Ilboru ilivyoingia kwa kishindo 10 bora matokeo kidato cha nne

January 16, 2021 8:08 am · Daniel
Share
Tweet
Copy Link
  • Imeingia kwenye orodha ya shule 10 bora kitaifa baada ya miaka 19.
  • Wanafunzi wake 118 kati 119 wamefanikiwa kupata daraja la kwanza.
  • Wanafunzi 51 kati ya 118 wamefanikiwa kupata daraja la kwanza la alama saba ikiwa ni ufaulu juu kabisa.
  • Nidhamu, kusoma kwa bidii kwawabeba watahiniwa wa shule hiyo.

Dar es Salaam. Unaweza kusema ni ndoto baada ya Shule ya Sekondari ya Ilboru ya mkoani Arusha kufanikiwa kuingia katika orodha ya shule 10 bora kitaifa katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika Novemba mwaka jana.

Ni ndoto kwa sababu kwa muda wa miaka 19 iliyopita, shule hiyo ya vipaji maalum haijawahi kuingia katika orodha hiyo ya dhahabu ya elimu Tanzania.

Katika matokeo yaliyotangazwa na Baraza la Mtihani la Tanzania (Necta) Januari 15, 2021, shule hiyo imefanikiwa kushika nafasi ya pili kitaifa nyuma ya shule ya Wasichana ya St Francis ya jijini Mbeya.

Shule hiyo ya wavulana imepanda kutoka nafasi ya 36 iliyoshikilia katika matokeo ya mtihani uliofanyika mwaka 2019.

Ilboru ambayo ni miongoni mwa shule kongwe za sekondari zinazomilikiwa na Serikali, katika orodha hiyo imeungana na shule za Cannosa (Dar es Salaam), Kemebos (Kagera) na  Feza Boys ya jijini Dar es Salaam.

Nyingine ni Ahmes, St Aloysius Girls, Marian Boys (Pwani) na St. Augustine Tagaste ya jijini Dar es Salaam.

Mara ya mwisho Ilboru kuingia kwenye 10 bora kitaifa ilikuwa mwaka 2001 ambapo ilishika nafasi ya tatu kitaifa, jambo linalodhihirisha kuwa shule hiyo imefanya kazi kubwa mpaka kurudi tena kwenye orodha hiyo ambayo kila shule inatamani kuingia.

Kwa mpangilio huo wa ufaulu wa kidato cha nne mwaka jana, Ilboru ndiyo shule pekee ya Serikali iliyofanikiwa kupenya katika 10 bora kitaifa huku zilizobakiwa zikiwa za binafsi.

Ufaulu wa matokeo ya mwaka 2020

Kilichoifanya shule hiyo kupata mafanikio hayo ni matokeo ya watahiniwa wake waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana ambapo wamefanya vizuri kwa kupata ufaulu kati ya daraja la I hadi II huku kukiwa hakuna mtahiniwa aliyepata daraja la III, IV wala 0.

Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyotangazwa na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde, kati ya wanafunzi 119 wa Ilboru waliofanya mtihani huo mwaka jana, 118 wamepata daraja la I huku mmoja akipata daraja II.

Jambo jingine la kipekee katika matokeo hayo, ni kuwa wanafunzi 51 kati ya 119 waliofanya mtihani mwaka jana katika shule hiyo wamepata daraja la kwanza la pointi saba ambalo ni daraja la juu kabisa katika ngazi za ufaulu, kwa mujibu wa Necta.

Ufaulu huo umevunja rekodi kwa sababu miaka ya hivi karibuni, shule hiyo haikuwahi kupata matokeo mazuri kama hayo.

Mathalan, katika mwaka 2015 na 2019 katika matokeo ya kidato cha nne, watahiniwa wa shule hiyo waliopata daraja la kwanza la pointi saba walikuwa 33 tu.


Zinazohusiana


Nini kimeifikisha hapo Ilboru?

Safari ya kutokana nafasi ya 36 kitaifa hadi nafasi ya pili ilikuwa siyo rahisi kwa shule hiyo ambayo haijahi kuingia 10 bora kwa miaka 19.

Mkuu wa shule hiyo, Denis Otieno ambaye amesema zimefanyika jitihada mbalimbali ikiwemo kuanzisha mifumo mipya kwa wanafunzi inayowawezesha kujisomea vizuri na kuwa tayari kwa mitihani ya kitaifa.

“Kupata matokeo mazuri ni mchakato. Tulianza kwa kuwapatia msingi bora kuanzia walipokua kidato cha kwanza, pili na hadi cha tatu. Pia tulipigana kuhakikisha tunamaliza mtaala mapema ili kuwapatia wanafunzi nafasi ya kujiandaa,”amesema Otieno.

Pia mafanikio hayo yamechangiwa na shule hiyo kuweka utaratibu kwa wanafunzi hao ambao wote wanakaa shuleni kufanya majaribio na mitihani ya mara kwa mara ili kujipima uwezo wao wa kuikabili mitihani ya kitaifa.

“Wanafunzi walikuwa wakifanya mitihani ya kujifua. Pia tulizingatia muda wa masomo,” amesema mkuu huyo wa shule aliyejawa na furaha ya mafanikio yaliyopatikana.

Shule ya wavulana ya Ilboru imeingia 10 bora kitaifa baada ya kutokuiona orodha hiyo kwa miaka 10 iliyopita. Picha|Ilboru Sekondari.

Huenda uboreshaji wa miundombinu ya shule kongwe za sekondari uliofanywa na Serikali miaka ya hivi karibuni, utakuwa umechangia ufaulu mzuri wa shule hiyo.

Wataalam wa elimu wanabainisha kuwa ili mwanafunzi afanye vizuri katika masomo yake anahitaji mazingira rafiki na miundombinu iliyoboreshwa ya kusomea ikiwemo madarasa na vifaa vya kujifunzia na kufundishia.

Mwaka 2019, Serikali ilitoa zaidi ya Sh42 bilioni kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya Sekondari 42 kati ya shule 88 kongwe zilizopo nchini kote ikiwemo shule ya Sekondari ya Ilboru.

“Dhamira yetu ni kuona watoto wetu wanasoma kwenye mazingira sahihi na ufaulu wao unaongeeaka kwa sababu tunawaandaa wataalam wa kesho wa Taifa letu,” alisema Naibu Waziri wa Fedha na Mipango wa wakati huo, Dk Ashatu Kijaji alipotembea Shule ya Sekondari ya Ruvu iliyopo mkoani Pwani Februari 2019.

Enable Notifications OK No thanks