Lugola ataja bodaboda wanaopaswa kupelekwa polisi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema kundi la pili ni bodaboda ambayo inahusika na kesi ambapo kesi yenyewe kama bodaboda hiyo imehusika kwenye ajali ya barabarani au bodaboda kama kielelezo cha kesi husika. Picha|Mtandao.
- Amesema ni wale wanahusika na uhalifu, kesi za ajali barabarani na zisizo na wamiliki.
- Awaonya polisi wanaochomoa vifaa vya bodaboda wanazozikamata.
- Amesema kwa sasa bodaboda wanakula raha na ‘kujinafasi’
Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ametaja makundi matatu ya pikipiki maarufu kama bodaboda zinazopaswa kukamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi ikiwemo zile zinazohusika na uhalifu na kesi za ajali barabarani.
Amesema kinyume na hapo, bodaboda inapaswa kuandikiwa faini ya kosa ililotenda.
Lugola aliyekuwa akitoa ufafanuzi bungeni leo (Mei 20, 2019), amesema bodaboda ni sehemu ya mikakati ya Serikali kupunguza umasikini kwa vijana na tayari alishatoa utaratibu wa makundi ya bodaboda zinazotakiwa kukamatwa na kupelekwa kituo cha polisi ili kuepusha usumbufu usio wa lazima.
Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Mwibara alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Tabora, Rehema Migilla ambaye alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuwarudishia pikipiki zao madereva wa bodaboda ambazo kuendelea kukaa katika vituo vya polisi kwa muda mrefu zinaharibika na baadhi ya vifaa vinaibiwa.
“Kundi la kwanza ni bodaboda ambayo imehusika kwenye uhalifu, bodaboda zinatumika kufanya uhalifu hiyo ikikamwatwa itapelekwa kituoni,” amesema Lugola huku akishangiliwa na wabunge.
Amesema kundi la pili ni bodaboda ambayo inahusika na kesi ambapo kesi yenyewe kama bodaboda hiyo imehusika kwenye ajali ya barabarani au bodaboda kama kielelezo cha kesi husika.
Kundi la tatu na la mwisho ni bodaboda ambayo haina mwenyewe, Lugola amesema,”sisi tunaita “unfound and unclaimed property”, polisi kwa sababu wanalinda mali za raia wataichukua ikae kituo cha polisi ikipata mwenyewe ichukuliwe.”
Ameweka wazi kuwa bodaboda nyingine zozote ambazo haziko kwenye makundi hayo matatu hazitakiwi kukamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi lakini wanatakiwa kupewa siku saba kulipa faini ya kosa walilotenda.
Zinazohusiana:
- Serikali yaangazia daladala, mabasi ya mikoani kuongeza mapato
- Usafiri, biashara kuwa sehemu ya mwelekeo wa halai ya hewa Dar
Kauli hiyo ya Lugola ni ahueni kwa waendesha bodaboda wengi nchini ambao vyombo vya moto vimekuwa vikikamatwa na kuwekwa vituo vya polisi hata makosa yanayohusu faini.
Hata hivyo, katika swali lake Migilla aliibua suala la baadhi ya vifaa kama betri na taa kuchomolewa wakati bodaboda zilizokatwa zikiwa katika vituo vya polisi.
Akijibu swali hilo, Waziri Lugola amesema tayari alitoa utaratibu kwa askari polisi kutoa hati kwa bodaboda zilizokamatwa ili kuepusha matatizo wakati wa kuzirudisha kwa wamiliki.
“Nimeelekeza kwamba bobadaboda ambazo ziko kwenye makundi matatu zitapaswa kupelekwa kwenye kituo cha polisi na zenyewe wataandikiwa hati itakayoonyesha vitu ambavyo viko kwenye bodaboda ile ili atakapokuja huyu mtu across check (athibitishe) na hati aliyopewa ili yule aliyechukua aweze kushughulikiwa,” amesema Lugola.
Amewatoa hofu wabunge juu ya usafiri huo huku akisema sasa hivi bodaboda nchi nzima wanakula raha mstarehe na ‘wanajinafasi’.
Sheria ya Usalama Barabarani sura ya 128 ya mwaka 2002, inampa polisi mamlaka ya kusimamisha chombo chochote barabarani na kukikagua kubaini kama kina makosa hatimaye kukizuia na kukikamata.