Uchaguzi Mkuu 2020: Kodi yateka ajenda vyama vya siasa Tanzania

September 8, 2020 6:38 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Vyama vyaainisha mipango ya kuwatua wananchi mzigo wa kodi na kuboresha mazingira ya biashara.
  • Chadema kufumua mfumo wa kodi uliopo sasa.
  • ACT-Wazalendo yasema itaondoa mfumo unaomlazimisha mfanyabiashara kulipa kodi kabla hajaanza kufanya biashara.
  • CCM kutoa elimu zaidi ili wananchi walipe kodi stahiki. 

Dar es Salaam. Licha ya kuwa kodi na tozo mbalimbali zinazotozwa na Serikali zimekuwa sehemu muhimu ya kuongeza mapato kwa ajili ya kutoa huduma za jamii, bado zimekuwa ni changamoto kwa wafanyabiashara na wawekezaji kuendeleza biashara zao nchini Tanzania. 

Kwa nyakati tofauti Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wafanyabiashara ikiwemo kufuta, kupunguza na kutoa msamaha kwa baadhi ya kodi zisizo rafiki kwa ukuzaji biashara na kipato cha mwananchi mmoja mmoja.  

​Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango katika hotuba ya bajeti kuu ya Serikali 2020/21, alipendekeza kufuta au kupunguza ada na tozo sitini zinazotozwa na wizara, idara na taasisi zinazojitegemea ili kuondoa kero na urasimu kwa wafanyabiashara na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Pamoja na hatua za serikali zilizopita katika kufuta au kupunguza tozo na kodi, bado vyama vya siasa vinavyowania fursa ya kuchaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 vimeahidi kuendelea kuzipunguza au kufuta baadhi ili kutoa ahueni zaidi kwa wananchi na wafanyabiashara. 

Vyama hivyo kikiwemo chama tawala Chama cha Mapinduzi (CCM) vimeeleza katika ilani zao na baadhi ya mikutano ya kampeni namna vitakavyoboresha mazingira ya upatikanaji wa kodi usiowaumiza wananchi.

Katika ilani za vyama vya CCM, Chadema na ACT-Wazalendo za mwaka 2020-2025 ambazo Nukta Habari (www.nukta.co.tz) imezifanyia uchambuzi, vyama hivyo vimeainisha mikakati mbalimbali ya kuwatua wananchi mzigo wa kodi vikifanikiwa kushika dola. 

Kipindi hiki cha kampeni kinawapa fursa wananchi ambao ni wapiga kura kuchagua sera na kuwapima viongozi watakaosaidia uwepo wa kodi zinazoendana na mazingira ya biashara yanayowazunguka.

Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akizungumza wakati wa mkutano wa uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge wa ACT Wazalendo jimbo la Kilwa Kusini, Selemani Bungara (Bwege) jana September 7, 2020. Picha|ACT-Wazalendo. 

Ajenda ya ACT-Wazalendo kuhusu kodi

Chama hicho ambacho kimemteua aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje ya Tanzania, Bernard Membe kupeperusha bendera ya urais, ilani yake inaeleza kuwa kikishika dola baada ya Oktoba 28 kitaondoa mfumo unaomlazimisha mfanyabiashara kulipa kodi kabla hajaanza kufanya biashara.

Chama hicho kimeeleza kuwa kitapitia mifumo yote ya kodi na kuhakisha kunakuwa na kodi rafiki kwa wananchi.

“Kodi sahihi zinazotozwa kwa wakati sahihi ili kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiyari ni muhimu zaidi ili kuhakisha biashara zinakua na kuimarika na siyo kuwa na mfumo wa kodi ambao utapelekea (utasababisha) kufunga au kuua biashara,” inasomeka sehemu ya ilani ya chama hicho. 

Chama hicho kimesema kitaondoa kodi ya ardhi ya kijiji kwa sababu wananchi huitumia kwa ajili ya kujikimu na kujihifadhi ikilinganishwa na wawekezaji ambao hutumia ardhi kwa ajili ya kuzalisha faida au kulimbikiza mali.

“Itarekebisha sera za kodi ili kuirejesha katika hali yake ya kawaida sekta ya utalii pamoja na mnyororo wake ambayo imeathirika sana na janga la virusi vya Corona,” imeeleza ACT-Wazalendo katika ilani yake.

Chama hicho kinachoongozwa na Kiongozi Mkuu Zitto Kabwe kimeeleza kuwa pia kitaondoa kodi na kuwezesha upatikanaji bure wa bidhaa za hedhi katika shule za msingi na sekondari Tanzania.


Soma zaidi:


Chadema kubadilisha mfumo wa kodi

Chama hicho kikuu cha upinzani Tanzania kimesema katika ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020 – 2025 kuwa iwapo kitashika dola baada ya uchaguzi wa mwishoni mwa Oktoba kitautazama upya mfumo wa kodi (Tax regime) kwa maana ya kuangalia viwango vya kodi, uratibu wa kodi na mawanda mazima ya matokeo ya kodi kwa wananchi. 

Baadhi ya mambo ambayo chama hicho kitayafanyia kazi ni kuhakikisha kiwango cha kodi ya kampuni (Corperate Tax)  hakizidi asilimia  20 na kisiwe chini ya asilimia 15 ya faida ya mfanyabiashara au mwekezaji.

“Ukipunguza kiwango hiki unayaongezea makampuni na wawekezaji binafsi pamoja na wafanya biashara nafasi ya kukuza mitaji yao na kupanua uwekezaji wao nchini na hivyo kuajiri Watanzania wengi zaidi,” inaeleza ilani hiyo. 

Chadema imesema kodi ya ongezeko la thamani haitazidi asilimia 15 lakini isiyopungua asilimia 10 ikilinganishwa na sasa hivi ambapo ni asilimia 18 ili kuwapunguzia maumivu ya kodi wananchi.

“Serikali ya Chadema itaweka utaratibu wa kuwa na viwango vizuri vya kodi ya ardhi kwa  wananchi ili kuweza kupima ardhi na kuwa na hati ambazo wanaweza kuzitumia kuingia mikataba na asasi za fedha kwa ajili ya kupata mitaji ya kuwekeza kwenye miradi mbalimbali ya kilimo, mifugo, uvuvi na mazao ya misitu,” inaeleza Chadema katika ilani yake.

Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Tundu Lissu akinadi sera zake kwa wapiga kura wa Unguja visiwa Zanzibar jana September 87, 2020. Picha|Chadema. 

CCM kuondoa vikwazo vya kikodi

Chama hicho tawala ambacho kinawakilishwa na Rais John Magufuli katika nafasi ya urais katika ilani yake kimesema kitaboresha mifumo ya uendeshaji biashara katika mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo kwa kuondoa vikwazo vya kibiashara  vikiwemo kodi na tozo mbalimbali pamoja na utoaji vibali kwa wakati.

“Kupunguza idadi na viwango vya tozo, ada na kodi na kuweka mfumo imara wa ufuatiliaji na tathmini,” inaeleza ilani ya CCM.

CCM imejidhatiti kuendeleza ujenzi wa majengo yatakayotumika kama ofisi kwa taasisi za Serikali ili kuipunguzia gharama kubwa ya kodi ya pango katika soko na fedha zitumike katika shughuli za maendeleo.

Katika hatua nyingine, chama hicho kikipata ridhaa ya kuongoza baada ya Oktoba 28, kimesema kitawasimamia wananchi katika ulipaji kodi kwa usahihi, ukamilifu na kwa wakati ili kuharakisha maendeleo.

Licha ya vyama hivyo vitatu kueleza vitakavyoshughulika na suala la kodi baada ya kuchaguliwa, imekuwa ngumu kupata ilani za vyama vingine kueleza kwa undani kuhusu kodi. 

Sera zipi za kodi zimekuvutia kutoka vyama vya siasa vinashiriki Uchaguzi Mkuu? Unayo nafasi ya kufanya maamuzi Oktoba 28, 2020 katika sanduku la kura.

Mgombea Mwenza wa Kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan akisalimiana na kuzungumza na wanachama wa CCM na Wananchi wa kijiji cha Kibiti Mkoani Pwani kwenye mkutano wa Kampeni za CCM jana Septemba 07, 2020. Picha| CCM.

Enable Notifications OK No thanks