Rais mstaafu Benjamin Mkapa afariki dunia, Tanzania ikitangaza siku saba za maombolezo

Mwandishi Wetu 2330Hrs   Julai 23, 2020 Habari
  • Amefariki dunia leo Jijini Dar es Salaam akiwa na umri wa miaka 81. 
  • Rais John Magufuli ametangaza kifo hicho usiku wa kuamkia leo Ijumaa Julai 24, 2020.
  • Pai ametangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa kuanzia leo Ijumaa Julai 24, 2020. 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa kuanzia leo Ijumaa Julai 24, 2020 kufuatia kifo cha Rais mstaafu wa wamu ya tatu, Benjamin William Mkapa kilichotokea Jijini Dar es Salaam.

Rais John Magufuli ametangaza kifo hicho usiku wa kuamkia leo kupitia televisheni ya Taifa (TBC) kuwa marehemu Mkapa amefariki dunia katika hospitali moja jijini humo. 

''Mzee Benjamin William Mkapa Rais wa awamu ya tatu amefariki. Amefariki kwenye hospitali jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa. Niwaombe Watanzania tulipokee hili. Taifa limepata msiba mkubwa. 

“Tuendelee kumuombea Mzee wetu Rais Benjamin William Mkapa ambaye ametangulia mbele ya haki," amesema Rais Magufuli.

                     

Aidha, Rais John Magufuli ametangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa kuanzia leo Ijumaa Julai 24, 2020 kufuatia kifo cha Rais mstaafu Mkapa huku akiwataka Watanzania kuwa watulivu, wastahimilivu na wamoja katika kipindi hiki kigumu cha majonzi. 

“Katika kipindi chote cha maombolezo, bendera zote zitapepea nusu mlingoti,” imeeleza taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu na kueleza kuwa taarifa zingine kuhusu msiba huo wa kitaifa zitatolewa baadaye.

Rais Magufuli amesema amesikitishwa na kifo cha rais Mkapa na Taifa limempoteza mtu imara aliyekuwa na mapenzi na nchi yake.

Mkapa alikuwa Rais wa Tanzania kati ya mwaka 1995 na 2005 kabla ya kukabidhi madaraka kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Alizaliwa Novemba 12, 1938.

Related Post