Kutana na Helena Mzena: Bosi mpya wa Jubilee Insurance Tanzania

May 4, 2021 9:35 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  •   Anakuwa miongoni mwa wanawake wachache vigogo katika sekta ya bima nchini.

Dar es Salaam. Helena Mzena, mmoja wa wanawake mashuhuri wa masuala ya kifedha nchini Tanzania, ameingia kwenye orodha vigogo wanaongoza taasisi za fedha na bima baada ya kuteuliwa kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya huduma za bima ya Jubilee Insurance.

Katika taarifa kwa umma iliyochapishwa Mei 3 mwaka huu katika akaunti ya Linkedin ya Jubilee Insurance Tanzania, Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni ya Jubilee Life Insurance Corporation Shabir Abji, amesema Mzena amekuwa ni kinara katika masuala ya uongozi, mikakati na uendelezaji wa biashara, fedha na bajeti, usimamizi wa kukabiliana na vihatarishi (Risk Management) na kuimarisha misingi imara ndani ya kampuni hiyo.

Kabla ya uteuzi huo, Mzena alikuwa Ofisa Mkuu wa fedha katika taasisi hiyo kwa zaidi ya miaka mitatu na tangu ajiunge na kampuni hiyo ameshika nyazifa mbalimbali za kiuongozi.

Abji amesema mama huyo ana Shahada ya Uzamili ya masuala ya fedha na menejimenti kutoka Chuo Kikuu cha Liverpool John Moores nchini Uingereza. Pia, ana Shahada ya kwanza ya Fedha na mifumo ya tehama ya kifedha (Finance and financial information systems) kutoka Chuo cha Greenwich huko huko Uingereza.


Zinazohusiana:


Mzena anashika wadhifa huo baada ya kukaa kwa zaidi ya miaka 10 katika kampuni hiyo yenye makao yake makuu katika Mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam. 

Kwa mujibu wa Abji, Mzena alijiunga Jubilee Insurance mwaka 2011 na ana uzoefu wa miaka 10 katika masuala ya bima.

Kwa miaka mingi sekta za fedha na bima nchini Tanzania imekuwa ikiongozwa na wanaume kiasi cha baadhi ya wadau kuchagiza mabadiliko kwa kutoa fursa kwa wanawake kwa kuwa nao wana uwezo wa kushika usukani katika kampuni na mashirika hayo.

Enable Notifications OK No thanks