MOI kuanza upasuaji wa ubongo kwa teknolojia ya kisasa

Mwandishi Wetu 1032Hrs   Julai 29, 2019 Teknolojia
  • Inahusisha kuondoa uvimbe kwenye ubongo kupitia kwenye tundu la pua na mishipa ya damu bila kufungua fuvu kwa kutumia teknolojia ya ‘Angio Suite’.
  • Itapunguza rufaa za wagonjwa kufuata matibabu ya ubongo nje ya nchi.
  • Manunuzi na ufungaji wa mitambo hiyo kukamilika Oktoba 2019. 

Dar es Salaam. Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) inakusudia kuanza kutumia teknolojia ya kisasa ya upasuaji wa  kuondoa uvimbe kwenye ubongo kupitia kwenye tundu la pua na mishipa ya damu bila kufungua fuvu la kichwa. 

Teknolojia hiyo ambayo kitaalam inajulikana kama ‘angio Suite’ inahusisha  upasuaji  kwa njia ya matundu ya pua na mishipa ya damu hadi kwenye ubongo na kurekebisha tatizo kwa kusaidiana na mashine za ‘Ultrasound’. 

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile ameweka wazi azma hiyo ya MOI  leo (Julai 29, 2019) wakati akifungua kongamano la kimataifa la mafunzo ya upasuaji wa uvimbe wa kansa za Ubongo na uti wa Mgongo kwa kutumia teknolojia  ya kisasa.

Amesema Serikali tayari imetoa fedha kwa ajili ya kununua na kusimika mitambo ya teknolojia hiyo katika taasisi ya MOI iliyopo chini ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH). 

“Serikali imetoa fedha kiasi cha Sh7.9 bilioni kwa ajili ya kununua na kusimika mitambo ya kisasa ya upasuaji wa ubongo ya ‘Angio Suite’ tunaamini kabla ya mwisho wa mwaka itaanza kazi maana wataalamu wapo tayari ambao Serikali iliwapeleka nchini China kupata mafunzo hayo,” amesema Dk Ndugulile. 

Kongamano hilo ambalo linalenga kuwajengea uwezo wataalam wa afya kutumia teknolojia ya kisasa katika shughuli za matibabu hasa ya ubongo n auti wa mgongo limeandaliwa kwa ushirikiano wa MOI na Chuo Kikuu cha Colorado cha Marekani.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini  wa MOI, Profesa Charles Mkony ameishukuru Serikali kwa kuendelea kufanya uwekezaji wa miundombinu ya MOI, jambo ambalo limesaidia kuboresha huduma za taasisi hiyo  na kumaliza rufaa za nje ya nchi.


Inayohusiana: Teknolojia ya kisasa kuongeza ufanisi matibabu ya figo Muhimbili


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na MOI, mchakato wa kununua na kufunga maabara ya kisasa ya upasuaji wa ubongo ya ‘Angio Suite’ utakamilika kabla ya Oktoba ambapo huduma zitaanza kabla mwaka huu haujaisha.

“Kuanza kwa huduma hizi za upasuaji wa ubongo kwa teknolojia ya kisasa kutaleta mageuzi makubwa kwenye utoaji huduma za upasuaji wa ubongo kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati kwani hakutakua na haja kwa wagonjwa kuzifuata huduma hizo nje ya nchi.

“Utakua upasuaji ambao unahusisha kupitia kwenye mishipa ya damu hadi kwenye ubongo na kurekebisha tatizo bila kufungua fuvu,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Respicious Boniface.

Kongamano hilo linahudhuriwa na zaidi ya madaktari 100 kutoka katika mataifa ya Kenya, Uganda, Rwanda, Sudan, Ethiopia pamoja na mataifa mengine kutoka katika nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile ameweka wazi azma hiyo ya MOI  leo (Julai 29, 2019) wakati akifungua kongamano la kimataifa la mafunzo ya upasuaji wa uvimbe wa kansa za Ubongo na uti wa Mgongo kwa kutumia teknolojia  ya kisasa.

Related Post