Mambo yatakayosaidia kupunguza uzalishaji gesijoto Tanzania

Daniel Samson 2351Hrs   Juni 28, 2022 Habari
  • Ina shabaha ya kupunguza uzalishaji kuanzia asilimia 30 hadi asilimia 35 itakapofika mwaka 2030.
  • Zinahitajika Dola za Marekani 19.2 bilioni (Sh44 trilioni) kufikia kiwango hicho.
  • Imebuni miradi ya kimkakati na inashirikia na washirika wa maendeleo kufikia shabaha hiyo.

Morogoro. Serikali ya Tanzania imeanza kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kubuni miradi itakayosaidia kufikia shabaha ya kupunguza uzalishaji gesijoto kutegemeana na uwezo kiuchumi kuanzia asilimia 30 hadi asilimia 35 itakapofika mwaka 2030.

Shabaha hiyo iko katika mchango wa kitaifa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi (Nationally Determined Contribution (NDC)) ambapo zinahitajika Dola za Marekani 19.2 bilioni (Sh44 trilioni) kufikia kiwango hicho.

NDC ni mwitikio wa kimataifa wa nchi wanachama wa mkataba wa umoja wa mataifa wa Mabadiliko ya tabianchi, kama ilivyofafanuliwa katika Kifungu cha 4 (2) cha Makubaliano ya Paris.

Kifungo hicho kinazitaka nchi mwanachama kuandaa na kuwasiliana mchango wake wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambao inakusudia kuifikia mwaka 2030.

Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Makamu wa Rais Catherine Bamwenzaki wakati akifungua warsha kwa waandishi wa Habari iliyolenga kujenga uwezo juu ya NDC hivi karibuni mkoani Morogoro amesema tayari Tanzania imeandaa, kukamilisha na kuwasilisha NDC kwa Umoja wa Mataifa.

“Malengo makuu ya kimataifa ya NDCs ni kuchangia katika kupunguza athari na kuimarisha ustahimilivu wa muda mrefu wa mabadiliko ya tabianchi; kuchangia katika juhudi za kupunguza uzalishaji wa gesi joto ili kufikia lengo kuu la mkataba (wa Paris) ambalo ni kupunguza uzalishaji wa gesi joto kwenye anga katika kiwango ambacho hakitaleta madhara kwenye mfumo wa hali ya hewa,” amesema Bamwenzaki.

NDC imeainisha hatua za kuchukuliwa kwenye eneo la kuhimili athari na pia kupunguza uzalishaji wa gesijoto ambapo imetaja sekta za kipaumbele zikiwemo sekta za kilimo, mifugo, misitu na wanyamapori.

“Maeneo mengine yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na nishati, mazingira ya bahari na ukanda wa pwani na uvuvi (bahari na maziwa), maji na usafi wa mazingira, utalii, makazi ya binadamu, afya, miundombinu, majanga na masuala mtambuka ikiwemo jinsia, tafiti, fedha na teknolojia,” amesisitiza Bamwenzaki.


Zinazohusiana:


Nini kinafanyika kupunguza gesijoto?

Katika kupunguza gesijoto sekta za kipaumbele ni pamoja na nishati, misitu, usafirishaji na taka. Sekta hizi ndiyo zinachangia kwa kiasi kikubwa katika uzalishaji wa gesijoto kwa sasa na zina fursa kubwa ya kuchochea na kuchangia maendeleo ya kiuchumi. 

Mtaalam huyo wa mazingira amesema hatua nyingine zilizochukuliwa ni pamoja na kuandaliwa kwa Mpango Kabambe wa Kimakakati, Maandalizi ya Mkakati wa Kitaifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, na Sera ya Mazingira ya 2021 iliyozinduliwa Februari, 2022. 

Tanzania ni mwanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) na ni miongoni mwa nchi zilizowasilisha NDC kwenye Sekretarieti ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi Julai 30 2021.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Tanzania inachangia asilimia 0.36 ya gesijoto yote inayozalishwa duniani, kiwango ambacho ni kidogo ikilinganishwa na mataifa yaliyoendelea kama Marekani na China.

Pia ni miongoni mwa nchi zilizoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame, mafuriko, maporomoko ya udongo, ongezeko la joto, kuibuka kwa mlipuko wa magonjwa ya mazao, mifugo na binadamu na uwepo wa viumbe vamizi.

Katika kukabiliana na athari hizo licha ya kuanda NDC, Serikali inatekeleza Mradi wa Kuhimili Mbadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo ya Ikolojia Vijijini (EBARR).

Mratibu wa mradi huo, Dk James Nyarobi amesema mradi huo ni wa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2018 hadi 2022 na umefadhiliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF) kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 7.7 sawa na Sh17.4 bilioni.


Tangazo:


Mradi huo unatekelezwa katika mikoa minne ya Tanzania Bara na mkoa mmoja wa Zanzibar: Simanjiro mkoani Manyara, Kishapu (Shinyanga), Mvomero (Morogoro), Mpwapwa (Dodoma) na Wilaya ya Kaskazini A mkoani Unguja.

Amesema katika mradi huo wanawawezesha wananchi vijijini  kupata maji, kutengeneza majiko banifu kupanda miti na kuhifadhi misitu na kuokoa maeneo yaliyoharibika na nyanda za malisho.

“Tunaimarisha upatikanaji wa taarifa na elimu kwa umma kuhusu mbinu bora za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia mifumo ya ikolojia,” amesema Dk Nyarobi.

Akizungumza katika warsha hiyo, Mtaalam wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Abbas Kitogo amesema wanashirikiana na Serikali ya Tanzania kufanikisha shabaha hiyo ya kupunguza uzalishaji wa gesijoto ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi. 

Amesema kwa sasa wanatekeleza miradi mbalimbali nchini ikiwemo kubuni na kutekeleza miradi ya nishati safi na salama ikiwemo matumizi ya majiko banifu na mkaa mbadala kwa kushirikisha makundi mbalimbali kwenye jamii.

Related Post