Magufuli, dunia wazungumzia kifo cha Rais mstaafu Mkapa

Rodgers George 0313Hrs   Julai 24, 2020 Maoni & Uchambuzi
  • Watanzania wamesema kifo chake ni pigo kubwa kwa Taifa.
  • Viongozi wa kimataifa wamesema mchango wake kwenye upatanisho na diplomasia hauwezi kusahaulika.
  • Amefariki dunia leo Ijumaa Julai 24, 2020 jijini Dar es Salaam. 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli, Watanzania na viongozi mbalimbali duniani wamesema watamkumbuka Rais mstaafu wa awamu ya tatu wa Tanzania Benjamin Mkapa kwa mchango wake katika kuimarisha uchumi wa nchi na diplomasi ya kimataifa. 

Mkapa amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Ijumaa Julai 24, 2020 jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa hospitalini, kwa mujibu wa Rais John Magufuli aliyetangaza kupitia televisheni ya Taifa (TBC).

Mkapa aliyefariki akiwa na miaka 81 alikuwa Rais wa Tanzania kati ya mwaka 1995 na 2005 kabla ya kukabidhi madaraka kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Dk Magufuli amesema mzee Mkapa atakumbukwa kwa uchapakazi na mapenzi yake makubwa kwa Taifa pamoja na utendaji wake katika kujenga uchumi wa Tanzania.

“Nimesikitishwa na kifo cha Mzee wetu Benjamin Mkapa. Nitamkumbuka kwa mapenzi yake makubwa kwa Taifa, ucha Mungu, uchapakazi na utendaji wake katika kujenga uchumi. 

“Hakika Taifa limepoteza nguzo imara. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina,” amesema Dk Magufuli kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Kufuatia msiba huo, Rais Magufuli ametangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa ambapo bendera zote zitapepea nusu mlingoti. 

Watanzania wakiwemo viongozi wa Serikali, wanasiasa, wafanyabiashara wameungana na Rais Magufuli kuomboleza msiba huo huku wengi wakimuelezea kuwa alikuwa mzalendo na mchapakazi aliyependa maendeleo ya Tanzania. 

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kifo cha Mzee Mkapa ni pigo kwa Taifa na atakumbukwa kwa mchango wake katika shughuli za maendeleo ikiwemo kuimarisha diplomasia ya Tanzania kimataifa. 


 

Kiongozi Mkuu Chama Cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe katika ukurasa wake wa Twitter amesema amepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Mkapa na ni hasara kwa Watanzania kwa sababu alikuwa chachu ya maendeleo. 

Mbunge aliyemaliza muda wake katika Jimbo la Mtama Mkoani Lindi Nape Nnauye amesema atamkumbuka Rais mstaafu Mkapa kwa kuwa alikuwa mlezi mzuri wakati wa uongozi wake hasa kwa vijana kama yeye. 

“Nakumbuka sana upendo, malezi na busara zako nikiwa Mkuu wa Wilaya Masasi (mkoani Mtwara)! Aaah, mwamba mwenye sifa halisi za kusini, what a loss (Ni hasara)!! Pumzika baba!.” ameandika Nape katika ukurasa wake wa Twitter. 


Viongozi wa Serikali nao wamzungumzia

“Binafsi nimejifunza mengi kupitia uongozi wa Mzee Mkapa na maisha yake kwa ujumla, Tunashukuru kwa kutuacha na kitabu cha maisha yako kitakachobaki kama kumbukumbu na sehemu ya sisi kujifunza na vizazi vijavyo,” ameandika Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo @jokateM katika ukurasa wake wa Twitter.

Mzee Mkapa kabla ya umauti kumfika alikuwa tayari ameandika kitabu chake cha “My Life, My Purpose” ambacho ameeleza mambo mbalimbali anayoyakumbuka wakati wa uongozi wake na Tanzania. 

“Pumzika kwa Amani CMR Benjamin Mkapa , umeondoka lakini bado unaishi katika mioyo yetu,” ameandika Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe katika ukurasa wake wa Twitter. 

Naye Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamisi Kigwangalla ametuma salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa kuondokewa na mtu muhimu Tanzania. 

Hata wakati wanasiasa wakiomboleza kifo cha kiongozi huyo, wafanyabiashara mashughuli nchini pia wameungana katika msiba huo wa kitaifa. 

Mkurugenzi Mtendaji kampuni ya MeTL Group, Mohammed Dewji naye amesema bado ni ngumu kukubali kwamba Mzee Mkapa hatunaye tena.

“Bado ni ngumu kukubali kwamba Mzee Mkapa hatunaye tena. Tangulia Baba, nasi tunakuja,” ameandika mfanyabiashara huyo katika ukurasa wake wa Twitter.

Akiwa Waziri wa Mambo ya Nje mwaka 1977 na 1980, Mzee Mkapa alikuwa ni shujaa wa kuhamasisha Umoja wa Mataifa (UN) huku akipinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini. Picha| Wikipedia.

Viongozi wa Afrika wazungumzia kifo cha Mkapa

Aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga amesema nchi hiyo inatunza kumbukumbu muhimu za upatanishi uliofanywa na Mzee Mkapa akishirikiana na watu mashughuli wakiwemo Mwana diplomasia Dk  Koffi Annan na mpiganaji wa haki za wanawake na watoto Graca Machel walioisaidia Kenya kurudi katika amani baada ya machafuko yaliyotokana na uchaguzi mwaka 2007.

“Mkapa aliamini katika Ushirikiano wa kikanda na ni shujaa wa kuiinua Jumuiya ya Afrika Mashariki. Afrika imepoteza mtu muhimu,” ameandika Odinga kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Naye mwanamuziki na Mbunge wa Jimbo la Starehe nchini Kenya, Charles Njagua Kanyi (Jaguar) amesema wananchi wa Kenya watamkumbuka Mkapa kama shujaa wa amani.

“Alisimama na sisi katika kipindi chetu cha giza nene,” ameandika Jaguar kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Mwanahistoria wa Marekani Derek Peterson aliyejikita kwenye historia ya Afrika Mashariki wameungana na Watanzania kukumbuka mema yaliyofanywa na Mzee Mkapa.

Peterson amesema akiwa Waziri wa Mambo ya Nje mwaka 1977 na 1980, Mzee Mkapa alikuwa ni shujaa wa kuhamasisha Umoja wa Mataifa (UN) huku akipinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.


Zinazohusiana


Wananchi wakumbuka daraja la Mkapa

“Kipindi yupo madarakani namkumbuka zaidi kwa ujenzi wa Daraja la Mkapa ilikuwa shida sana kuvuka pake kuelekea mikoa ya Lindi na Mtwara. Kama kijana nakumbuka zaidi alivyotujengea uwanja wa Taifa wa kisasa kabisa,” amesema Maulid Magaya, mkazi wa jijini Dar es Salaam wakati akiongea na Nukta.

Tofauti na siku nyingine hali ya jiji la Dar es Salaam ni tulivu huku sehemu kubwa za kelele za muziki zimezoeleka kusikika maeneo ya stendi na maduka makubwa zikiwa hakuna.

“Hali ya jiji leo imepoa sana kuliko siku nyingine kwa sababu kila mtu yupo kwenye masikitiko. Tumezoea kuona hapa bajaji chache zikiwa zimepaki sababu nyingi zinakuwa kwenye shughuli lakini leo unatuona wote tumekaa hapa tunajadili kuhusu kifo cha Mkapa,” amesema Salim Abdul dereva wa Bajaji kituo cha Victoria jijini hapa. 


Taasisi na mashirika

Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania nao unaungana na Watanzania katika kuomboleza kifo cha Rais mstaafu #Benjamin William Mkapa na umeeleza kuwa akiwa Rais alifanya kazi bila kuchoka kuleta amani na ustawi, siyo tu kwa Tanzania bali kwa kanda yote. 

“Mchango wake hautasahaulika,” amesema ubalozi huo katika taarifa yake iliyotolewa leo. 

Nayo taasisi ya Uongozi imesema mzee Mkapa alikuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza programu za taasisi hiyo ambapo alifanya uhamasishaji wa kutafuta suluhu ya matatizo ya Afrika bila kuchoka. 

Mzee Mkapa alizaliwa Novemba 12, 1938. 

Related Post