Rais Samia aitaka tume kuleta viwango halali vya kodi Tanzania

October 4, 2024 6:13 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Inatakiwa kufanya tathmini ya mfumo wa kodi na tozo nyingine na kutoa mapendekezo ya maboresho
  • Imeundwa kwa kuzingatia mrejesho na mawazo mbalimbali ya wananchi, wadau wa sekta binafsi na wawekezaji.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameielekeza tume iliyoteuliwa kufanya tathmini ya mfumo wa kodi nchini kuhakikisha inapata viwango stahiki vya kodi vitavyokubalika na walipa kodi kwa haki bila malalamiko ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.

Mapema Julai 31, 2024 mkuu huyo wa nchi aliunda Tume ya Rais ya Kufanya Tathmini ya Mfumo wa Kodi ili kuboresha ufanisi katika ukusanyaji mapato na kuongeza uhusiano bora na walipa kodi.

Wakati wa uzinduzi wa tume hiyo leo Oktoba 4, 2024 Ikulu Dar es Salaam Rais Samia amesema kodi ni damu ya Serikali hivyo tume hiyo, iliyoundwa na wajumbe wenye uzoefu wa masuala ya kodi, inatakiwa kupata viwango halisia vya kodi kwa kila mtu anayetakiwa kulipa malipo hayo.

 “Hakuna mlipa kodi, mtu anaefanya biashara, kazi, anaepata mapato aachiwe asilipe kodi ya nchi,” amesema Rais Samia.

Agizo hilo lililolenga mifumo ya sera za kodi na kanuni za usawa katika mifumo ya ukusanyaji wake limeweka wazi kwamba kila mtu anapaswa kulipa kiwango sawia cha kodi kinachozingatia usawa na kinachokubalika kisheria kulingana na ukubwa wa biashara yake.

“Jambo kubwa na la msingi kwetu ni kwamba tunataka kujenga mfumo wa kodi unaotenda haki ambapo kila mmoja anaepaswa kulipa kodi alipe kodi stahiki na kodi zote zitozwe kwa mujibu wa sheria,” amesema kiongozi huyo. 

Katika hotuba hiyo, Rais Samia amesema wanataka mfumo wa kodi unaochochea ukuaji wa uchumi wa viwanda na utakao changia ukuaji jumuishi na unaoiwezesha Serikali kutimiza malengo yake ya kuleta ustawi wa wananchi.

Wajumbe wa tume hiyo wanaongozwa na Mwenyekiti wake ambaye ni Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu Balozi Ombeni Sefue akiwa na wajumbe wengine mashuhuri kwenye masuala ya kodi wakiwemo Prof Florance Lwoga aliyewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania na Balozi Maimuna Tarishi.

Wajumbe wengine ni Balozi Mwanaidi Sinara, Leonardi Msusa, Prof Mussa Assad aliyewahi kwa CAG, David Tarimo, CPA Muhamad Abubakar na Kamishna Mkuu wa TRA wa zamani Rished Bade.

Jukumu la msingi la tume hiyo ni kufanya tathmini ya mfumo wa kodi na tozo nyingine na kutoa mapendekezo ya jinsi ya kuboresha ili kuondoa malalamiko kuhusu mfumo wa kodi, tozo na kuboresha mazingira ya biashara ili kuvutia mitaji na uwekezaji.

Katika utekelezaji wa majukumu yake tume hiyo itafanya kupitia mazungumzo na wadau wote muhimu wa kodi, kufanya vikao na mikutano na makundi mbalimbali na wananchi, kupokea taarifa kutoka kwa wananchi pamoja kupitia mifumo ya taasisi zinazokusanya kodi na maduhuli kwa lengo la kubainisha changamoto.

Rais amesema uchumi wa Tanzania unaendelea kukua kwa kasi lakini ni kinyume na uhalisia wa ukusanyaji wa mapato yanayopaswa japo ukusanyaji umeongezeka kufikia Sh3 trilioni Septemba 2024 kutoka wastani wa makusanyo ya Sh2 trilioni kwa mwezi ndani ya mwaka 2022/23.

Kwa nyakati tofauti kumekuwa na malalamiko lukuki kutoka kwa walipa kodi kuhusu wingi wa kodi na tozo, viwango visivyo rafiki, mchakato wa muda mrefu wa ulipaji kodi, kutozingatia weledi wakati wa ukusanyaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks