Mambo muhimu ya kuzingatia unapoandaa lishe ya watoto wadogo
- Ni pamoja na kuhakikisha ulaji wa makundi yote ya chakula.
- Usafi na uchanganyaji sahihi wa makundi ya chakula anachopewa mtoto.
- Wataalamu wa afya wasema kutozingatia mambo hayo kutazorotesha afya ya mtoto.
Dar es Salaam. Kupata mtoto ni moja kati ya ndoto ya familia nyingi duniani. Wakati mtoto anazaliwa huashiria kuanza kwa msimu mpya wa malezi kwa wazazi na jamii inayowazunguka.
Kwa baadhi ya wazazi wanaopata mtoto kwa mara ya kwanza huwa ni safari ya kujifunza zaidi, ikiwataka kuwa makini kwa kila uamuzi watakaouchukua ikiwemo uamuzi wa kuchagua lishe bora kwa ajili ya mtoto wao.
Uamuzi sahihi wa lishe bora ndiyo utakaoamua afya na ustawi wa mtoto huku ikimuhakikishia ukuaji bora mpaka anapokuwa mtu mzima.
Shirika la afya Duniani (WHO) linasema mtoto akifikia umri wa miezi sita mahitaji ya nishati na virutubisho huongezeka, kiasi ambacho maziwa ya mama hayawezi kutosheleza hivyo vyakula vya ziada huhitajika.
Kadiri mtoto anavyokua ulaini na uzito wa chakula ubadilishwe taratibu kwenda kwenye vyakula vilivyopondwa hadi kufikia vyakula vyenye vipande vya kutafuna na hatimaye kula chakula cha familia.Picha|Magreth Mhoha.
“Ikiwa mtoto hataanzishishiwa vyakula vya ziada akifikisha umri wa miezi sita au kama vitatolewa isivyofaa, ukuaji wa mtoto mchanga unaweza kudhoofika,” inasema WHO.
Mbali na kudhoofika, Dk Jeremia Masiaya kutoka kituo cha afya cha Chiodya mkoani Lindi anasema lishe duni ni chanzo cha magonjwa mengi kwa watoto ambayo hutokana na kudhoofika kwa kinga ya mwili.
“Ukosefu wa lishe utapelekea upungufu wa vitamini vinavyoimarisha ubongo unaohusika na kuchangia hatua ya mtoto kuongea,” amesema Dk Masiaya.
Huenda unajiuliza ni makundi gani ya chakula unayotakiwa kumpa mtoto wako baada ya kufikisha miezi sita, ondoa shaka upo mahali sahihi unapoweza kujifunza ili kuepuka madhara ya kiafya yanayoweza kumpata mtoto wako.
Soma zaidi
-
Vyakula vinavyoimarisha kumbukumbu, uelewa wa kimasomo kwa watoto
-
Zifahamu faida za kula wadudu lishe
Hakikisha lishe ina makundi yote ya chakula
Kwa mujibu wa mwongozo wa utoaji huduma ya lishe kwa watoto wadogo ulioandaliwa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), mtoto anatakiwa kupata makundi matano ya chakula kwenye mlo wake wa kila siku.
Makundi hayo ni vyakula vya nafaka, mizizi na ndizi vinavyohusisha mahindi, mchele, mtama, ulezi, ngano, uwele, viazi vikuu.
Kundi lingine ni vyakula vya jamii ya kunde na vyenye asili ya wanyama ikiwemo kunde, karanga, soya, nyama, samaki, dagaa, maziwa, na maayai.
Makundi mengine yanayoshauriwa ni pamoja na mbogamboga na matunda ambayo ni chanzo cha vitamini ikiwemo vitamin C.
Mtaalamu wa lishe kutoka TFNC, Dorice Kitana anasema kwa siku mtoto anatakiwa apate angalau aina moja ya chakula kutoka kwenye kila kundi, hii itamuweka kwenye nafasi nzuri ya kupata virutubisho vyote vinavyotakiwa ili kuimarisha afya yake.
Uchanganyaji sahihi wa makundi ya chakula
Mtaalamu huyo wa lishe anasema mara nyingi wazazi huchanganya nafaka za aina moja kwenye lishe mfano, mahindi, mchele, uwele bila kujua kuwa zina aina moja tu ya kirutubisho ambayo ni wanga na kusahahu makundi mengine.
Mbali na hilo baadhi ya wazazi wanachanganya nafaka isivyotakiwa jambo linalochangia kula chakula kilichopikwa sana au kibichi jambo linaloweza kutengeneza sumu mwilini.
Mathalan, uchanganyaji wa nafaka na karanga, mtaalamu huyo anasema karanga ni nzuri lakini ina kiwango kikubwa cha sumu kuvu ambayo ni chanzo cha udumavu na saratani.
“Ikiwa mzazi anataka kuchanganya nafaka asichanganye zaidi ya nafaka mbili, na nyingine azisage pembeni na azichanganye wakati wa kupika,” amesema mtaalam huyo.
Mlo wa mtoto unatakiwa uwe na aina mbili au zaidi za makundi ya chakula ili kurahisisha ukuaji bora wa afya ya akili na mwili.Picha|Prillens roducts\Facebook.
Hakikisha unampa mtoto kiwango sahihi
Mwongozo wa TFNC unasema mtoto mwenye umri wa miezi sita anatakiwa kupewa vijiko viwili mpaka vitatu vya chakula mara mbili kwa siku,mtoto wa miezi saba na nane yeye anatakiwa kupewa milo mitatu ikiambatana na nusu kikombe cha uji wa lishe kwenye kila mlo.
Mtoto mwenye umri wa miezi 9 mpaka mwaka mmoja anatakiwa kupewa milo mitatu itakayohusisha kikombe kimoja cha lishe.
Hakikisha usafi wakati wa kuandaa lishe
Jambo la kwanza na la msingi wakati wa kuandaa lishe ni usafi ambao unahusisha mazingira yanayotumika kuandaa chakula cha mtoto, vyombo vinavyotumika pamoja na muandaaji.
Mtaalamu wa lishe Kitana anasema ikiwa lishe itakuwa sahihi na mazingira ya uandaaji, vyombo au mpishi hajazingatia usafi ni rahisi kwa vimelea vya magonjwa kuingia na kushambulia afya ya mtoto.