kudhibiti ubora wa vyuo vikuu binafsi ili kuhakikisha kila chuo kinaandaa wahitimu walio bora na wenye weledi wa hali ya juu.

“Itaanzisha vyuo vikuu vya Taifa vipya vitano vyenye uwezo wa kudahili wanafunzi wasiopungua 20,000 kila kimoja, vitatu Tanzania Bara (Mtwara, Kigoma na Tanga), viwili Zanzibar (Pemba na Unguja),” kimeeleza chama hicho katika ilani yake ambacho mgombea wake wa urais ni Benard Membe, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania. 


CCM kuboresha mfumo wa utoaji mikopo

Wakati ACT-Wazalendo ikijinasibu kuwa kitawalipia ada wanafunzi wote wa vyuo vikuu, chama tawala CCM katika ilani yake kimeeleza kuwa kitaimarisha na kuboresha mfumo wa ugharamiaji wa elimu ya juu, ikiwemo Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ili kuhakikisha wanafunzi wengi zaidi wenye uhitaji na sifa stahiki wanapata fursa ya kujiunga na elimu ya juu.

Sambamba na hilo kitaongeza rasilimali watu katika taasisi za elimu ya juu, ikijumuisha wahadhiri, wakutubi, wataalam wa maabara na karakana ili kukidhi mahitaji ya viwango na ubora wa elimu.

“Tutaboresha na kuongeza miundombinu na vifaa vya kujifunzia, kufundisha na kutafiti ili kuongeza uwezo wa Taifa wa kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi,” imeeleza CCM katika ilani yake ya uchaguzi ya 2020-2025. 


Soma zaidi:


Pia kinakusudia kuhuisha mitaala na kuanzisha programu kulingana na mahitaji ya kitaifa, kikanda na kimataifa ili wahitimu wawe na stadi stahiki za kumudu kufanya kazi mbalimbali za kuajiriwa na kujiajiri. 

CCM ambayo inawakilishwa na Rais John Magufuli katika nafasi ya urais imesema itaimarisha mafunzo ya lugha kwa kutoa programu maalum ya lugha ya Kiswahili na lugha nyingine za kigeni kwa ajili ya kuzalisha wataalam na wakalimani wa Kiswahili wenye viwango vya kimataifa.

“Tutaongeza udahili katika Elimu ya Juu kwa makundi yote yakiwemo wanafunzi kutoka nje ya nchi na kuimarisha mfumo wa malezi kwa wanafunzi vyuoni kwa kuwapa stadi za maisha na huduma za ushauri nasaha ili kupata wahitimu wenye maadili,” inaeleza ilani hiyo. 

Mgombea Mwenza wa Kiti cha Urais Tanzania kwa tiketi ya CCM Mama Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Wananchi wa Kijiji cha Somanga, Kilwa mkoani Lindi alipokuwa njiani kuelekea mkoani Mtwara kwa ajili ya mikutano ya kampeni jana Septemba 09, 2020. Picha|CCM


Chadema kitapunguza kiwango cha marejesho ya mkopo 

Katika kuwapatia ahueni wanafunzi wa vyuo vikuu, chama hicho katika ilani yake kimesema kitapunguza kiwango cha marejesho ya mikopo ya elimu ya juu hadi kufikia asilimia tatu ya mshahara wa mnufaika na kutanua wigo wa muda wa marejesho hadi kufikia miaka 25 tangu mnufaika apate ajira.

“Aidha, Serikali itafuta riba na tozo zote zitokanazo na adhabu ya kuchelewesha marejesho ya mkopo wa elimu ya juu,” inasomeka sehemu ya ilani ya Chadema ya 2020-2025.Kwa utaratibu wa sasa, kiwango cha marejesho ya mkopo wa elimu ya juu ni asilimia 15 ya mshahara wa mnufaika na anatakiwa kurejesha ndani ya miaka 10 tangu aanze kupata mkopo. 

Lengo kuu la kupunguza kiwango cha marejesho na kuongeza muda wa kulipa ni kuweka mazingira wezeshi ili kila mhusika alipe na usiwe mzigo wa kumfanya asiweze kuwekeza katika shughuli zingine za uzalishaji.

Pia wanafunzi wote wenye sifa za kujiunga na vyuo vya kati, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu, Chadema imesema watapewa mikopo bila ya ubaguzi wowote na serikali hiyo mpya itakapochaguliwa Oktoba 28. 

Pamoja na uchambuzi wa ilani za vyama hivyo vitatu ambavyo Nukta imefanikiwa kupata sera zake za uchaguzi, bado Watanzania hasa vijana wa elimu ya juu wenye sifa ya kupiga kura wana haki ya kuchagua chama chochote wanachoona kinawafaa. 

Sera za chama kitachochaguliwa, ndiyo zitatoa mstakabali wa elimu ya juu katika kipindi cha miaka mitano  ijayo.

Katika moja ya mikutano ya mgombea urais kwa tiketi ya Chdema, Tundu Lissu amesema "Tunahitaji Rais atakayetufariji. Na mimi naomba niseme hapa, mkikipa chama chetu dhamana ya kuongoza nchi hii,  mtakuwa mmepata mfariji mkuu". Picha| Chadema.

Related Post