Kisiwa cha Mafia: Pepo kwa ajili ya wapendanao

February 13, 2020 8:44 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kisiwa chenye ukubwa wa kilometa za mraba 822.
  • Kuogelea na nyangumi pamoja na kushuhudia makundi ya kobe wa baharini ni kati ya vivutio utakavyokutana navyo.
  • Utafika Kisiwani huko kwa usafiri wa ndege au boti  kupitia Bandari ya Kilindoni.

Dar es Salaam. Kuna upekee fulani endapo sikukuu yako ya wapendanao yaani Valentine Day ukiifanya nje ya Februari 14.

Mbali na kwamba umpendaye atahisi kupendwa nje ya mipaka, uwezekano wa wewe na mwenzio kufurahia muda wenu kwa pamoja ni mkubwa kwa kuwa mtapata mambo mengi ya kustajabu kwa pamoja.

Zipo njia nyingi ambazo unaweza kuzifurahia katika msimu huu wa wapendanao ikiwemo kutembelea sehemu mbalimbali za kitalii ikiwemo visiwa vinavyoifanya nchi ya Tanzania kuwa pepo ifaayo kwa ajili ya watu wenye nia ya kuimarisha na kuendelea mahaba yao.

Kati ya visiwa hivyo ni kisiwa cha Mafia ambacho ni moja ya hifadhi kubwa za baharini ambacho kinapatikana katika bahari ya Hindi nje kidogo ya mkoa wa Pwani.  

Kwa mujibu wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania, kisiwa hicho kina ukubwa wa kilometa za mraba 822 ndani ya bahari ya Hindi inayochukua asilimia 20 ya uso wa dunia.

Papa aiana ya “Whale shark” huogelea karibu na watalii bila wasiwasi. Picha| Taasisi ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania.

Utakayokutana nayo katika kisiwa hicho

Kama hujawahi kumuona farasi wa baharini (sea horse) ambaye kwa mujibu wa chaneli ya “National Geographic” anaogelea wima wima na mwenye maajabu yake mengi, basi hii ndiyo fursa yako.

Maajabu hayo yakiwemo samaki huyo wa kiume kubeba ujauzito na kuzaa watoto badala ya samaki huyo wa kike utayaona kwenye Kisiwa cha Mafia ambacho kitakutambulisha wewe na umpendaye kwa viumbe wengine wengi wa kuvutia.


Zinazohusiana


Kupitia shughuli za kupiga mbizi na kuogelea kwenye mchanga safi wa kisiwa hiki, utafurahia vivutio vingi vinavyopatikana msimu hadi msimu.

Msimu wa Juni hadi Agosti utakusogeza karibu na kobe wa baharini ambao huogelea kwa makundi makundi huku msimu wa Julai hadi Agosti ukikupatia muda wa kufurahia nyangumi aina ya “humpback”.

Endapo utapenda kutembelea kisiwa hiki kuanzia mwezi Oktoba hadi Februari utafurahia kumtazama samaki mkubwa zaidi duniani “whale shark” ambaye watalii wengi huogelea karibu naye bila wasiwasi. Bado hauna sehemu ya kwenda katika msimu wa sikukuu?

Ni mahala penye maisha ya viumbe bahari wakiwemo samaki aina 400 ambao wamegunduliwa hadi sasa.

Zaidi, kisiwa hiki kitawarudisha wewe na mwenzi wako miaka 600 kabla ya kuzaliwa kwa Kristo (BC) huku kikisheheni hadithi nyingi za kale zikiwemo za karne ya 19.

Pia utafahamishwa juu ya magofu ya karne ya 13 na mabaki ya sanaa za mikono zilizotumiwa na watu wa zamani.

Unafikaje Mafia?

Kama wewe na umpendaye mpo katika Jiji la Dar es Salaam, unaweza kufika katika kisiwa hicho kwa dakika 30 kwa usafiri wa ndege.  Pia, usafiri wa boti au feri unatoka mikoa iliyopakana na bahari hadi katika Bandari ya Kilindoni iliyopo Mafia.

Usafiri huo unapatikana kuanzia saa 12 asubuhi huku ukitumia saa tano kufika katika kisiwa hicho kwa gharama ya Sh16,000.

Siyo tu utashuhudia vivutio mbalimbali, bali utapa muda mzuri wa kupumzika katika hoteli nzuri za kitalii kulingana na unene wa mfuko wako. Baadhi ya hoteli hizo ni Polepole, Chole na Shamba kilole.

Enable Notifications OK No thanks