Hatma ya wafanyabiashara soko la Simu 2000 kujulikana Julai 13

July 8, 2024 12:32 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila awatuliza wafanyabiashara.
  • Amesema suluhu ya malalamiko itapatikana Jumamosi.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amesema hatma ya wafanyabiashara soko la Simu 2000 walioandamana kupinga kuhamishwa katika maeneo yao ya biashara kupisha ujenzi wa karakana ya mabasi yaendayo haraka (Mwendokasi) itajulikana Julai 13 mwaka huu.

Chalamila aliyekuwa akizungumza na waandamanaji hao leo Julai 8, 2024 katika Soko la Simu 2000 lililopo Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam amewataka kuendelea na kazi mpaka siku ya jumamosi watakapofanya kikao cha pamoja.

“Leo ni Jumatatu hebu nawaomba muendelee na kazi zenu alafu Jumamosi nakuja nataka nikamsikilize mtu wa DART (Wakala wa Mabasi Yaendayo haraka) nikamsikilize mtu wa LATRA (Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini), nimsikilize wa Halmashauri ya Ubungo…

..Halafu kwa kuwa sio siri Jumamosi nikija, waje na wao wanieleze mbele yenu wanachotaka kukifanya na namna wanavyojali na kutaka kupuuza maslahi ya wafanyabiashara,” amesema Chalamila.


Soma zaidi:Debunked: Kenyan MP’s did not eat in the bush following bill protest


Kauli ya chalamila imekuja ikiwa ni takribani saa nne tangu waandamanaji hao ambao ni wafanyabiashara wadogo wadogo wa soko la Simu 2000 waingie barabarani kupinga hatua ya Manispaa ya Ubungo kukabidhi eneo hilo lenye ukubwa wa mita za mraba 36,000 kwa DART kwa ajili ya kujenga karakana ya mabasi yake, mbadala wa ile iliyopo Jangwani, jijini Dar es Salaam.

Wafanyabiashara hao pia walifunga biashara zao, na kuingia barabarani wakibeba mabango yenye jumbe mbalimbali yakishinikiza Serikali kuyatupia macho malalamiko yao.

Aidha, Chalamila ametuliza waandamaji kwa kukiri uwepo wa malalamiko ya wafanyabiashara hao licha ya kutopokea kibali rasmi kutoka kwa mamlaka husika kutekeleza azimio hilo.

Hii ni ya mara ya pili kwa wafanyabiashara kuandamana ndani ya kipindi cha mwaka mmoja nchini Tanzania huku madai yakipishana kiduchu au kufanana na yale yanayojitokeza katika maandano yaliyotangulia.

Juni 24 mwaka huu pia wafanyabiashara wa Soko la Kimataifa Kariakoo waliandamana kuishinikiza  Serikali kutatua kero zao ikiwemo utitiri wa kodi, biashara ndogo za wazawa kufanywa na wageni  pia usumbufu wa maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Enable Notifications OK No thanks