Hatua kwa hatua: Mahitaji, namna rahisi ya kutengeneza nywele asilia

August 13, 2020 1:24 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Unapoosha nywele zako, hakikisha umeandaa nguo ya kukaushia ambayo ina malighafi ya pamba.
  • Hakikisha unatenga muda wa kutosha kwa ajili ya kuhudumia nywele zako walau mara mbili kila mwezi.
  • Nywele za kiafrika ni nzuri na kwa muda mrefu wanawake wameaminishwa tofauti. Niwakati wa kujikubali.

Dar es Salaam. Pamoja na mtindo wa nywele asilia kuendelea kupendwa na wanawake wengi, matokeo mazuri ya mtindo huo yanatokana na umakini na kufuata kwa undani hatua kwa hatua katika kuzitunza. 

Katika makala haya leo tunaangazia undani wa matunzo ya nywele asilia na umuhimu wa kufanya hivyo. 

Kutofuata masharti kwa kina ya kutunza nywele asilia kumewafanya wengi kushindwa na kurejea kwenye nywele za dawa, ambazo baadhi ya wataalamu wa afya wanashauri kuwa siyo nzuri kiafya. 

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini kampasi ya Dar es Salaam (TUDARCo) Deodetha Balile anasema kutunza nywele zake hutumia asali, ndizi au parachichi na yai la kienyeji kwa kila Jumapili mbili kwa mwezi.

“Ninavisaga kwa pamoja kisha napaka. Nakaa nayo kwa saa moja baada ya hapo nazisuuza na kukausha kwa blow drier. Zikikauka napaka mafuta tu kisha nabana tayari kwa kutoka,” anasema Deodetha na kuanisha kuwa mlolongo wote huo hutumia saa moja na nusu na gharama yake, “haifiki hata Sh10,000”.

Kama ilivyo kwa Deodetha, mkazi wa Mbeya mjini,  Rachel Essau anasema hutumia malighafi zikiwemo parachichi, kitunguu swaumu, kitunguu maji, na bamia. 

“Njia hii haina madhara kwa mtumiaji (chemical free) na upatikanaji wake ni wa urahisi hata mtu wa kijijini anaweza kutumia njia hii,” anasema Rachel.

Rachel, ambaye nywele zake za asilia zinafika mabegani kwa sasa, anasema kuna aina nyingi za steaming (chakula cha nywele) za asili mfano steaming ya parachichi hujulikana kama steaming ya protini.

“Nywele zetu zimeundwa na na protini inayoitwa “Keraten” ambayo huzipa nguvu nywele zisikatike upungufu wa “keratin” hufanya nywele ziwe dhoofu na nyepesi na kukatika kwa wepesi,” anaongeza Rachel ambaye kwa sasa amebobea katika mtindo huo wa nywele. 

Kutofuata masharti kwa kina ya kutunza nywele asilia kumewafanya wengi kushindwa na kurejea kwenye nywele za dawa. Picha| Josephine Nelson/TUDARco.

Undani wa mchanganyiko wa parachichi

Kwa mujibu wa Rachel yeye hutumia Parachichi lililoiva sana, asali na wakati mwingine akipenda hutumia maziwa.

 Anasema ukimaliza kupaka mchanganyiko huo wa kichwani, utachukua kofia za kuogea ambazo ni za nailoni utafunika nywele zako na kusubiri kwa dakika 45.

Baada ya hapo, huosha nywele zake kwa shampoo (sabuni ya nywele). 

Rachel anasema usitumie sabuni ya kipande na kama utapata maji ya vuguvugu kwa ajili ya kuoshea nywele, ni vyema zaidi.

Msisitizo wa Rachel ni kuwa ukimaliza kuosha nywele zikaushe kwa kutumia nguo yenye malighafi ya pamba kama T-shirt, taulo au khanga.

“Usitumie mashine ya kukaushia nywele (blow dryer) au pasi. Si salama zinaua Keratin ya nywele. 

Baada ya nywele kukauka, Rachel anasema unaweza kupaka mafuta ya maji kama ya mzaituni (Olive oil), mafuta ya nazi au mafuta ya mnyonyo (Castrol oil).


Zinazohusiana:


“Mafuta ya mgando si rafiki wa nywele”

“Mafuta ya mgando hayashauriwi kupaka kwenye nywele yanafanya nywele kunata na pia hayaingii mpaka ndani ya nywele,” anashauri Rachel.

Katika mchakato huo wa kuandaa nywele, hutakiwi kuwa na mapepe yaani shughuli nyingi kwa wakati huo ili kuhakikisha unafuata msharti yote kikamilifu. 

Salama Masoud, ambaye ametunza nywele zake asilia kwa muda sasa, anasema watu wengi wanaotunza nywele asilia wana kitu kinaitwa “Wash day” yaani siku maalumu ambayo unatakiwa kusahau kila kitu na kuweka makini yako katika nywele zako.

Salama, ambaye hujishughulisha na biashara ya maua jijinii Dar es Salaam anasema siku hiyo inatumika kuosha nywele zako, kuzifukiza (steaming), kuosha tena na kuzipa kila huduma inayoshauriwa.

“Siyo rahisi, lakini kama unafahamu unachotaka, ni kitu kidogo. Kuna raha ya kushika kichwa ukijua unashika nywele zako na siyo za mmea au kiumbe mwingine,” anasema Salama.Kuna raha ya kushika kichwa ukijua unashika nywele zako na siyo za mmea au kiumbe mwingine| Picha Leyla Siraj/TUDARCo.

Kuwa makini na nywele zako, usikurupuke

Mtaalamu wa nywele kutoka saluni ya Wealthy Style iliyopo Sinza jijini Dar es Salaam, Caren Hezron anasema ili kufahamu aina ya nywele yako ni muhimu kufika kwa wataalamu kwa kuwa siyo kila nywele zinaweza kushamiri kwa kutumia bidhaa za nyumbani pekee.

Caren anasema kuna aina nyingi za nywele za kiafrika lakini Watanzania wengi wana nywele zinazoitwa “4C” ambayo mara nyingi siyo nyeusi na siyo imara.

“Hata mimi nywele zangu hazifanyi vizuri nikitumia bidhaa za asili lakini zinafanya vyema nikitumia bidhaa za dukani. Ninaweza kupaka maparachichi na nika kaa nayo masaa na masaa na yasifanye chochote,” anasema Caren.

Mtaalamu huyo anashauri kama unahitaji kuanza safari yako ya kutunza nywele asilia ni muhimu kutembela saluni za wataalamu wa nywele asilia na kufahamu nywele zako zinahitaji nini na siyo kuanza “kujikandika maparachichi”. Tafuta taarifa nyingi zaidi kuhusu aina ya nywele zako ili kupata matokeo mazuri. 

Je, unawezaje kuandaa steaming ya protini kwa ajili ya nywele zako?

Dhana potofu zilizojengeka katika utunzaji wa nywele asilia

Kutokana na kuwepo kwa nadharia mbalimbali za uongo kuhusu utunzaji wa nywele zikiwemo za nywele asilia kutokuwa nzuri, kuwa ngumu ndiyo sababu ya baadhi ya watu kuamua kurudia nywele za dawa au kuamua kunyoa na kuvaa mawigi. Hata hivyo, wadau wa nywele asilia wameona siyo busara kukaa na hisia zao juu ya nywele zao na hivyo kongea na Nukta.

“Kwa miaka mingi tumeaminishwa kwamba ili uonekane mrembo, lazima uwe na nywele laini, ndefu na zenye mfanano na umagharibi. Kiuhalisia, Nywele zako ni asili na utambulisho wako. Ni nzuri sana endapo utazipenda na kuzitunza. Amesema Lucy Protas Mwasisi wa jukwaa la Sports for Change ambaye amekuwa na nywele za asili kwa miaka nane sasa.

Naye Mkuu wa Oparsheni kutoka kampuni ya A trader Dar es Salaam, Fadhila Ahmad amesema watu wengi wanafikiri nywele za kiafrika hazirefuki. “Zinarefuka cha msingi ni matunzo tu,” amesema Fadhila ambaye nywele zake zinamfikia kifuani licha ya kuwa na tabia ya kuzikata kila mwaka.

Kwa mujibu wa fadhila, nywele za kiafrika zinachukua mifumo mingi na hiyo ni bahati kubwa.

“Nywele za kiafrika zikiloa zinajikunja na kuwa fupi, zikikauka zinarefuka na hiyo inakupatia uhuru juu ya muonekano wako,” amesema fadhila ambaye pia amesema siri yake kubwa ya utunzaji nywele ni maji.

Makala inayofuata, itakueleza uzuri na ubaya unaoambatana na matumizi ya dawa za nywele. Usikose.

Enable Notifications OK No thanks