Hivi ndivyo unavyoweza kufanya utalii ukiwa angani Tanzania
- Ni utalii wa kupanda puto linaloendeshwa na mashine kukutembeza katika mbuga za wanyama.
- Unaweza kufanya safari za utalii huo katika Hifadhi za Taifa za Ruaha, Serengeti na Tarangire.
- Pia ni fursa kwa wawekezaji kuwekeza katika aina hiyo ya utalii katika hifadhi mbalimbali nchini.
Dar es Salaam. Kwanini uishie kuyaangalia kwenye filamu na picha za mtandaoni wakati unaweza kupanda na kufurahia safari yake mwenyewe tena hapa hapa nchini bila hata haja ya kukwea pipa?
Ndiyo, huenda umewahi kusikia juu ya utalii kwa njia ya maputo ( au hata kutazama kwenye filamu, lakini unahitaji kufahamu kuwa utalii huo umekufikia nchini Tanzania tangu mwaka 1989.
Kama wewe ni mdau, ni muhimu kufahamu kuwa hadi sasa, unaweza kufanya safari za utalii huo katika Hifadhi za Taifa za Ruaha, Serengeti na Tarangire.
Huko utaona kwa urahisi wanyama na mimea mbalimbali ukiwa angani ambao ni vigumu kuwaona ukiwa kwenye gari la watalii.
Hata hivyo, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) imeendelea kutoa miongozo kwa ajili ya watu binafsi kuwekeza katika utalii huo ambao ni kivutio kikubwa cha watalii duniani.
Endapo haufahamu ni wapi unaweza kuwekeza kwenye utalii huu, Tanapa imeainisha kuwa hilo linaweza kujadiliwa na uongozi wa hifadhi na kushauri stesheni za maputo ni vizuri zikakaa karibu na ofisi za utawala za hifadhi husika ili kufuatilia uendeshaji wake.
Zaidi, ili kufanya shughuli hizi, unahitaji leseni itakayotolewa kwa mtu atakayepata tenda hiyo. zaidi uzoefu wa rubani ni kigezo moja wapo.
Zinazohusiana
- Hoteli zaanza kufungwa kuepuka Corona Tanzania
- Waziri Kanyasu ataka tathmini ifanyike ajira hoteli za kitalii Tanzania
- Umemejua unavyoweza kuzinufaisha hoteli Tanzania
Hata hivyo mtu huyo atapata nafasi hiyo endapo amekidhi vigezo vya mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) huku mkataba unaodumu kwa miaka mitano ukisainiwa baina yake na Tanapa.
Pamoja na hayo, Tanapa imetoa angalizo kuwa shughuli hizo hazitoruhusiwa kufanyika kwenye maeneo ya nyumba za wafanyakazi au watalii.
Pia zitafanyika kwenye urefu wa mita 30 kwenda juu na mwekezaji kutakiwa kutoa taarifa wakati akirusha puto au kufanya mabadiliko yoyote.
Unasubiri nini kuwekeza katika utalii huo ilinkujipatia kipato? Hata kama hauwezi kuwekeza lakini una fursa ya kupanda puto hilo huku ukishuhudia mandhari nzuri za asili za hifadhi za wanyama Tanzania.