Maboresho: Kupitia Twitter utatazama video mubashara

September 15, 2018 5:29 pm · Zahara
Share
Tweet
Copy Link
  • Maboresho hayo kuwafaidisha zaidi wanasiasa na wanamuziki kuliko watu wenye wafuasi wachache.
  • Itafungua milango kwa kampuni na wafanyabiashara kutangaza bidhaa na huduma wanazotoa.
  • Hatua hiyo inatajwa kama mkakati wa Twitter kuwa karibu na wateja wake, kuimarisha ushindani wa teknolojia duniani.

Dar es Salaam. Kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii kama Facebook na Instagram wanafahamu huduma ya kurusha vitu mubashara, huku Instagram unaletewa ujumbe mtu akiwa mubashara lakini kwa watumiaji wa Twitter unaweza ukapitwa na video inayorushwa mubashara kwa sababu tu hukupata taarifa.

Basi tatizo hilo linaelekea kuwa historia kwasababu mtandao wa Twitter umefanya maboresho ili kumrahisishia mtu kuona video mubashara za watu au makampuni aliyoyafuata katika mtandao huo.  

Swali la kujiuliza, utajuaje kama mtu uliyemfuata yupo mubashara? Ni kwamba katika ukurasa wako upande wa juu utakuonyesha uliyemfuta kama yupo mubashara bila kutafuta au yeye kukuambia.

Hii ni fursa kwa vyombo vya habari, taasisi,wasanii hata wanasiasa kuitumia katika kuhakikisha wanawafikia wafuasi wao kwa wakati, kujitangaza na kuonyesha bidhaa na huduma wanazotoa ikizingatiwa kuwa vdeo hizo zitaonekana katika ukurasa wa mbele pindi mtu anapofungua mtandao huo.  


Zinazohusiana:


Hata hivyo, ili kuona video hizo unapaswa kuwafuata wale ambao unahitaji kujua mambo yao na kwa upande wako unatakiwa kufanya jitihada kuongeza wafuasi ili video yako isambae haraka. Pia wapenzi wa kufuatilia video mbalimbali za michezo zinazoendelea duniani watapata urahisi zaidi wa kuburudika. 

Wadau wa mtandao wanaona hii ni fursa ya kujitangaza lakini uamuzi wa kutumia fursa hiyo unabaki kwa mtumiaji kuchagua kile anachokipenda kwasababu kila siku video nyingi zinatengenezwa.  

“Hii ni nzuri kwani huwezi kupitwa na baadhi ya matukio muhimu katika mtandao,” amesema Zainab Abdalla, mtumiaji wa Twitter na Mjasiriamali kutoka Bagamoyo huku akionyesha wasiwasi kwa wale ambao watakuwa na wafuasi wachache kama watanufaika kwa kupata watazamaji.

“Kwa wenye wafuasi wachache wanaweza wasifaidike sana ila kama wanasiasa na wasanii ni fursa kwao,”amesema Abdalla.

Jinsi ukurasa wako wa Twitter utakavyokuwa pindi mtu unayemfuata atakapokuwa mubashara.Picha| Twitter.

Enable Notifications OK No thanks