Kidato cha sita Tanzania kujiandaa mitihani kwa siku 28
- Muda huo ni mfupi kuliko ule uliosalia kabla ya shule hazijafungwa kutokana na COVID-19.
- Prof Ndalichako ataka matokeo yatoke kabla ya Agosti 31
Dar es Salaam. Ni rasmi sasa kuwa wanafunzi wa kidato cha sita watakuwa na siku 28 tu za kujiandaa na mitihani ya Taifa baada ya Serikali kueleza kuwa mitahani ya kuhitimu kiwango hicho cha elimu itaanza rasmi Juni 29.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako amewaambia wanahabari Ijumaa (Mei 22, 2020) jijini Dodoma kuwa baada ya shule zenye kidato cha sita kufungua Juni mosi wanafunzi watakuwa na muda wa kusoma na kujiandaa na mitihani hadi Juni 28.
“Mitihani ya kidato cha sita itaanza rasmi tarehe 29 Juni 2020 na itafanyika hadi 16 Julai 2020. Mitihani hii ya kidato cha sita itaenda sambamba na mitihani ya ualimu,” amesema.
Kwa ratiba hiyo mpya, wanafunzi hao watakuwa na muda mchache wa kujiandaa wa takriban mwezi mmoja tu ikilinganishwa na mwezi mmoja na nusu uliokuwa umesalia kabla ya kufunga shule katikati mwa Machi kutokana na kuingia kwa ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) nchini.
Kabla ya shule kufungwa Machi 17, Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) lilikuwa limepanga mitihani ya kidato cha sita ianze kufanyika Mei 4 ikiwa ni mwezi mmoja na nusu wa maandalizi.
Zinazohusiana:
- Shule 24 vigogo ‘zilizoteka’ kidato cha nne
- Mbinu zinazoweza kuisaidia Temeke kutokomeza sifuri elimu ya sekondari.
- Udanganyifu mitihani darasa la saba kujirudia tena mwaka huu?
Katika hotuba yake ya Mei 21, Rais John Magufuli aliagiza kidato cha sita warudi masomoni Juni mosi na kutaka uandaliwe mpango maalumu (crush program) utakaowasaidia wanafunzi hao kujifunza ndani ya muda huo ili waweze kujiunga na elimu ya juu.
Prof Ndalichako amesema shule za bweni zinaweza kuanza kuchukua wanafunzi kuanzia Mei 30 na shule zile za kutwa zifanye maandalizi ili inapofika Juni mosi waanze masomo kama ilivyoelekezwa na Rais John Magufuli.
Kutokana na hatua hiyo, Prof Ndalichako ameiagiza NECTA kuhakikisha inasambaza mara moja ratiba ya mitihani hiyo.
Mitihani ya kidato cha sita ni ngazi muhimu kwa wanafunzi kujiunga na elimu ya juu Tanzania kuanzia ngazi za stahashada na shahada.
“Tumeliagiza baraza la mitihani la Taifa kuhakikisha kwamba matokeo ya kidato cha sita yatoke kabla ya Agosti 31 2020,” amesema waziri huyo akieleza kuwa hatua hiyo ni kuhakisha wanaendana na maelekezo ya Rais Magufuli kuwa wanafunzi hao wanaenda vyuo vikuu kwa kufuata utaratibu wa kawaida wa mihula.